Baada ya
majibizano ya hapa na pale kuendelea kwa muda mrefu baina ya Serikali,
Wanaharakati na Wananchi wa Mikoa ya Kusini sasa inaonekana mgogoro huo kukua
zaidi siku hadi siku. Ililipotiwa hapo kabla kuhusu Naibu Waziri wa Nishati kwenda
usiku huko Msimbati na kufukuzwa, ingawaje Serikali kwa upande wake ilikanusha
habari hiyo na kudai ni maneno ya kizushi na udanganyifu wa watu kujitafutia
umaarufu.
Katika kile
kinachoonekana kuwa ni hatari, asubuhi ya leo tumepata taarifa kwamba gari
lililoenda kwa ajili ya kumbeba Bibi kwenda naye kusikojulikana limechomwa
moto. Taarifa zinasema, watu kadhaa akiwemo kijana mmoja mwenye asili ya ukaazi
wa kijiji hicho walikamatwa jana usiku na wanakijiji cha Msimbati wakidai
wameagizwa kuja kumchukua Bibi huyo ili wakafanye maongezi na Wakubwa ambao pia
hawakuweza kuwekwa bayana ni Wakubwa gani hao. Kinachoelezwa ni kwamba, baada
ya mtafaruku huo, watu hao walichoropoka na kukimbia kitu kilichowapa hasira
Wananchi na kuamua kuchoma gali hilo ambalo walikuja nalo.
Ni hatari,
kwasababu mbali na propaganda za viongozi wetu wa Kitaifa kwamba suala la gesi
ni la Wanamtwara Mjini tu, eti kwamba wenyewe wa Msimbati na Mtwara Vijijini
kwa ujumla wako tayari gesi hiyo kupelekwa Dar es salaam, kumbe si kweli.
Leo
hii, wale wanaodaiwa kuwa tayari kuruhusu gesi hiyo wameteketeza gari, je wale
wasio tayari kwa hilo kesho watafanya nini? Wananchi hao wamesema wako tayari
kumlinda Bibi huyo usiku na mchana kwa kuhofia kurubuniwa na Serikali ili
abadili simamo wake.
Serikali
isidharau wananchi na wale wenye matakwa mema na nchi hii, kwani mbali na
mamlaka ambayo serikali imepewa katika kusimamia rasilimali za nchi bado
uhalali wa wamiliki asilia wa rasilimali hizo ambao ni wananchi hauwezi kuporwa.
Wananchi wanaozungukwa rasilimali husika ndio wamiliki halali wa rasilimali
hizo kabla ya Serikali na jamii zingine za nchi. Hivyo wanufaika wa kwanza wa
rasilimali husika ni lazima wawe ni wale wenye uhalali wa Ki-asili na si
vinginevyo.
Tuache dharau,
leo gari limechomwa na kama hii hali itaendelea kuwa hivi tusishangae kuambiwa
kunamtu pia kachomwa au kapoteza maisha kwasababu hizihizi zinazofanyiwa
masihara na viongozi wetu. Tuweni wazalendo jamani, tutetee maendeleo ya nchi
na watu wake kwa vitendo, tuache porojo.
Hassani
Samli, Mtwara.
إرسال تعليق