Mazoezi Simba yamduwaza Mzungu Yanga



Jamhuri Kihwelu �Julio�
KOCHA mwenye maneno na mbwembwe nyingi, Jamhuri Kihwelu �Julio�, jana Jumatatu alitua rasmi Simba na kufanya mambo ambayo yalimshitua Mholanzi wa Yanga, Ernest Brandts na msaidizi wake Fred Felix `Minziro�. 

Julio ambaye amerudi Simba akishika nafasi ya Meneja ingawa Mwanaspoti linajua bado hajasaini mkataba, alianza programu yake kwa kuipeleka timu kwenye ufukwe wa Coco ambako aligongana na Yanga ya Brandts. 

Simba walianza matizi kwenye ufukwe huo majira ya saa moja asubuhi na dakika chache baadaye Brandts akatua na Yanga yake na kuduwaa dakika chache akishangaa kuiona Simba ikijifua upande wa pili wa ufukwe huo chini ya Julio ambaye atafanya majukumu hayo akisaidiana na Richard Amatre mpaka Kocha Mkuu Mfaransa Patrick Liewig atakapowasili baadaye mwezi huu. 

Minziro alisema: �Hii haijawahi kutokea lakini kwa upande wangu nachukulia kitu cha kawaida. Nasema hivyo kwa sababu sisi tulipanga tangu Ijumaa tufanye mazoezi ufukweni labda na wao walikuwa na programu kama hiyo.� 

James Kisaka, ambaye ni kocha wa makipa wa Simba alisema: �Ni vitu ambavyo haviepukiki na ukizungumzia ufukwe, una sehemu kubwa kama hivyo sisi tumefanya upande wetu na wao wamefanya upande wao.� 
Simba walifanya mazoezi yao upande wa kushoto na Yanga upande wa kulia. 

Simba 
Walifanya mazoezi tofauti na zaidi ilikuwa kukimbia, kuchezea mpira na viungo walifanya kidogo. Julio kama kawaida yake baadaye akawaweka chini wachezaji na kuwapa somo. 

Aliwaambia: �Mnajua hii ni kazi na kila mtu afahamu anachokifanya. Kubwa na la msingi ni nidhamu katika mazoezi. Ukifanya mchezo katika hili hauwezi kufanikiwa. 

�Lengo ni kuhakikisha tunakuwa vizuri na kupata pointi za kufidia ili kuwapita wenzetu hao Azam na Yanga.� 

Julio ambaye aliwahi kuichezea timu hiyo miaka ya nyuma na kisha baadaye kuifundisha, hivi karibuni alijigamba asingekubali kuwa deiwaka kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. 

Hata hivyo hiyo jana Jumatatu alianza kazi bila ya kuingia makubaliano rasmi. 

Simba imemaliza mzunguko wa kwanza Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa nafasi ya tatu, ina pointi 23. Azam ni ya pili ikiwa na pointi 24 na Yanga ndiyo inaongoza msimamo kwa pointi 29. 

Amatre alisema: �Tuko kwa mazoezi haya ya ufukweni baada ya kumaliza ya gym. Baadaye tunaingia uwanjani kwa ajili ya mambo ya ufundi.� 
Katika mazoezi hayo, Mussa Mudde, raia wa Uganda, Mmali Komanbilli Keita na Henry Joseph anayekipiga klabu ya Kongsvinger ya Norway ni miongoni mwa wachezaji wenye majina makubwa waliokuwapo huku Emmanuel Okwi wa Uganda pamoja na wachezaji wa Taifa Stars wakikosekana. 

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Nyange Kaburu alikuwa mazoezini kuhakikisha mambo yanakwenda sawa wakati wakimsubiri Kocha Mfaransa ambaye wamesema watampa mkataba wa miezi sita na Kocha Mganda Moses Basena atarejeshwa kikosini kama Mkurugenzi wa Ufundi. 
Keita ametoa kauli nzito Simba baada ya kusema: �Sitaki mchezo kabisa, nimekuja kufanya mambo makubwa. 

�Nimejipanga na naamini nitafanikiwa kwa sababu penye nia pana njia na kikubwa namwomba Mungu anilinde na majeruhi.� 

Mussa Mudde alisema: �Namshukuru Mungu nimepona kabisa na sasa ni kazi tu. Nimejipanga sana.� 

Keita na Mudde ndiyo wachezaji pekee wa kimataifa waliokuwa wakifanya mazoezi na kikosi chao cha Simba jana Jumatatu. 

Yanga 
Walikuwa chini ya Brandts, Minziro na kocha wa makipa, Mfaume Athuman. Wao walikuwa tofauti kidogo kwani walichezea mpira zaidi. Mazoezi ya viungo na kukimbia walifanya kidogo tu. 

Brandts alisema kuwachezesha mpira ndio kitu cha kimsingi zaidi kwani pamoja na kufanya mazoezi ya viungo wakiwa wanachezea mpira kuna vitu wapata. 

�Mazoezi ya ufukweni ni kwa ajili ya kujiimarisha kwa stamina, lakini wakati tunaitengeneza hiyo tunakimbia kwa kutumia mpira ndiyo kama hivyo zaidi tunacheza.� 

Hata hivyo, sio cha kushangaza kwa wale wanaofuatilia soka kwani wana kawaida ya kuchezea mpira zaidi kuliko mazoezi ya nguvu. 

Mathalani kocha wa timu ya taifa ya Uholanzi, Louis Van Gaal hupendelea wachezaji wake kufanya mazoezi ya viungo kwa kutumia mpira zaidi. 
Van Gaal anaamini mchezaji akichezea mpira kwa muda mrefu ina maana atauzoea zaidi na kuongeza uwezo na ufanisi wake katika kuumiliki. 
Wachezaji wa Yanga ambao walikuwa wengi kuliko wa Simba mbali na kufanya mazoezi mazito zaidi walirushiana mipira wakati fulani huku vijembe na masihara vikitawala. 

Mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara unaendelea Januari 19 mwakani. 
Yanga inatazamiwa kujipima nguvu na Tusker ya Kenya Desemba 26 jijini Dar es Salaam itaondoka nchini Desemba 28 kwenda Uturuki kwa kambi ya mazoezi ya wiki mbili na Mwanaspoti linajua itakaa kwenye ufukwe wa Antalya ambao uko kando kando ya Bahari ya Mediterenean  Chanzo:- http://www.mwanaspoti.co.tz
 

Post a Comment

Previous Post Next Post