Na Hassan Ali, Zanzibar
MELI za mitumba zilizotumika kwa muda wa miaka 15 hazitosajiliwa au
kupewa lesseni ya kuchukua abiria na mizigo visiwani Zanzibar.
Hatua hiyo imechukuliwa na serikali
kufuatia muswada wa marekebisho ya sheria namba 5 ya mwaka 2006
unaotarajiwa kuwasilishwa katika kikao cha Baraza la Wawakilishi
Zanzibar (BLW) Januari mwakani.
Marekebisho hayo ya sheria yamekuja kufuatia ajali mbili za kuzama meli
katika mwambao wa Zanzibar na kusababisha mamia ya wananchi kupoteza
maisha na wengine kutoweka baharini mwaka 2011 na mwaka huu.
Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano
Zanzibar, Rashid Seif Suleimani, anatarajia kuwasilisha muswada huo
ambao umeanza kulalamikiwa na baadhi ya wawekezaji katika sekta ya
usafirishaji baharini Zanzibar.
Kifungu cha 17 A(1) cha muswada huo kinasema: “Hakuna meli ambayo
itazidi umri wa miaka 15 tokea tarehe ya kutumika kwake, itakayosajiliwa
au kupewa lesseni kwa ajili ya kuchukua abiria na mizigo Zanzibar.”
Kwa mujibu wa muswada huo, chombo chochote cha usafiri kinachotua nchi
kavu, ikiwa asili ya utengenezaji si kwa ajili ya matumizi ya kuchukua
abiria, hakitosajiliwa au kupewa leseni kwa madhumuni ya kuchukua abiria
katika visiwa vya Zanzibar kwa sababu za kiusalama.
Waziri Seif alisema katika muswada huo kuwa, hakuna meli itakayosajiliwa
au kupewa leseni kwa madhumuni ya kuchukua abiria ndani ya Zanzibar
ikiwa imebadilishwa kutoka katika muundo asili wa utengenezaji wake.
Aidha, muswada unapiga marufuku wawekezaji katika sekta ya usafirishaji
kubadilisha muundo wa meli kama mashine za umeme, vyombo vya
mawasiliano, winchi au vitu ambavyo havitokani na muundo wake asilia.
Chanzo - Tanzania Daima
Post a Comment