Msikiti uliopo katika Mji wa Timbuktu, Mali eneo ambalo limechukuliwa na Majeshi ya Ufaransa na Mali |
Majeshi ya Ufaransa na Mali yanaendelea kufanya doria katika Mji
uliojaaliwa misitu mingi wa Timbuktu baada ya kupata mapokezi ya
kishujaa kutoka kwa wakazi wake baada ya Makundi ya Kiislam ambayo
yalikuwa yameweka makazi yao kwa kipindi cha miezi tisa kuondoka.
Doria hii ni harakati za kufanya uchunguzi kama Wapiganaji wa Makundi ya
Kiislam wameendelea kujihifadhi katika maeneo mbalimbali kwenye Mji wa
Timbuktu baada ya kuingia kwenye eneo hilo bila ya kukabiliwa na
upinzani wa aina yoyote.
Wananchi wa Mji wa Timbuktu wameonesha furaha yao pindi tu majeshi ya
Ufaransa na yale ya Mali yalipofanikiwa kuingia katika Mji huo ikiwa ni
ishara ya kuurejesha tena kwenye mikono ya serikali baada ya kuanguka
kwa wapiganaji hao.
Wakazi wa timbuktu wamewapokea wanajeshi wa Ufaransa na Mali kama
mashujaa huku wakiimba “Mali, Mali, Mali” na kupeperusha bendera za
mataifa hayo mawili ambayo yamekuwa mstari wa mbele kuyatokomeza makundi
hayo ya Kiislam.
Rais wa Ufaransa Francois Hollande amekiri hatua ya kuuchukua Mji wa
Timbuktu ni hatua kubwa katika mapambano yao ya kigaidi ambayo
wameyaanzisha katika eneo la Kaskazini mwa Bara la Afrika.
Hollande amesisitiza wana wakati mgumu katika mapambano hayo dhidi ya
ugaidi kutokana na vitendo hivyo kukita mizizi katika eneo la Kaskazini
mwa Bara la Afrika lakini wamekuwa na mwanzo mzuri.
Katika kufanikisha harakati za kumaliza makundi ya kigaidi Kaskazini mwa
Mali tayari Japan imetangaza kutoa msaada wa dola milioni 120 ikiwa ni
sehemu ya kusaidia kuimarisha hali ya usalama katika eneo la Sahel.
Msaada huo unakuja ikiwa ni siku kumi baada ya raia wa Japan kupoteza
maisha kwenye shambulizi la utekeaji nyara lililotekelezwa nchini
Algeria kwenye kiwanda kimoja cha kuzalisha gesi.
Umoja wa Afrika AU nao umeandaa mkutano maalum ukishirikisha mataifa ya
Magharibi kuchangia pesa kwa ajili ya kusaidia vita vinavyoendelea
Kaskazini mwa Mali lengo likiwa ni kumaliza Makundi ya Kiislam ambayo
wamekuwa wakiyaita ya kigaidi.
Via kiswahili.rfi.fr
Post a Comment