Wazee wa El Bur walazimishwa kulipa fidia kwa mauaji ya al-Shabaab

Na Ali Adam, Mogadishu

Wazee watatu wa kikabila huko El Bur wamekuwa katika mahabusu ya al-Shabaab kwa kipindi cha zaidi ya wiki tatu kwa kutolipia adhabu ya fidia kwa niaba ya wanamgambo ambao waliwaua vijana wawili kinyume cha sheria mwezi Disemba 2012.

Wapiganaji wa al-Shabaab wakiandamana wakati wa zoezi la jeshi huko Mogadishu tarehe 1, Januari 2010. Kutokea hapo, kikundi hicho chenye mfungamano na al-Qaeda kiliondolewa katika mji mkuu huo na katika maeneo muhimu ya kiuchumi, jambo lililoambatana na migogoro yao ya fedha. [AFP/Stringer]

Waathirika hao, Qasim Ali mwenye umri wa miaka 21 na Mohamed Aadan mwenye umri wa miaka 25, waliuawa wakati wapiganaji wawili wa al-Shabaab walipowafyatulia risasi vijana waliokuwa wakicheza mpira wa miguu huko El Bur, wakaazi waliiambia Sabahi.

Viongozi wa al-Shabaab walisema vifo hivyo vilikuwa ajali kwani wakosaji walikusudia kuwatisha vijana na kuondoa mkusanyiko, na siyo kuwaua, kwa mujibu wa Abdullahi Farah, mkaazi wa El Bur mwenye umri wa miaka 25. Kulingana na ufafanuzi huo wa al-Shabaab kwamba wapiganaji hao wawili walihusika kama raia na si kama askari, wanamgambo hao waliwapa amri wazee kutoka katika kabila la wapiganaji hao wawili kulipa adhabu ya fidia kwa familia zilizoathirika kwa kutoa ngamia 200.

Kabila hilo lilikataa kulipa fidia hiyo kwa sababu ya hali ya kutokuwa na uhalali wa amri hiyo. Lakini tarehe 12 Januari, al-Shabaab waliwakamata wazee 17 wa kikabila, wakiwaachia 14 kati yao siku sita baadaye baada ya kukubaliana chini ya vitisho kuwa wazee watatu waliobakia watakuwa mahabusu ya al-Shabaab hadi ngamia 200 wamelipwa.

"Hali hii imekuwa na athari kubwa [katika jamii]," Farah alisema. "Tumesikitishwa, lakini kama raia hatuwezi kufanya chochote. Ni vigumu kwa wazee kukusanya ngamia kwa sababu baadhi ya watu ambao wanapaswa kulipa ni masikini sana."

Jamii haihusiki na makosa ya al-Shabaab
Abukar Osman, mmoja wa wazee walioachiwa, alisema kwamba wakati wa mazungumzo wazee hawakufaulu kuwasihi viongozi wa al-Shabaab, wakiwaeleza kwamba jamii haitawajibika kwa kuwa wakosaji hawakuwa raia bali wanamgambo wa al-Shabaab.

"Tuliwaambia al-Shabaab kulipa fidia wao wenyewe," Osman aliiambia Sabahi. "Wauaji ni wanamgambo wenu, na hatuwezi kumudu kulipa mnachokidai," alisema waliwaambia wapiganaji.

"Walikataa kutusikiliza. Walikataa hata kulipa sehemu ya fidia na kutuambia lazima tulipe kila kitu. Hatuna uchaguzi mwingine bali kufuata amri zao na kuchukua ngamia," aliiambia Sabahi.

"Hata kama hawakutupatia tarehe ya mwisho, tunalazimika kutekeleza haraka kwa sababu watu wetu [wasiokuwa na hatia] wamefungwa jela," alisema Osman, akiongeza kwamba wazee walioachiwa huru hawakudhurika wakati walipokuwa mikononi mwa al-Shabaab.

Abdiaziz Aadan, mkazi wa El Bur mwenye umri wa miaka 32, alisema kukamatwa kwa wazee kumerejesha hofu na wasiwasi miongoni mwa wananchi.

"Hali hii kwa kweli ni ngumu kwetu. Al-Shabaab inatuonyesha nguvu yake," alisema. "Watu ambao walipaswa kulipia ngamia wanakumbwa na ugumu kwa jinsi ilivyo."

Aadan alisema malipo ya kiwango cha juu kwa ajili ya ngamia yameongeza msukumo mkubwa kwa wafugaji wenyeji ambao wamekuwa wakijaribu kukabiliana na kipindi kigumu chenye mvua chache na malisho yasiyotosheleza kwa ajili ya wanyama wao.

"Wakaazi tayari hawakuwa na chakula cha kutosha kwa ajili ya kula wakati al-Shabaab walipoyazuia mashirika ya kutoa misaada na sasa wanawaagiza kutoa wanyama wachache wanaowamiliki ambao waliponea ukame wa mwaka jana kwa ajili ya kulipia fidia [kwa niaba yao ]," alisema Aadan.

Tukio kama hilo lilitokea mwezi Juni 2012 wakati al-Shabaab ilipoagiza wakaazi wa Tiyeglow katika mkoa wa Bakool kulipa dola 100,000, kwa mujibu wa Mayow Ibrahim, kiongozi wa ukoo mwenye umri wa miaka 56. Katika mkasa huo, al-Shabaab haikuwa inakusanya fidia, lakini waliagiza tu wakaazi kusaidia fedha kwa ajili ya operesheni zake za ugaidi, Ibrahim aliiambia Sabahi.

Post a Comment

أحدث أقدم