Neno La Leo: Gesi Yetu Na Alichoniambia Profesa Chachage Jana Usiku...

b5 0c8f5

Ndugu zangu,

Profesa Chachage ananiambia: " Binadamu havunjwi kwa pesa wala kwa mabavu"

Jana kuamkia leo nimelala usiku wa manane, nilikuwa naongea na Profesa wangu Chachage. Napata tabu kumwita marehemu, maana, unapomsoma Chachage unaona jinsi fikra zake zilivyo hai kuliko labda za walio hai.

Naam, jana usiku, baada ya kutafakari sana yanayotokea Mtwara na hususan sakata la gesi,  niliamua kupekua kwenye maktaba yangu, huko nikakutana na maandiko ya Profesa Chachage. Ikawa ndio chakula changu cha kulalia. Hakika, ilikuwa ni kama nazungumza na Profesa Chachage.


Na kwa anachozungumza kupitia kitabu chake cha ' Makuadi wa Soko Huria', Profesa amenishawishi nipange safari ya kwenda Lindi na Mtwara. Nitapenda nikutane na baadhi ya aliokutana nao huko, maana, mazungumzo na watu hayo yamo kitabuni pia. Na majina ya watu hao yanafahamika.
Naamini, kuwa ukitaka kujua unakokwenda, angaza kwanza ulikotoka, ndipo utaelewa ulipo, na labda kwanini uko hapo. Kisha utapata mwanga wa unakokwenda.
Chachage alikiona kile ambacho wengi hawakukiona, wachache walikiona, lakini hawakutaka kukiona. Kinachotokea Mtwara na Lindi leo Profesa Chachage alikiona, na ushahidi uko kwenye maandiko yake. E nendeni mkayasome.
Chachage aliweka kando usomi wake,  aliwasikiliza watu wa Mtwara na Lindi. Kupitia maandiko yake, Profesa Chachage anatuma nafasi adimu ya kuwasikiliza Watanzania wa Mtwara na Lindi. Walichokisema Wazee wale wa Mtwara na Lindi miaka ile, ndicho kinachotokea sasa, walishaziona ishara.

Lakini wanasiasa waliwabeza, na ndilo kosa linalotaka kurudiwa sasa, kuwabeza watu wa Lindi na Mtwara kuhusiana na suala gesi. Ninapomsoma Chachage, na ninapoona ya sasa, mimi kama Mtanzania, siioni njia nyingine ya kumaliza kadhia hii ya gesi kwa amani bila Serikali na Wananchi wa Lindi na Mtwara kupitia wawakilishi wao, kukaa chini na kuzungumza.
Siku zote naamini, kuwa ' Kila kitu inazungumzika, ni namna tu ya kuutafuta msogeleo sahihi ( approach)'.
Hebu nikumegee kidogo alichoambiwa Profesa Chachage na watu wa Lindi;
" Wanataka kufuga kamba! Hawa walioumbwa na Mwenyezi Mungu. Tunasikia   kwamba wanataka kuchimba mahandaki Rufiji yote na kutuhamishia twende  tukaishi kwingine. Tukaishi wapi? Hawa wamekusudia kuangamiza maisha yetu na kututokomeza tupotee kabisa  katika uso wa dunia hi!"

" Naye Makamu wa Rais (Marehemu  Dr Omar Juma)  alifika hapa na kihelikopta chake, kimezunguka leo kwenye vijiji  vingi tu na kila alipokwenda , tunavyoambiwa , alikwenda kuhutubia. Hapa kwetu, badala ya kutusikiliza tuna nini cha kumwambia, alikuja akahutuhutubia kule shuleni. Tulikuwa  umati mkubwa tu, hata watu wa vitongoji  na vijiji  vya karibu walikuwepo. Haikuuwa hotuba, bali matusi kwa kadri tunavyofahamu sisi. Alidai  ( Makamu wa Rais) kwamba sisi watu wa Rufiji ni wavivu na ndio maana hatuna maendeleo. Alidai kwamba rasilimali tunazo lakini tumezikalia, na ni kutokana na tabia zetu za ushirikina. sasa tunapinga mradi  ambao utaikoa nchi yetu  kwa kuiletea fedha nyingi za kigeni. Alihitimisha  hotuba yake kwa kudai kwamba  kutokana na kupinga kwetu maendeleo ndio sababu tulikuwa tunaishi kwenye madungu na kushindwa hata kuwanunulia wake zetu nguo za ndani! Kama haya si matusi ni kitu gani? Na Kiongozi kama yeye kuthubutu  kusema vile? Na hao wabunge wetu  walitikisa vichwa kwa kuitikia  pale mbele , kama vile sisi hatukuwachagua!"  (Chachage;  Makuadi wa Soko Huria, Ukurasa wa 152)

Naam, kuna mengi kwenye maandiko ya Chachage, nitazidi kuyachambua, yatusaidie kuyaelewa yanayotokea sasa, ili tupate mwanga wa tunakokwenda.
Maggid Mjengwa,
Iringa.

Post a Comment

أحدث أقدم