HALI ya utulivu na amani mkoani Mtwara imetoweka baada ya baadhi ya
wananchi kuendeleza mapambano na serikali wakipinga gesi asilia
iliyovumbuliwa mkoani humo kusafirishwa kwenda Dar es Salaam bila
kuwanufaisha wao kwanza.
Vurugu hizo zilizoibuka tena jana mkoani humo, zimeelezwa kuwa kubwa
kuliko za juzi zilizotokea mjini Mtwara, kwani watu wanne, akiwamo
askari polisi, wameuawa na wengine saba kujeruhiwa vibaya wakati polisi
walipokuwa wakipambana na waasi hao.
Vurugu za jana zilihamia wilayani Masasi ambako majengo ya serikali na ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), yaliteketezwa kwa moto.
Mashuhuda wa tukio hilo waliliambia Tanzania Daima Jumapili kuwa chanzo
cha fujo hizo ni mzozo uliotokeza kati ya polisi na kijana mmoja
mwendesha pikipiki (bodaboda), ambaye anadaiwa kupigwa na askari.
“Wakati mwendesha pikipiki akibishana na polisi, ilitokea hali ya
kutoelewana, hivyo polisi wakampiga kijana huyo na wakati wanampiga,
mwenzake aliona na kwenda kuwaita waendesha bodaboda wengine na kuibua
vurugu kubwa wakitaka kuchoma moto kituo cha polisi ili kulipa kisasi,”
alisema shuhuda wetu.
Kwa mujibu wa shuhuda huyo, wakati waendesha bodaboda hao wakianzisha
vurugu, baadhi ya wananchi wa kawaida ghafla waliungana nao kuibua madai
mengine ambayo hayakuwa na uhusiano na madai ya waendesha bodaboda.
Madai yaliyoibuliwa na wananchi hao na kuyaunganisha na waendesha
bodaboda ni pamoja na kupinga polisi kuwaonea waendesha pikipiki,
kuitaka serikali iachane na mpango wa kusafirisha gesi yao kwenda Dar es
Salaam na kupinga kulaunguliwa kwenye uuzaji wa zao la korosho.
Hali hiyo ilisababisha polisi kukusanyika na kuanza kupambana na
wananchi hao na kufanikiwa kuwadhibiti wasichome moto jengo la polisi.
Baada ya mpango wa kutaka kuchoma kituo cha polisi kukwama, wananchi hao
waligeuzia hasira zao kwenye majengo ya ofisi za serikali na kuchoma
jengo la ofisi ya Elimu na jengo la CCM Wilaya ya Masasi.
Mali na vitu vingine vilivyochomwa ni pamoja na gari la halmashauri,
nyumba na magari matatu ya Mbunge wa Masasi, Mariam Kasembe, ambaye
amelalamikiwa kwamba amewasaliti katika sakata hilo la gesi.
Pia waliiteketeza nyumba ya Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah (CCM)
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho. Mama Abdallah analalamikiwa
na wananchi hao kwamba ameshindwa kupandisha bei ya zao hilo.
Polisi walionekana kuzidiwa nguvu kutokana na uchache wao kwani wengi
wao juzi walipelekwa Mtwara kukabiliana na vurugu zilizozuka mjini hapo.
Wakiwa katika Mahakama ya Mwanzo ambako walichoma mafaili yote, polisi
walizingirwa na vijana waliokuwa wamebeba mawe na kufunga barabara zote
za kuingia na kutoka kituo kikuu cha mabasi na eneo la soko kuu, licha
ya kufyatua hewani mabomu ya machozi.
Barabara nyingi zilifungwa na kuchomwa moto matairi ya magari, hali iliyozidisha hofu kwa wananchi hao.
Kabla ya jana, vurugu nyingine zilitokea juzi mjini Mtwara, ambapo
wananchi wanaodai kupinga gesi yao kusafirishwa hadi jijini Dar es
Salaam, walichoma moto gari la polisi na jengo moja la Mahakama ya
Mwanzo.
Kituo Kidogo cha Polisi cha Shangani mkoani Mtwara kimechomwa moto huku
Ofisi ya Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nkanaledi mkoani Mtwara, ikivunjwa
vioo.
Pia nyumba ya Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia, ambaye ni Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa
(TAMISEMI), ilinusurika kuchomwa moto kwa madai kuwa amewasaliti wapiga
kura wake katika mzozo huo wa gesi.
Hosteli ya wanafunzi wa Chuo cha Utumishi maeneo ya Kiyangu ‘B’ Mtwara,
nayo ilikoswakoswa kuchomwa moto na wananchi hao kwa kile kinachodhaniwa
kuwa na uhusiano na Hawa Ghasia, ambaye anaitwa msaliti.
“Watu wanne wamekufa katika vurugu hizi akiwamo askari mmoja na wengine
saba wamejeruhiwa vibaya na wamelazwa katika Hospitali binafsi ya
Victoria iliyopo wilayani hapa. Nilishuhudia gari la halmashauri
likichomwa moto, na wakati tukio hilo linatokea mkurugenzi alikuwepo
ofisini kwake na aliomba msaada wa polisi lakini walishindwa kutokana na
uchache wao,” alisema mtoa habari wetu.
Kwa mujibu wa habari hizo, polisi walifika eneo hilo la tukio baada ya
takriban saa nne wakitokea mjini Mtwara na wakati huo hali ya utulivu
ilikwisha kurejea.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Maria Nzuki, alipopigiwa simu,
hakuweza kupatikana licha ya simu yake ya mkononi kuita bila majibu.
Hata hivyo habari zilizopatikana baadaye jana, zilisema kuwa uongozi wa
Mkoa wa Mtwara ulikuwa na kikao cha dharura cha Kamati ya Ulinzi na
Usalama, kwa kuwashirikisha maofisa wa polisi na maofisa Usalama wa
Taifa, waliotoka Dar es Salaam kuongeza nguvu, ambao waliwasili Mtwara
jana kwa helikopta.
Wakati hali ikizidi kuwa tete, serikali inajiandaa kwenda Mtwara kutoa
elimu kwa wananchi hao, kwani madai yao ni ya msingi na yanazungumzika.
Hata hivyo baadhi ya viongozi na wananchi waliozungumza na gazeti hili
wamemtaka Rais Jakaya Kikwete kukatisha ziara yake nje ya nchi ili
arejee kumaliza tatizo hilo.
Chanzo: freemedia.co.tz
إرسال تعليق