
KOCHA wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Kim Poulsen
KWA UFUPI
Ulimwengu na Samata wanadaiwa kushindwa kujiunga na wenzao kwenye kambi ya mazoezi kwa sababu ya kuwa majeruhi.
WAKATI kocha wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Kim Poulsen akisimama kwenye mstari wa uamuzi wa kutowatumia Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu kwenye mechi dhidi ya Zambia, wachezaji hao wamemwangukia na kumwomba radhi.
Stars inaikaribisha Chipolopolo ya Zambia mwishoni mwa wiki hii katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kim aliyechukizwa na kitendo cha wachezaji hao kushindwa kujiunga na wenzao kujiandaa na mchezo huo, amekubali kuwasamehe, lakini akisisitiza hatawatumia kwenye mchezo huo.
Akizungumza na Mwananchi jana, Poulsen alisema yeye kama mzazi hapendi kuona watoto wanakosea, lakini hata hivyo ameamua kuwasamehe nyota hao wanaocheza timu ya TP Mazembe ya DRC.
“Msamaha wangu hauhusiani na mechi ya Zambia. Nitawatumia wachezaji waliofanya mazoezi na wenye afya nzuri. Ingawa [Samata na Thomas] wako kambini na wana nia ya kucheza, lakini hilo haliwezekani kwa sasa,” alisisitiza Poulsen.
Ulimwengu na Samata wanadaiwa kushindwa kujiunga na wenzao kwenye kambi ya mazoezi kwa sababu ya kuwa majeruhi.
Kutojiunga kwenye kambi ya Stars kulimkera Poulsen ambaye mwanzoni mwa wiki hii alitoa kauli kali ya kuwashutumu akisema wamekosa uzalendo na mapenzi kwa timu ya taifa.
Akizungumza na gazeti hili jana Samata, alisema ana mapenzi makubwa na Stars na kwamba mashabiki wasimhukumu kwa kilichotokea.
Samata alitua nchini tangu Desemba 12 akitoka DRC na kutakiwa kuripoti kambi ya Stars haraka, lakini hakufanya hivyo mpaka aliporipoti Jumanne.
Samata amesema ni kweli yeye mgonjwa wa malaria, lakini pia anasumbuliwa na maumivu ya bega ya muda mrefu.
“Nilimtuma ndugu yangu atoe taarifa za kuchelewa kwangu kuripoti, kwa sababu nilikuwa natumia muda mwingi kwenda hospitali hivyo ingekuwa usumbufu kwa wenzangu kambini,” alisema.
“Ningependa Watanzania kutonifikiria vibaya, binafsi nina mapenzi makubwa na timu ya taifa na najisikia vibaya ninaposhindwa kucheza,” alisema Samata.
Aliongeza: “Siwezi kuidharau nchi yangu, wala sijawahi kuwa na mawazo kama hayo kwa sababu tu mimi ni mchezaji wa kulipwa.
“Nimeweza kupata mafanikio nikitokea nyumbani (Tanzania), sasa iweje leo nidharau sehemu iliyonikuza hata kupata mafanikio?”
Wakati huohuo; kikosi cha mabingwa wa Afrika, Zambia kimewasili jana jioni kikiwa na wachezaji wake wote tayari kwa mchezo wa Jumamosi dhidi ya Tanzania utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
إرسال تعليق