DHARAU HAZITOSAIDIA KUTATUA MGOGORO WA GESI.


Baada ya majibizano ya hapa na pale kuendelea kwa muda mrefu baina ya Serikali, Wanaharakati na Wananchi wa Mikoa ya Kusini sasa inaonekana mgogoro huo kukua zaidi siku hadi siku. Ililipotiwa hapo kabla kuhusu Naibu Waziri wa Nishati kwenda usiku huko Msimbati na kufukuzwa, ingawaje Serikali kwa upande wake ilikanusha habari hiyo na kudai ni maneno ya kizushi na udanganyifu wa watu kujitafutia umaarufu.

Katika kile kinachoonekana kuwa ni hatari, asubuhi ya leo tumepata taarifa kwamba gari lililoenda kwa ajili ya kumbeba Bibi kwenda naye kusikojulikana limechomwa moto. Taarifa zinasema, watu kadhaa akiwemo kijana mmoja mwenye asili ya ukaazi wa kijiji hicho walikamatwa jana usiku na wanakijiji cha Msimbati wakidai wameagizwa kuja kumchukua Bibi huyo ili wakafanye maongezi na Wakubwa ambao pia hawakuweza kuwekwa bayana ni Wakubwa gani hao. Kinachoelezwa ni kwamba, baada ya mtafaruku huo, watu hao walichoropoka na kukimbia kitu kilichowapa hasira Wananchi na kuamua kuchoma gali hilo ambalo walikuja nalo.

Ni hatari, kwasababu mbali na propaganda za viongozi wetu wa Kitaifa kwamba suala la gesi ni la Wanamtwara Mjini tu, eti kwamba wenyewe wa Msimbati na Mtwara Vijijini kwa ujumla wako tayari gesi hiyo kupelekwa Dar es salaam, kumbe si kweli.

 Leo hii, wale wanaodaiwa kuwa tayari kuruhusu gesi hiyo wameteketeza gari, je wale wasio tayari kwa hilo kesho watafanya nini? Wananchi hao wamesema wako tayari kumlinda Bibi huyo usiku na mchana kwa kuhofia kurubuniwa na Serikali ili abadili simamo wake.

Serikali isidharau wananchi na wale wenye matakwa mema na nchi hii, kwani mbali na mamlaka ambayo serikali imepewa katika kusimamia rasilimali za nchi bado uhalali wa wamiliki asilia wa rasilimali hizo ambao ni wananchi hauwezi kuporwa. 

Wananchi wanaozungukwa rasilimali husika ndio wamiliki halali wa rasilimali hizo kabla ya Serikali na jamii zingine za nchi. Hivyo wanufaika wa kwanza wa rasilimali husika ni lazima wawe ni wale wenye uhalali wa Ki-asili na si vinginevyo.

Tuache dharau, leo gari limechomwa na kama hii hali itaendelea kuwa hivi tusishangae kuambiwa kunamtu pia kachomwa au kapoteza maisha kwasababu hizihizi zinazofanyiwa masihara na viongozi wetu. Tuweni wazalendo jamani, tutetee maendeleo ya nchi na watu wake kwa vitendo, tuache porojo.

Hassani Samli, Mtwara.

Post a Comment

Previous Post Next Post