TAIFA STARS KUIKABILI CAMEROON ‘FIFA DATE’


Na Boniface Wambura
TANZANIA (Taifa Stars) itacheza na Cameroon katika moja ya mechi za kirafiki za Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)- FIFA Date zitakazofanyika duniani kote Februari 6 mwaka huu.
Mechi hiyo itafanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 11 kamili jioni. Kikosi cha Cameroon kinachoundwa na wachezaji wengi wa kulipwa wanaocheza katika nchi mbalimbali duniani kitaanza kuwasili nchini Februari 3 mwaka huu.
Nchi kadhaa ziliomba kucheza na Taifa Stars katika tarehe hiyo ya FIFA, lakini Kocha wa Stars, Kim Poulsen ameamua kucheza mechi hiyo dhidi ya Cameroon ambayo nahodha wake ni mchezaji nyota wa kimataifa, Samuel Etoo Fils.
Congo Brazzaville, Equatorial Guinea, Rwanda na Swaziland nazo zilikuwa zimeomba kucheza dhidi ya Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager. Ukiondoa Swaziland iliyotaka mechi hiyo ichezwe Dar es Salaam, nyingine zilitaka kucheza nyumbani kwao.
Wakati huo huo, Kocha Kim Poulsen atakutana na Waandishi wa Habari kuzungumzia maandalizi ya mechi hiyo ikiwemo kutaja kikosi ambacho atakitumia. Mkutano huo utafanyika saa 5 kamili asubuhi kwenye ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Post a Comment

Previous Post Next Post