Mtwara : Serikali inavunja nchi kwa kutosikiliza Wananchi
Kwa wiki ya tatu mfululizo kumekuwa na malumbano kuhusiana na suala
la ujenzi wa Bomba la gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam. Kumekuwa
na madai yenye nguvu ya hoja kutoka kwa wananchi wa Mtwara dhidi ya
porojo kutoka kwa viongozi wenye dhamana ya kujibu madai haya ya watu wa
Mtwara. Watu wa Mtwara kwa umoja wao na kwa kuungwa mkono na viongozi
wa dini zote wamekuwa wakitaka Serikali ifikirie upya suala la mradi wa
ujenzi wa Bomba la gesi na badala yake kujenga mitambo ya kufua umeme
mkoani Mtwara na kusafirisha umeme huo kwenda maeneo mengine ya nchi.
Kwenye moja ya maandishi yangu (Serikali iwasikilize watu wa Mtwara)
nimeshauri kuwa Taifa liwe na gridi nyingine ya Taifa ambayo itatokana
na Gesi tu na ianzie Mtwara.
Ikumbukwe kwamba katiba ya nchi, ibara ya 9 katika mabano J inataka
mamlaka ya dola na vyombo vyake vyote kuhakikisha ya kwamba shughuli
zote za kiuchumi zinaendeshwa kwa namna ya kwamba pasiwe mrundikano wa
utajiri au shughuli za uzalishaji kwa watu wa chache. Katiba inaendela
kwa kuelekeza kwamba uchumi wa nchi upangwe katika uwiano sawia (9, d).
Watu wa Mtwara wanatekeleza matakwa haya ya katiba kwa kukataa
mrundikano wa shughuli za kiuchumi wa nchi na utajiri wa nchi kua kwenye
mikoa michache na hasa mkoa wa Dar-Es-Saalam.
Serikali imekuwa ikitoa majibu ya porojo na kuwatusi watu wa Mtwara
na kama ilivyozoeleka Rais Jakaya Kikwete na Mawaziri wake wamekuwa
wakisema suala la Mtwara linatumika na wanasiasa kujitafutia umaarufu.
Inasikitisha sana kuona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
akiwaambia mabalozi wa nchi za kigeni waliopo hapa nchini kuwa
yanayoendelea mkoani Mtwara yanachochewa na Wanasiasa tuliosimama na
wananchi wanaodai haki ya kufaidi utajiri wa nchi yetu. Rais Kikwete na
Mawaziri wake wameshindwa kabisa kuonyesha uongozi katika suala hili na
hatimaye kuhatarisha umoja wa kitaifa.
Kwa udhaifu wa serikali na tabia ya kutafuta mchawi badala ya kutatua
tatizo la msingi, wananchi wameendelea kukutana na hata wengine sasa
kuanza kusambaza ujumbe wa kukata kipande cha nchi na kuanzisha Jamhuri
ya Kusini. Nimeona kwenye mabango ya mkutano wa hadhara uliofanyika
19/1/2013 wananchi wakibeba mabango yanayoaishiria kuchoka kuwa sehemu
ya Tanzania na kuanzisha Jamhuri ya Makonde kuanzia jiwe la Mzungu
wilayani Kilwa mpaka mto Ruvuma. Haya yanatoka na kiburi cha Serikali
kujishusha na kuwasikiliza wananchi wanao dai haki yao ya kikatiba.
Ni Serikali iliyokosa uhalali wa kutawala inayoweza kudharau hisia
hizi za wananchi. Serikali ielewe kwamba kamwe haitaweza kulinda kila
nchi ya bomba hili iwapo italijenga kwa nguvu. Badala ya kuzungumza na
vyombo vya habari Serikali ifanye mazungumzo na wananchi wa Mtwara na
kukubaliana na matakwa yao. Kitendo cha Serikali kung’ang’ania msimamo
wake dhidi ya watu wa mtwara ni kitendo kinacho weza kuipasua nchi na
hivyo kwenda kinyume na masharti ya katiba ibara ya 28 ambayo inasema:
“kila raia ana wajibu wa kulinda uhuru wa nchi, uhuru mamlaka na umoja
wa taifa.”ibara ya 28, 1.
