Malinzi |
CHAMA cha
Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kimepanga kufanyika mdahalo kwa
wagombea wa nafasi za juu za uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Nafasi ya Urais TFF, inagombewa na Athumani Nyamlani na Jamal Malinzi.
Uamuzi wa
kuendesha mdahalo huo ulifikiwa kwenye kikao cha Kamati ya Utendaji ya TASWA
kilichofanyika jana (Januari 23, 2012), ambapo pia kilijadili masuala
mbalimbali yahusiyo chama hicho.
Nyamlani |
Tayari kikao
kimeiagiza Sekreterieti ya TASWA ifanye maandalizi ya mdahalo huo kwa
kuzungumza na vituo vya televisheni ili uweze kuoneshwa moja kwa moja kwenye
vituo hivyo ili wananchi waweze kuwasikia wagombea hao.
Pia
mazungumzo ya awali na wadhamini mbalimbali yameanza kuweza kufanikisha tukio
hilo la kuendesha mdahalo wa 'live' kwenye televisheni. Nafasi ambazo wahusika
watafanyiwa mdahalo ni Rais na Makamu wa Rais.
TASWA
imekuwa ikifanya mdahalo kwa wagombea wa nafasi za juu kwenye uchaguzi wa TFF,
ilifanya hivyo mwaka 2001 na mwaka 2004 ingawa haukuwa wa live, ikafanya wa
live mwaka 2008, ambapo yote ilikuwa ya mafanikio makubwa, hivyo itafanya
mawasiliano na TFF ili iweze kupata msaada wa karibu kufanikisha jambo hilo.
Tunaamini
ushirikiano uliopo kati ya TFF na TASWA utasaidia kwa namna fulani kufanikisha
jambo hilo, ambapo mdahalo utahusisha waandishi wa habari waandamizi wa
michezo, wahariri wa baadhi ya michezo na wadau wachache wa soka.
Kutokana na
hali hiyo Kamati ya Utendaji ya TASWA imemteua mwandishi wa habari mkongwe
ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Redio ABM, Abdallah Majura kuwa mwendeshaji wa
mdahalo huo kutokana na uzoefu wake katika masuala ya habari na mambo ya
michezo.TASWA inaamini Majura ambaye ni mwanachama wa TASWA akiwa pia amepata
kuwa Katibu wa TASWA FC na Mhazini wa TASWA ni mtu makini, asiyeyumba na mwenye
kutenda haki.
Pia Kamati
ya Utendaji imesisitiza katika kikao chake kwamba uchaguzi wa TFF haimuungi
mkono mgombea yeyote na haina mpango wa kumuunga mkono mgombea yeyote, hivyo
TASWA inaonya kama kuna baadhi ya wagombea wenye ndoto za kutaka kutumia mgongo
wa TASWA kwamba chama kinawaunga mkono ili wapate mteremko kufikia malengo yao
hazitatimia.
Kama kuna
kiongozi au mwanachama wa TASWA ambaye anamuunga mkono mgombea yeyote wa TFF,
huo utakuwa msimamo wake binafsi si wa chama na kama atahusisha chama kwa namna
yoyote atakuwa anakosea na hatutasita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa katiba
ya chama.
Tunawaomba
waandishi wa habari za michezo nchini kuzidisha umakini kipindi hiki cha
uchaguzi wa TFF na kujiepusha na makundi ya aina yoyote ambayo yatatia doa
taaluma ya habari kwa namna yoyote ile.
إرسال تعليق