Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene
SERIKALI imetaja manufaa na faida ambazo wanatarajia kuzipata
wananchi wa Mtwara pamoja na Lindi endapo gesi itasafirishwa kwenda
Jijini Dar es Salaam. Imesema Mkoa wa Mtwara ndipo utakapo jengwa mtambo
mkubwa wa kusafishia gesi hiyo kabla ya kusafirishwa kwenda jijini Dar
es Salaam kwa matumizi ya uzalishaji umeme na matumizi ya moja kwa moja
viwandani.
Kauli hiyo imetolewa jana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini,
George Simbachawene alipokuwa akizungumza katika Kipindi cha Dakika 45
kinachorushwa na Kituo cha Radio One jijini Dar es Salaam.
Naibu waziri huyo ameweka wazi kuwa mkoani Mtwara licha ya Serikali
kupanga kujenga viwanda vingine kadhaa, inajenga mtambo wa megawati 250
ambao utakuwa ukizalisha umeme na mwingine kujengwa mkoani Lindi eneo la
Somanga Funga utakao kuwa ukizalisha megawati 520.
Akifafanua zaidi Simbachawene alisema eneo la Mikindani katika Kijiji
cha Msijute mkoani Mtwara kinatarajiwa kujengwa kiwanda kikubwa cha
saruji Afrika Mashariki na Kati chenye uwezo wa kutoaji ajira kwa watu
6000 jambo ambalo ni manufaa ya Wanamtwara.
Alisema pia tayari kuna wawekezaji wa viwanda vya mbolea wamejitokeza
kujenga viwanda mkoani Mtwara na Serikali itaviacha vinu vya kuchimba
na kusindika gesi eneo hilo jambo ambalo bado ni manufaa makubwa kwa
wananchi.
“Viwanda vya kusindika gesi hii vimepangwa kujengwa maeneo ya Lubasi,
Kishere, Mchinga Bay, Lindi, Sudi Bay, Airport pamoja na
Mikindani…viwanda vyote hivi vitatoa ajira kubwa sana,” alisema Naibu
Waziri.
Alisema licha ya manufaa hayo, gesi itakapopelekwa Dar es Salaam
itazalisha umeme wa uhakika pamoja na kutumika moja kwa moja viwandani
jambo ambalo litailetea taifa tija kubwa ikiwa ni pamoja kupunguza ukali
wa maisha.
“Ni kweli gesi imepatikana Mtwara lakini ni lazima uipeleke sokoni
ili iweze kupata soko (wateja)…Dar es Salaam ndio kwenye soko, huwezi
ukaiacha Mtwara ambako hakuna soko; mbali na kuzalisha umeme kuna
viwanda 37 na hoteli kadhaa zinataka ziitumie moja kwa moja ni lazima
iletwe huku, Mtwara pale hakuna soko,” alisema.
Aidha alitolea mfano kuwa zipo nchi mbalimbali ambazo zimegundua gesi
lakini zimelazimika kuisafirisha kwa mabomba kwenda eneo la soko.
Alibainisha kuwa nchi ya Urusi inasafirisha gesi yake hadi nchini
Ujerumani huku Iran ikisafirisha hadi India gesi yake kutafuta soko
lilipo.
Alisema miundombinu mikubwa ya umeme ipo jijini Dar es Salaam hivyo
kuna kila sababu ya gesi hiyo kuletwa jijini humo ili iweze kuzalisha
umeme na matumizi ya viwandani moja kwa moja pamoja na matumizi mengine,
ambapo tayari wateja wamepatikana.
Aidha aliongeza kuwa uzalishaji umeme wa kutosha kwa kutumia gesi
utapunguza bei ya umeme na kuuzwa kati ya senti 6 na 8 za Marekani jambo
ambalo litapunguza ugumu wa maisha na pia bei ya bidhaa nchini.
Pamoja na hayo amevitaka baadhi ya vyama vya siasa na taasisi zisizo
za Serikali (NGO’s) zinazowapotosha Wanamtwara juu ya mradi huo kuacha
kitendo hicho kwani hakuna asiyejua umuhimu wa gesi hiyo kuja Dar es
Salaam.
“Hivi ni nani asiyejua kuwa tatizo la kutokua na umeme wa uhakika
nchini ndilo linalokwamisha uchumi wa nchi…Tanzania inapoteza bilioni
4.5 kwa ajili ya kununua mafuta ya kuzalisha umeme kwenye mitambo yake,
sasa gesi itaokoa fedha hizi,” alisema Simbachawene.
Hata hivyo amesema Serikali haiwezi utekeleza mradi huo kwa nguvu
bali itaendelea kuwaelimisha Wanamtwara umuhimu na manufaa ya gesi hiyo
kuletwa Dar es Salaam na inaimani wataelewa na malumbano kumalizika.
chanzo: http://www.thehabari
Post a Comment