Akina mama wa Kenya wanatumia kwa faida desturi ya kunywa chai ya Somalia

Kundi la wasafiri wakiwa kwenye mapumziko ya kunywa chai huko Lafey, Wilayani Mandera. [Bosire Boniface/Sabahi]
Nuna Issa Harun alikulia katika nyumba iliyopo Wilaya ya Wajir nchini Kenya mahali ambapo chai inakuwa tayari wakati wowote kwa ajili ya wageni.


Baba yake, mzee wa heshima mtaa wa Bulla Maow katika mji wa Wajir, alipokea wageni wengi ambao walikuwa na mazoea ya kufanya ziara ya kwenda kumtembelea kwa heshima, na kila wakati walipokuja, walikaribishwa kwa chai.

"Katika jamii ya Kisomali, kutompa mtu kikombe cha chai kunachukuliwa kama ni kumdharau mgeni," Harun, mwenye umri wa miaka 22, aliiambia Sabahi. "Katika utaratibu huo, nilijifunza kutoka kwa mama yangu namna ya kuandaa chai nzuri, ambayo iliwafanya wageni kurudi tena kwa kujifanya kuja kumtembelea baba yangu."

Wakati baba yake, ambaye alikuwa mtafuta rizki, alipofariki dunia mwezi Septemba 2011, familia ilijitahidi kujitegemea. Baada ya miezi michache, wazee waliokuwa marafiki wa baba yake walimwambia Harun anapaswa kuibadilisha chai yake anayoiandaa kwa ustadi kuwa ya biashara.

"Ilikuwa ni kama kunipaka mafuta kwa mgongo wa chupa kwa wazee kusema kuwa walikuwa wakiikosa chai yangu tamu," alisema.

Kisha familia ilianza kutafakari pendekezo hilo la biashara. Harun na familia yake iligundua kuwa kutoa chai kwa watu ambao wanaondoka makwao wakati wa muda wa kazi ni fursa ambayo wanaweza kuitumia kwa faida.

Mwezi Januari 2012, Harun alichagua eneo lenye msongamano mkubwa wa magari kandokando ya njia ya waendao kwa miguu ya barabara ya Wajir-Garissa na kuanza kuuza chai iliyokwishaandaliwa tayari. Mwaka mmoja baadaye jaribio lake lilibadilika na kuwa biashara, alisema mama yake na ndugu zake hawakuhangaika tena.

Wateja wake wanajumuisha watembea kwa miguu wanapoelekea kazini na mafunda gari kutoka katika gereji za jirani ambao hununua chai yake wakati wa mapumziko.

"Wateja wangu wa siku zote wameongezeka kutoka kumi wakati nilipoanza mwanzoni, hadi zaidi ya 100," alisema. "Ninapata zaidi ya shilingi 40,000 (dola 457) kwa mwezi, lakini ninawafahamu [wachuuzi] wengine ambao wanapata zaidi," alisema.

Chai ya Somalia inawekwa viungo vyenye iliki zilizosagwa, karafuu, mdalasini na viungo vingine, na kwa kawaida inawekwa maziwa na sukari.

Harun alisema gharama ya kikombe kimoja cha chai inategemea msimu. "Wakati wa msimu wa mvua maziwa ya ngamia, mbuzi na ng'ombe ni mengi inabidi tutoze kiasi kidogo cha shilingi 10 (dola .11) lakini wakati wa msimu wa kiangazi wakati maziwa ni [ghali] kikombe kinaweza kufika hadi shilingi 30 (dola .34)," alisema.

Halima Abdi Adan, mwenye umri wa miaka 31 mwenye kibanda cha kuuzia chai katika barabara ya Wajir-Moyale, anasema biashara yake ya chai imekuwa nzuri. Anawauzia wafanyakazi wenye shughuli jirani, mashirika na ofisi za serikali.

"Nimesaini mkataba na asasi mbili zisizo za kiserikali na baadhi ya ofisi za serikali ili kuwapelekea chai na wanalipa mwishoni mwa mwezi," Adan aliiambia Sabahi. "Pia tunauza chai kwa mkopo kwa wateja wetu wa kila siku [wanaposhindwa kulipa]."

Adan anasema biashara yake imekua na sasa anaajiri watu watatu ambao wanamsaidia kusambaza. Anasifia mafanikio yake kwa kutoa huduma nzuri kwa wateja na chai yenye ubora mzuri kwa wateja wake.

Kuuza chai kumemuwezesha kusaidia familia yake ya watu wanne, alisema.

Wakati wote ni wakati wa chai
Zeinab Sheikh Mohammed, mkurugeni wa Shirikisho la Wafanya biashara na Viwanda la Kenya katika Jimbo la Kaskazini Mashariki, aliiambia Sabahi kwamba wanawake katika jamii ya Somalia wana akili kwa kutumia wateja wanaokunywa chai kupata uhuru wa kifedha.

"Biashara imeshamiri kwa miaka miwili iliyopita. Wanawake waligundua kwamba wanaweza kutumia nafasi ya utamaduni mzuri kuzalisha kipato," alisema. "Katika jimbo hili, wakati wote ni wakati wa chai. Hata kukiwa na joto kali hapa, ni kawaida kuwaona watu wakinywa kikombe cha chai inayotoa mvuke mchana."

Habari za biashara hii mpya zimeenea hadi katika vijiji vya ndani na sasa vibanda vinavyouza chai vinaweza kupatikana kando ya barabara zinazopita kuelekea vijijini ambako wanawake wanawalenga wasafiri, alisema.

"Hatuna idadi kamili ya wanawake wanaofanya biashara hii, lakini mitaa na vichochoro katika miji mikubwa ya Jimbo la Kaskazini Mashariki vimezibwa na watu wanaouza chai na wateja wakinywa," alisema, akiongeza kwamba biashara ya chai ni fursa kubwa kwa sababu haihitaji mtaji mkubwa wa kuanzia.

Utamaduni wa chai hueneza amani
Mratibu wa Wakala wa Amani na Maendeleo wa Wajir Hussein Adan Mohamud aliiambia Sabahi kwamba watu wazima ambao ni wateja wa kunywa chai wamesaidia kuleta mshikamano miongoni mwa vikundi vya makabila yenye wasiwasi.

"Wateja wa kunywa chai huvuka vizuizi vya kikabila, kijamii, kisiasa na kielimu. Watu wenye elimu hunywa chai pamoja na wale wasiokuwa na elimu katika vibanda hivi vya kuuzia chai," alisema.

Alisema utamaduni wa chai unachukuliwa kama njia nzuri ya kumfanya mgeni ajisikie kukaribishwa vizuri, na baada ya mzozo au kutoelewana, mtu kumnunulia mwenzie kikombe cha chai ni ishara kwamba hakuna anayejisikia vibaya dhidi ya mwenzie.

Hata kwa watu wasiokuwa wa jamii ya Kisomali ambao wanaishi au kufanya kazi katika jimbo hili wamefuata utamaduni wa kunywa chai.

"Nilipokuja hapa, kunywa chai hakikuwa kitu nilichokipenda, lakini sasa ninaipenda," alisema Nick Musasia, ambaye anafundisha teknolojia ya habari katika Chuo cha Achievers Computer College katika mji wa Wajir.

"Kwa siku moja, ninaweza kunywa zaidi ya vikombe kumi vya chai. Kwa kawaida huenda katika kibanda ninachokipenda cha kuuzia chai wakati wa mapumziko kila baada ya saa mbili," alisema.

Post a Comment

أحدث أقدم