AFAFANUA CHIMBUKO LA MKATABA KATI YA
MAKANISA, SERIKALI
KWA mara ya
kwanza, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.
Willibrod Slaa, ameweka bayana chimbuko la mkataba wa makubaliano kati
ya serikali na makanisa, huku akiwasihi Watanzania kujiepusha na
malumbano yenye hisia za udini.
Dk. Slaa
alitoa tahadhari hiyo jana katika ufafanuzi wake aliouandika kwenye
mtandao wa kijamii wa Jamii Forum, kuhusu mkataba huo (Memorandum of
Understanding - MOU) kati ya Baraza la Kikristo Tanzania, Baraza la
Maaskofu Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema kuwa
amelazima kutoa ufafanuzi baada ya kuona mkataba huo umewekwa kwenye
mtandao wa kijamii, huku watu wengi wakiwa wanauzungumzia kwa kupotosha
ukweli wa jambo hilo, na kulihusisha na masuala ya udini.
“Kama
mnavyoona, mimi nilikuwa nafahamu historia yote, nafahamu MOU, lakini
sikuwa nayo. Mtu huwezi kujua kila kitu, na au kuwa na kila kitu, ‘we
need to complement each other’.
“Ninarudia
kuwaomba wenzangu, tumetumia muda mrefu sana kujadiliana kwa hisia ya
aina mbalimbali. Watanzania hatukuzoea huko nyuma kuulizana dini zetu,
wala kabila, wala ukanda. Haya mambo tukiyaendekeza taifa letu litakuwa
hatarini,” alisema.
Alisema
Watanzania wanapaswa kutambua kuwa, kubomoa ni kazi nyepesi, lakini
kujenga tena inachukua muda mrefu, na ni kazi ngumu, na wakati mwingine
hata ukifanikiwa huwezi kujenga kama ilivyokuwa.
Akifafanua
historia ya jinsi na kwanini MOU hiyo ilizaliwa, Dk. Slaa alisema kuwa
huko nyuma serikali ilitaifisha shule nyingi za madhehebu ya dini.
Kwamba
utaifishaji huo uliendana pia na ardhi, hasa ikizingatiwa kuwa wakati
huo shule zilijengwa kwenye maeneo ya madhehebu ya dini na papo hapo
kukiwa na kanisa, nyumba za mapadre na vitu vingine.
Alisema kuwa
kwenye miaka ya 1980, madhehebu yakataka warudishiwe ardhi yao, hasa
ambayo ina majengo mengine yasiyohusiana na shule hizo.
Dk. Slaa
alifafanua kuwa, mchakato wa mjadala ulishika kasi mwaka 1986 Baraza la
Maaskofu Katoliki (TEC), lilipopitisha azimio rasmi na kumtaka Katibu
Mkuu, awasiliane na serikali kuanzisha mchakato wa kufanya upembuzi na
kutenga ardhi ya shule rasmi, kutoka kwenye ardhi inayotumika kwa huduma
nyinginezo za madhehebu ya dini.
“Wakati huo
mimi (Dk. Slaa), ndiye nilikuwa Katibu Mkuu wa TEC baada ya kupokea
rasmi kazi hiyo Desemba1985. Wakati huo madhehebu yaliishakudai
yarudishiwe shule zao kwa kuwa zimegeuka kuwa aibu kwa kukosa ukarabati,
na ziko kwenye hali mbaya sana,” alisema.
Aliongeza
kuwa serikali ilikuwa imekataa ombi hilo kwa lengo la kuwa, shule hizo
zinawahudumia Watanzania wote bila ubaguzi, jambo ambalo ndilo lilikuwa
lengo kuu la utaifishaji, na sababu ya utaifishaji ilikuwa bado
inaendelelea.
Dk. Slaa
aliongeza kuwa, mawasiliano yalipoanza na serikali, wakati huo kupitia
Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Elimu, serikali iliomba TEC na
madhehebu ya dini kwa ujumla, kama yanaweza kusaidia ukarabati wa shule
hizo kwa kuwa ziko kwenye hali mbaya na hali ya uchumi wa nchi haikuwa
nzuri.
