
CHAMA cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepitisha mpango mkakati wake wa
kuelekea kushika dola mwaka 2015 kwa kumega madaraka ya makao makuu
katika kanda kumi.
Maazimio
hayo yalipitishwa na Kamati Kuu (CC) juzi kwa agenda moja kubwa ambayo
ni kupitisha mpango mkakati wa mwaka 2013 ili kushinda chaguzi zote
kuanzia serikali za vitongoji, vijiji na mitaa mwaka 2014 na Uchaguzi
Mkuu 2015.
Akizungumza
na wajumbe wa kikao cha dharura cha Baraza Kuu jana, Mwenyekiti wa
CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema kuwa mpango mkakati huo umelenga kufanya
mabadiliko ya uongozi kuanzia ngazi ya taifa kwenda katika majimbo na
kukipanga upya chama hicho kwa mustakabali wa taifa.
“Mtakumbuka
kwamba wakati tunakianzisha chama chetu, tulizungumzia sera ya majimbo
na kuainisha kazi zake…sasa tumeanza kupanga kazi zenyewe kwa kugawa
majukumu katika kanda kumi.
“Tunataka
tuishi vile tunavyosema kwa kuwa katika miaka mingi ya kuwa chini ya
uongozi wa serikali ya CCM, wananchi wamekuwa wakiamriwa mambo yao na
kundi dogo la watu wanaojikusanya sehemu moja ya nchi, hilo kwetu si
mfano bora wa uongozi,” alisema.
Mbowe
aliongeza kuwa katika miaka 20 ya kuhimili misukosuko ya kisiasa chama
hicho kimejifunza mengi na sasa kiko tayari kushika dola ndio maana
wameanza kugawa majukumu kwa wananchi kupitia uongozi wa kikanda.
Alisema kuwa
wamejiandaa kwa mashambulizi ya aina zote na sasa jukumu kubwa la kila
kanda litakuwa ni kuhakikisha kila mwananchi anaiunga mkono CHADEMA
katika eneo atakalokuwa.
Mwenyekiti
huyo alitaja kanda hizo na mikoa husika kuwa ni Kanda ya Ziwa Magaharibi
(Mwanza, Geita, Kagera), Ziwa Mashariki (Mara, Simiyu, Shinyanga), Ziwa
Magharibi (Kigoma, Tabora, Katavi) na Kati (Singida, Dodoma, Morogoro).
Zingine ni
Kata za Nyanda za Juuu Kusini (Mbeya, Ruvuma, Iringa), Kusini (Lindi na
Mtwara), Mashariki (Pwani, Dar es Salaam na Tanga), Kaskazini
(Kilimanjaro, Manyara, Arusha), Pemba na Kanda ya Unguja.
Mbowe
alisema katika kuhakikisha vikosi hivyo vinafanya kazi zake vizuri, kila
kanda itajengewa ofisi, kununuliwa magari, pikipiki na vifaa vyote vya
ofisini na za mikutano.
“Lengo la
mkakati huo pia ni kuhakikisha CHADEMA inasimama katika chaguzi zote
bila kupingwa…tunataka CCM ndiyo ipingwe katika chaguzi na hili
tutalifanikisha,” aliongeza.
Katika suala
zima la Muungano, Mbowe alisema uwepo wa serikali tatu hauepukiki kwa
kuwa tayari Tanzania Visiwani wameshakuwa na serikali yao hivyo ni
jukumu la Watanzania Bara kupata serikali ya Tanganyika na kisha kuwepo
na serikali ndogo ya Muungano.
Alisema
serikali tatu inawezekana ikiwa viongozi wataacha unafiki wa kusema
muungano utavunjika huku tayari wakitoa uhuru wa Zanzibar kuwa na Rais,
bendera na wimbo wao ya taifa.
Tunawaunga
mkono wenzetu Wazanzibar katika kupigania uhuru kamili na kwa sasa sisi
ndio tunaoonekana wa ajabu kushindwa kuuliza serikali ya Tanganyika,”
alisema.
Mbowe pia
aligusia tume huru ya uchaguzi akisema serikali ihakikishe Watanzania
wanapata tume hiyo kwa kuwa tayari hata viongozi wa chombo hicho
wameshatoa maoni na kutaka wapewe uhuru wa kufanya kazi.
Alisema
serikali kama inafikiri kuwa CHADEMA itaingia katika uchaguzi wa 2015
ikiwa chini ya tume iliyopo sasa watakuwa wanajidanganya na badala yake
watalazimisha upatikanaji wa tume hiyo.
Wailiza CCM Kagera
Katika hatua
nyingine chama hicho kimeiliza CCM katika uchaguzi mdogo wa vijiji na
vitongoji uliofanyika wilayani Muleba mkoani Kagera Jumapili iliyopita.
Licha ya
wilaya ya Mulebe yenye majimbo mawili ya uchaguzi kusini na kaskazini
yakiwa chini ya CCM, CHADEMA imeweza kunyakuwa viti vingi vilivyokuwa
vikishikiliwa na chama hicho tawala.
Katika
uchaguzi huo CHADEMA ilinyakuwa vijiji vitatu kati ya vitano katika
jimbo la Muleba Kusini linaloongozwa na Prof. Anna Tibaijuka ambavyo ni
Kasenyi, Kabunga na Ihangilo.
CHADEMA pia
imechukua vitongoji sita vya CCM kati ya 12 vilivyofanya uchaguzi.
Vitongoji hivyo ni Nyamagojo, Mushumba, Nyakabingo, Kyamyorwa, Katanda
na Kyogoma.
Katika Jimbo
la Muleba Kaskazini, linaloshikiliwa na Charles Mwijage, CCM ilipoteza
vijiji viwili vya Katoke na Kahumulo kati ya vitano vilivyofanya
uchaguzi huku vitongoji vinne vya Rundu, Kalee, Lwanganilo na Kituvi
vikiangukia kwa CHADEMA.
Akizungumza
na Tanzania Daima kwa njia ya simu kutoka Muleba, Katibu wa Baraza la
Vijana wa Taifa (BAVICHA), Robert Rwegasira, alisema wamepata ushindi
huo kutokana na wananchi kuanza kuwaamini.
Mafanikio
hayo yametokana na hamasa ya vuguvugu la mabadiliko la CHADEMA (M4C)
ambalo lilifanyika katika mkoa wa Kagera Novemba mwaka jana.
Katika jimbo
la Muleba Kusini, CHADEMA ingeweza kupata viti vya vitongoji zaidi ya
idadi iliyopata kwani walisimamisha wagombea tisa kati ya 12 huku nafasi
tatu wakiwaachia CUF na NCCR-Mageuzi ambao hawakuambulia chochote.
Post a Comment