BADO
ni mwanzoni tu mwa mwaka na tayari limetokea tukio la ajabu la
kushitusha la maiti ya kichanga kugeuka jogoo ndani ya chumba cha
kuhifadhia maiti kwenye Hospitali ya Mwananyamala, jijini Dar es Salaam,
ambalo hadi sasa linaweza kuwa ni tukio la kwanza kubwa na la
kushangaza tangu kuanza kwa mwaka huu na lililoshika namba moja ya
bmwaka huu kuzidi mengine yote ya ajabu yanayoweza kutokea kwa mwaka huu
wa 2013.
Mwananyama
ni hospitali yenye hadhi ya mkoa kitabibu, ina rekodi za kuwa na
matukio ya ajabu, ila hili siyo tu kwamba linaingia miongoni mwa hayo
bali pia linaweza kutia fora.
Asubuhi
ya Jumatano iliyopita, ilikuwa kizaazaa pale jokofu lililotumika
kuhifadhi maiti ya kichanga cha mtoto, kukutwa ndani yake kukiwa kuna
jogoo.
Mshangao zaidi ni kwamba ndani ya lile jokofu, pembeni ya yule jogoo, kulikuwa na hirizi pamoja na tunguri.
Habari kutoka vyanzo vyetu,
zimewekwa wazi kuwa Jumanne iliyopita, saa 7 mchana, polisi walipigiwa
simu, wakataarifiwa kuhusu maiti ya mtoto iliyokuwa imetelekezwa eneo la
Kigogo, Mbuyuni, Dar es Salaam.
Vyanzo vyetu vimebainisha kuwa
polisi baada ya kupata taarifa hizo walifika eneo la tukio na kukuta
maiti hiyo ya kichanga ikiwa imefunikwa kwa kuzungushiwa sanda.
Kwa mujibu wa Moses Madilu,
mkazi wa Kigogo, aliyedai kushuhudia tukio hilo, polisi walipofika eneo
la tukio waliikagua maiti hiyo na kubaini kwamba ni ya kike.
Chanzo chetu kikaeleza kuwa
baadhi ya mashuhuda, hususan wanawake, walitokwa na machozi kwa
masikitiko kwamba itakuwa mtu alijifungua halafu akakinyonga kichanga
hicho kabla ya kukitelekeza eneo hilo.
“Baada ya kujiridhisha kwa
kazi yao, polisi waliichukua maiti hiyo ya kichanga, wakaipakia kwenye
‘difenda’, wakaipeleka Hospitali ya Mwananyamala,” kilieleza chanzo
chetu.
HOSPITALI YA MWANANYAMALA
Ndani ya hospitali hiyo,
mwandishi wetu alielezwa kuwa polisi walipofika, walishusha maiti hiyo
na kumkabidhi mganga wa zamu aliyejulikana kwa jina moja la Dk. Liwa.
“Dk. Liwa aliwaambia wale polisi wapeleke maiti hiyo mochwari.
“Polisi walifanya hivyo lakini
kule mochwari walimkuta msimamizi mkuu, Omar Buyoya aliyekataa kuipokea
kwa vile daktari hakuthibitisha kama kile kichanga kilikufa au kilikuwa
hai.
“Polisi na Buyoya walivutana
kwa muda mrefu, alitokea mhudumu mwingine wa mochwari aliyekuwa akijuana
na polisi mmoja aliyebeba ile maiti, alikubali kuupokea mwili huo na
kuingiza ndani kwenye jokofu la kuhifadhia maiti.”
Muuguzi huyo aliendelea kusema
kuwa siku iliyofuata, Dk. Liwa alifika mochwari na alipofungua jokofu
na kufunua sanda, badala ya kukuta maiti ya kichanga, alikuta jogoo,
tunguri na hirizi.
“Dk.Liwa alipatwa na mshangao
mkubwa huku jasho likimtoka kutokana na uoga, aliwaita wafanyakazi ambao
walijazana hapo mochwari kushuhudia.
“Baadhi ya wafanyakazi
walipigwa na butwaa huku wengine wakicheka hadi kudondoka chini na
wakawa wanajiuliza kama kweli polisi wanaweza kupeleka jogoo hospitali
au ni mambo ya kishirikina,” alisema muuguzi huyo.
Dk. Liwa na wafanyakazi wenzake waliondoka mochwari na kuacha hilo jogoo katika chumba cha maiti huku wakishindwa la kufanya.
KAULI YA MGANGA MKUU.....
Uwazi ilimtafuta Mganga Mkuu
wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk. Sophinias Ngonyani ambaye alikiri
kuonekana kwa jogoo badala ya maiti ya kichanga.
“Polisi walituletea kifurushi
wakiamini kuwa ni maiti ya kitoto kichanga ambapo tulikipokea lakini
ilipotazamwa na daktari, tulikuta jogoo, hirizi na tunguri, tuliamua
kumchoma moto kwa sababu kile ni chumba cha kuhifadhi maiti siyo cha
kuhifadhia mizoga ya kuku, ng’ombe au mbwa,” alisema Dk. Ngonyani.
KAULI YA POLISI ...
Naye Kamanda wa Mkoa wa
Kipolisi wa Kinondoni, ACP Charles Kenyela alipoulizwa juu ya sakata
hilo alisema kwamba wao kama jeshi la polisi walipigiwa simu na raia
mwema kuwa kuna maiti ya kichanga ambapo askari waliondoka hadi eneo la
tukio na kuichukua mpaka Hospitali ya Mwananyamala.
“Polisi waliichukua hadi
Hospitali ya Mwananyamala kwa wataalamu na baada ya kuikabidhi
waliondoka na kuendelea na shughuli nyingine, nami nashangaa kusikia
kwamba madaktari walikuta jogoo,” alisema Kenyela.
MASWALI MATANO
Je, ni kweli polisi waliikagua maiti na kugundua ni kichanga cha kike?
Kama ndiyo, ilikuwaje kikageuka jogoo?
Kwa nini daktari hakuipima ile maiti, badala yake akaelekeza ipelekwe mochwari?
Je, au polisi walibeba mzoga wa jogoo, wakampakia kwenye difenda wakidhani ni maiti ya kichanga?
Mkweli nani, polisi wanaodai
kupeleka maiti ya kichanga, au hospitali wanaosema walipelekewa mzoga wa
kuku, tunguri na hirizi? Habari kwa hisani ya Unique Model Blog
Post a Comment