Inawezekana Serikali inaogopa kuvunja makubaliano na Wachina ya mkopo
wa dola za kimarekani 1.2 bilioni ambao imeuingia bila hata
kushirikisha Bunge. Inawezekana Serikali na hasa watendaji wa Serikali
waliojadili mkopo huu wameshapata chao na hivyo kuogopa kusikiliza madai
halali ya wananchi. Lakini yote hayo hayawezi kuwa zaidi ya Umoja wa
nchi yetu. Hatuwezi kukubali nchi yetu ipasuke vipande vipande kwa
sababu tu ya kulinda mkataba wa bilioni 1.2 tuliokopa China, ambayo
serikali inang’ang’ania.
Tunafahamu kwamba ubalozi wa China umeandika barua serikalini
kuwaondoa raia wa China waliopo Mtwara kwa hofu ya maisha yao. Serikali
inaficha ukweli huu kama ilivyoficha ukweli kwamba Naibu Waziri wa
Nishati na Madini bwana George Simbachawene alifukuzwa na wananchi wa
Mtwara alipokwenda hivi majuzi. Serikali itaficha ukweli mpaka lini?
Lazima tupate majawabu.
Kwanza Serikali iweke wazi mkataba wa ujenzi wa Bomba hili. Kamati ya
Bunge ya POAC ilipokuwa inapitia mahesabu ya TPDC iliomba mkataba na
kwa mshangao mkubwa wabunge wakaambiwa Mkataba haupo TPDC bali upo
Wizarani. Kwa nini Mkataba huu wa matrilioni ya Fedha unafichwa? Mkataba
huu ulisainiwa pamoja mikataba mingine 2, mmoja wa kujenga nyumba za
wanajeshi wa thamani ya dola za kimarekani 400 milioni na mwingine wa
mawasiliano jeshini wa dola za kimarekani 110 milioni, na mikataba yote
mitatu imesainiwa kimya kimya bila kushirikisha wananchi kupitia Bunge.
Lazima mikataba yote hii iwekwe wazi.
Pili, Mkataba huu uchunguzwe kama unalingana na thamani ya fedha
maana kwa utafiti wa awali inaonyesha kuwa bei ya ujenzi wa bomba
imepandishwa maradufu. Wastan wa kujenga bomba la gesi duniani ni dola
za kimarekani 1.2 milioni kwa maili moja. Mradi huu wa Tanzania
utagharimu dola za kimarekani 2.2 milioni kwa kilomita moja (maili 1 ni
sawa na kilomita 1.6).
Tatu, Serikali ibadilishe Mkataba huu kuwa wa mkopo wa kujenga
Mitambo ya kufua umeme Mtwara na ujenzi wa Msongo wa Umeme kama gridi ya
pili ya Taifa. Kwa sasa Tanzania ina gridi moja ambayo inabebwa na
bwawa la Mtera linalo tegemea mto Ruaha ambao hivi sasa unakauka miezi 5
katika miezi 12 ya mwaka. Ni dhahiri kwamba kwa usalama wa Taifa na
hata kwa gharama Nchi itafaidika zaidi kwa kujenga gridi nyingine
kutokea Mtwara badala ya kusafirisha gesi kuja Dar-Es-Salaam.
Serikali haitashinda vita hii kwa kuzusha kwamba ama wanasiasa
wanaopinga wanatumika na makampuni mengine au kwa mataifa ya magharibi
kutaka kuvuruga nchi. Serikali ijitazame yenyewe. Bila kufanya hayo
tunayo pendekeza hapo juu, wananchi wataendelea kupigania hako yao. Hii
ni vita ya uwajibikaji. Wananchi wanataka kufaidika na rasilimali za
nchi yao. Kwa vyovyote vile upande wa wananchi utashinda. Vita ya
uwajibikaji kwenye rasilimali za nchi sio ya vyama vya siasa, ni vita ya
wananchi. Chama cha siasa kitakachokwenda kinyume na matakwa ya
wananchi, kinajichimbia kaburi.
Na:- Zitto Zubery Kabwe (MB)
Post a Comment