Nahodha wa Ghana Asamoah Gyan akishangilia goli na Kiungo wake Emmanuel Agyemang Badu |
Na Nurdin Selemani Ramadhani
Timu ya Taifa ya Ghana maarufu kama Black Stars imefanikiwa kutinga
hatua ya robo fainali baada ya kufanikiwa kumaliza kinara wa Kundi B
kutokana na ushindi ambao waliupata dhidi ya Niger. Ghana wameibuka na
ushindi mnono wa magoli 3-0 mbele ya Niger na hivyo wamefanikiwa kupata
tiketi ya kucheza na Cape Verde katika mchezo wa hatua ya robo fainali.
Nahodha Asamoah Gyan ndiye alipachika goli la kwanza kabla ya Christian
Atsu na John Boye kufunga magoli mengine ambayo yakaisadia Ghana kusonga
mbele katika hatua ya robo fainali.
Ghana wamepata ushindi huo kutokana na kucheza soka ya kuvutia hatua
ambayo imewafanya mashabiki wao kushangilia muda wote baada ya kukata
tiketi ya kuingia kwenye nane bora.
Kundi B pia limeshuhudia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC
ikiondolewa kwenye mashindano kufuiatia kupata sare ya goli 1-1 dhidi ya
Mali ambayo imepata tiketi ya kutinga robo fainali.
DRC ndiyo walikuwa wa kwanza kufunga goli kupitia mkwaju wa penalti
iliyokwamishwa nyavuni na Dieumerci Mbokani kitu ambacho kilitoa
matumaini ya Congo kuweza kusonga mbele lakini matumaini yao yakapotea.
Dakika kumi na moja baadaye Mali walisawazisha kupitia Mahamadou Samassa
na hivyo kujipatia pointi moja baada ya sare dhidi ya DRC na hivyo
watacheza na wenyeji Afrika Kusini maarufu kama Bafana Bafana kwenye
robo fainali.
Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika yataendelea kwa michezo miwili
ya Kundi C ambapo Burkina Faso watapambana na Zambia huku Ethiopia
watakuwa na shughuli dhidi ya Nigeria.
Via kiswahili.rfi.fr
Post a Comment