“Wakati
mchakato huo kwa upande wa elimu umeanza, kulikuwa pia na mgogoro kati
ya serikali na TEC baada ya serikali kuichukua Hospitali ya Bugando kwa
utaratibu huo huo wa kuitaifisha,” alibainisha.
Kwamba
hospitali hiyo ilikuwa kwenye awamu ya pili ya ujenzi kwa msaada mkubwa
wa Shirika la la Maendeleo la Baraza la Maaskofu Katoliki la Ujerumani
(Misereor).
Alisema kuwa
Katibu Mkuu wa TEC alipowasiliana na wahisani, walikataa katakata
kujihusisha tena na ujenzi au ukarabati wa shule au hospitali, vituo vya
afya na zahanati, kwa kuhofia kuwa Serikali ya Tanzania imekuwa
ikitaifisha huduma hizo bila majadiliano ya aina yoyote.
Wahisani hao
walisema hawawezi kuwekeza fedha za walipakodi wao (Ujerumani), lakini
walikuwa tayari kuendelea na huduma mbalimbali za kusaidia dawa na elimu
kwa shule ambazo bado ziko chini ya madhehebu ya dini kwa kuwa hawawezi
kuwaadhibu wananchi na watoto.
Kwa mujibu
wa Dk. Slaa, kwa kuwa shughuli zote za Bugando zilikuwa zinaelekea
kusimama, na kulikuwa na mgomo kila siku kwa madaktari, manesi na
watumishi, serikali ikaomba wajadiliane upya juu ya mambo makubwa
mawili.
Mambo hayo
ni utoaji huduma katika sekta za huduma za jamii, na kuwa na chombo cha
mawasiliano na majadiliano kati ya Ikulu na madhehebu ya dini.
Lakini kwa
kuwa madhehebu ni mengi, wakaomba chombo hicho kiundwe na viongozi wakuu
wa madhehebu yaliyokuwa yanajulikana kwa mujibu wa sheria.
Hivyo,
Waislamu wakawakilishwa na Bakwata, TEC na CCT (kwa madhehebu zaidi ya
60 yaliyoko chini ya Christian Council of Tanzania), na baada ya
mashauriano waliunda chombo hicho.
Alifafanua
kuwa kutokana na hali mbaya ya shule, serikali iliomba madhehebu ya dini
kusaidia ukarabati kwa zile zilizoonekana zitafungwa kutokana na hali
mbaya.
“Nasi kwa
upande wetu, kwa nia njema ya kuisaidia serikali, lakini pia kuwahudumia
Watanzania, tuliwasiliana na wahisani ambao walikazia msimamo wao kuwa
hawako tayari kuingia kwenye shughuli za ujenzi wala ukarabati kwa
kukosa msimamo wa wazi na wa kisheria wa Serikali ya Tanzania kuhusiana
na utaifishaji wa huduma hizo,” alisema.
Katibu huyo
aliongeza kuwa, serikali ilipojulishwa ilichukua hatua ya kuanzisha
mchakato mzima wa kupata suluhu ya jambo hilo. Ndipo akapewa jukumu
hilo, Anne Makinda, wakati huo akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu.
“Hatimaye,
serikali ilikubali kuwa haitataifisha tena na kwa kuthibitisha hivyo,
ikawa tayari kuwekeana mkataba na madhehebu ya dini. Ndipo tukaanzisha
mchakato wa majadiliano na wahisani, nao katika umoja wao kati ya
dhehebu la kikatoliki Ujerumani na Kilutheri pia la Ujerumani,
tukaanzisha mchakato wa namna bora ya kutoa huduma za jamii,” alisema.
Hatimaye,
makubaliano yalifikiwa na ndipo kikazaliwa chombo kipya, Tume ya
Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC), chenye sekretarieti yake, hivyo
huduma ya Christian Medical Board ya TEC na CCT, ikavunjwa na kuwekwa
chini ya CSSC.
Dk. Slaa
aliongeza kuwa, kwa upande wa serikali aliweka saini Edward Lowassa,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu wakati huo. Kwamba TEC na CCT nazo
zikawekeana na wahisani mikataba yao ya ndani ili kupata misaada ya
ujenzi, ukarabati na uendelezaji wa huduma zote za jamii.
Chanzo:- http://chademablog.blogspot.com
إرسال تعليق