TAMKO LA NDUGU BENJAMIN WILLIAM MKAPA
Katika wiki za hapa karibuni kumekuwa na mijadala na mazungumzo mengi
kuhusu mikakati ya maendeleo ya mikoa ya Kusini hususan Mkoa wa
Mtwara. Mazungumzo hayo yamekuwa na lugha kali na yameambatana,
hatimaye, na maandamano na mikutano ya hadhara. Kiini chake ni matumizi
ya gesi iliyogunduliwa mkoani kwa ajili ya miradi au mipango ya
maendeleo ya mkoa huo, mipango iliyopo mbioni kutekelezwa au
inayotarajia kutekelezwa. Mwenendo wa mazungumzo, maandamano na
mikutano ya hadhara imeelekea kuashiria shari na kuvunjika kwa amani.
Aidha vituko na kauli hizo zimekaribia kujenga kutokuelewana kati ya
Viongozi wa Vyama vya Siasa na Serikali, kati ya wanachama wa vyama vya
siasa na viongozi wao, kati ya wananchi na viongozi wa Serikali.
Mtafaruku huu haufai kuachwa uendeleee na kutishia usalama. Mipango ya
maendeleo siyo Siri. Mikakati na mbinu za Utekelezaji wake siyo Siri.
Maelezo yake mazuri yanaweza kutolewa yakadhihirisha namna na kasi
ambayo raslimali zitawanufaisha wananchi wa eneo zilizomo na Taifa
zima. Utekelezaji wa miradi unategemea masharti kadhaa, k.m. Uwapo wa
mitaji na teknolojia. Lakini pia mwekezaji, awe Serikali au Sekta
binafsi, atataka iwepo hali ya utulivu na usalama wa watu, hali na
mali. Hayo yatadaiwa na wawekezaji wa ndani na wa nje. Vurugu, fujo,
vitisho havivutii uwekezaji.
Nikiwa Mwana Mtwara na raia mwema mpenda nchi, nimefadhaishwa sana na
matukio haya ya siku za karibuni Mtwara. Kwa sababu hiyo natoa wito
kwa wadau wote wa maendeleo ya Mtwara kusitisha harakati hizi na
maandamano na mihadhara na badala yake wajipange KUKAA PAMOJA
katika meza moja, kupitia historia, kutathmini mipango, kuchambua kwa
kina mikakati ya utekelezaji wake, na hatimaye kufikia muafaka wa Ujia
wa maendeleo. Fujo, vitisho, kupimana nguvu na malumbano kamwe si
masharti ya maendeleo. Mazungumzo yataboresha sera, ya uwekezaji ya
mkoa na nchi.
Linalowezekana leo lisingoje kesho.
Benjamin William Mkapa
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Post a Comment