KAULI ya
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa kwamba hawezi
kujiuzulu, imeamsha hasira ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), ambacho kimesisitiza kwamba maandamano ya kumng’oa yako pale
pale na sasa amebakiza siku kumi.
Kauli hiyo
ilitolewa jana na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John Mnyika wakati
alipotakiwa kueleza msimamo wa chama chao, hasa baada ya kauli ya Waziri
Kawambwa jana kwamba hawezi kujiuzulu.
Akizungumza
na gazeti hili jana, Mnyika ambaye ni Mbunge wa Ubungo, alisema kauli
aliyoitoa Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe kwamba anampa
siku 14 Waziri Kawambwa ajiuzulu, vinginevyo atang’olewa kwa maandamano
bado ipo pale pale.
Alisema
majibu ya Waziri Kawambwa yameonesha dharau kwa Watanzania, hasa
walalahoi ambao ndio watoto wao wengi wamepata ziro katika mitihani yao
ya kidato cha nne.
“CHADEMA
tunaendelea kusisitiza kwamba Waziri Kawambwa ang’oke, awajibike,
ameshindwa kazi na hili tunamaanisha,” alisisitiza Mnyika.
Alisema CHADEMA inaangalia namna ya kuitisha maandamano hayo kwa kuwashirikisha vijana waliofeli kwani wanaamini wamehujumiwa.
Mnyika
aliwataka Watanzania na wengine wenye uchungu na udhaifu wa elimu ya
Tanzania, hasa wazazi wajitokeze kwani fedha walizowekeza kwa watoto wao
kwa ajili ya elimu, zimeteketea.
Wakati
akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika hivi karibuni katika
viwanja vya Furahisha, Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, ikiwa ni
ufunguzi wa Baraza la Viongozi wa CHADEMA, Kanda ya Ziwa Magharibi,
Mbowe alitoa siku 14 kwa Dk. Kawambwa na Naibu wake, Philipo Mulugo,
kuhakikisha wamejiuzulu nyadhifa zao.
Mbowe ambaye
aliongoza maandamano makubwa ya magari na pikipiki kuelekea uwanjani
hapo, alisema Kawambwa, naibu wake, Mulugo, pamoja na katibu mkuu wa
wizara hiyo, wameshindwa kuiongoza sekta hiyo muhimu, ndiyo maana kwa
sasa wanafunzi wanaishia kuandika matusi na kupata sifuri katika
mitihani.
Alisema
waziri huyo lazima ajiuzulu nafasi hiyo, kwani taifa ameliingiza pabaya
na kuanza kuzalisha maelfu ya watoto wa maskini kumaliza elimu zao za
msingi na sekondari wakiwa hawajui kusoma na kuandika.
Alisema hili
ni janga la kitaifa, hivyo lazima Kawambwa aondoke ndani ya wiki mbili,
vinginevyo CHADEMA itaitisha maandamano makubwa nchi nzima kushinikiza
kiongozi huyo ang’oke madarakani.
“Kwa vile
Kawambwa ameshindwa kuisimamia vema sekta hii ya elimu, na kwa vile
watoto wetu wengi wanafeli na kuishia kuandika matusi kwenye mitihani
yao, CHADEMA tunampa wiki mbili awe amejiuzulu.
“Kila mwaka
wanafunzi 1,200,000 hadi 1,300,000 nchi nzima wanafanya mitihani yao.
Lakini wanaoshinda ni kati ya 35,000 hadi 400,000 pekee, hivyo watoto
wengine wanashindwa kuendelea na masomo yao. Kwa hiyo tunataka huyu
waziri na naibu wake wajiuzulu ndani ya wiki mbili,” alisema Mbowe.
Alisema kwa
sasa Tanzania inazalisha vijana wapatao 800,000 kwa mwaka ambao wanakosa
fursa ya kuendelea na masomo yao, na alimtaka Rais Jakaya Kikwete
kuacha kucheka na kubembeleza viongozi wabovu wanaodidimiza maendeleo ya
nchi na raia wake, na kwamba Tanzania inakabiliwa na majanga makubwa
mawili ya elimu duni na udini.
Naye Naibu
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe, alimtaka Waziri Kawambwa na Naibu
wake, Mulugo, kuwajibika na kupisha katika wizara hiyo.
Pia alimtaka Rais Kikwete aichukue wizara hiyo na kuwa chini ya ofisi yake.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Zitto alisema kuwa ni muhimu viongozi wanaosimamia wizara hiyo wakawajibika.
Alisema uwajibikaji huo unapaswa kufanyika kuanzia kwa katibu mkuu wa wizara hiyo pamoja na kamishna.
Zitto
alisema kuwa rais anapaswa aelezwe kuwa iwapo matokeo yatabaki hivi
mwakani, na yeye atatakiwa kuondoka katika nafasi hiyo.
Post a Comment