NAIBU
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto
Kabwe, amekishutumu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwamba kinachonganisha
viongozi wa chama chake kwa lengo la kukidhoofisha wakati huu
kinapoelekea kushika dola mwaka 2015.
Zitto
alisema hayo jana alipokuwa anazungumza na viongozi wa CHADEMA wa matawi
na kata zote kutoka Jimbo la Kigoma Kaskazini ukiwa ni mkakati wake wa
kuendelea kukijenga chama na kujua matatizo ya kisiasa na kijamii
yanayowakabili wananchi wake.
Mbunge huyo
ambaye ameamua kupiga kambi jimboni humo kwa lengo la kuwazuia CCM
wasipotoshe wananchi wake wakati huu wanapoadhimisha miaka 36 ya
kuzaliwa chama chao, alisema kuwa licha ya maneno na uvumi kuzagaa
kwamba CHADEMA Taifa inakabiliwa na mgogoro baina ya viongozi, jambo
hilo si kweli.
Zitto
alibainisha kuwa hali hiyo inakuzwa na watu waliopandikizwa na kutumiwa
na CCM kwa ajili ya kuleta mpasuko na kukigawa chama ili kupunguza kasi
yake ya kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
“CHADEMA
hakuna mpasuko wala migogoro kama inavyotafsiriwa na wengi, badala yake
kuna kakundi kanataka kutuhujumu kwa kutugawa kwa kutumia itikadi za
kidini, kimaeneo, kimitazamo na hata kiitikadi kama walivyotumwa na
hicho chama chao.
“Ninachoweza
kusema ni kwamba ndani ya chama chetu kuna majungu, fitina, kuoneana
wivu, usaliti na hata kumalizana kisiasa, haya tutahakikisha
tunayamaliza kikatiba kwa sababu hiyo ndiyo sheria mama inayotuongoza
ili tufikie malengo tuliyojiwekea,” aliongeza Zitto.
Alidai kuwa
wajibu wake ni kupigania misingi ya uwajibikaji na demokrasia ndani ya
CHADEMA ili kuondokana na vitendo vya uongozi wa kutumia mabavu kama
ilivyo kwa CCM, ambayo imekuwa ikitumia nguvu katika kuendesha mambo
yake, sambamba na serikali iliyopo madarakani.
Hata hivyo,
aliwashutumu viongozi wa jimbo lake kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo
katika kujenga chama na badala yake kila kitu kumtegemea yeye kama
mbunge ikiwa ni pamoja na vikao na mikutano ya hadhara.
“Ili tujenge
chama chenye nguvu na heshima, ni lazima viongozi wote tushirikiane
kuanzia ngazi ya matawi, kata na jimbo badala ya kila kitu kunitegemea
mimi mbunge, lazima tuweke misingi imara ya chama ili mgombea ajaye wa
CHADEMA asipate wakati mgumu wa kufanya kampeni,” alisisitiza.
Zitto
aliongeza kuwa, wakazi wa Kigoma kwa miaka mingi wamekuwa hawana mtetezi
katika ngazi za kitaifa, kiasi kwamba hoja za kuendeleza mkoa kwa
kupatiwa miradi ya maendeleo zinapata upinzani mkubwa kwenye vikao vya
uamuzi kama vile Baraza la Mawaziri na Bunge.
“Lazima sisi
watu wa Kigoma tuwe na umoja kwa sababu tumekuwa wanyonge kwa miaka
mingi, na daima nguvu ya wanyonge ni umoja baina yaoNa sisi tunapaswa
kuwa na umoja kwa ajili ya maendeleo ya mkoa wetu na hata hii miradi
inayoletwa Kigoma sasa ni kutokana na kelele tunazopiga,” alisema.
Aliongeza
kuwa hata kama hatagombea nafasi yoyote ndani ya chama, bado ataendelea
kuwa mwanachama mwaminifu na ataitumikia CHADEMA kwa vile misingi
aliyoshiriki kuitengeneza kwa ajili ya ustawi wa chama hicho bado
haijakamilika na hawezi kuiacha ikiwa hivyo.
Post a Comment