VYAMA vya
NCCR-Mageuzi na Chadema vimeng’aka kuhusu matokeo mabaya ya kidato cha
nne, huku Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia akimtaka Rais Jakaya
Kikwete kuunda tume yenye wataalamu mbalimbali wa elimu ili kulinusuru
taifa.
Mbatia alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa matokeo hayo ni matunda ya nchi kuwa na mfumo mbovu wa elimu.
Mbatia
ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa, alisema kama zinavyoundwa kamati za
kuchunguza mauaji na ajali, hata sekta ya elimu inatakiwa kuundwa kamati
kwa kuwa imeoza na kwamba ni janga kwani wanafunzi wengi wanafaulu kwa
kukakiriri sio kuelewa.
“Umefika
wakati wa kuweka tofauti zetu za kisiasa pembeni, tufanye kazi kwa
pamoja ili kulinusuru taifa letu na elimu hii ya maafa, nilishangazwa
sana na kitendo cha wabunge wa CCM kuipinga hoja yangu, haya ndio
matokeo sasa,” alisema Mbatia na kuongeza:
“Matatizo
yapo mengi mfano ni kitendo cha kila waziri kubadilisha somo, kufuta
mtihani au kuunganisha masomo mawili kuwa moja. Mawaziri wote waliopita
tangu 1995 wanatumia mtalaa ule ule bila kuzingatia mabadiliko ya
sayansi na teknolojia”.
Kwa upande
wake, Chadema kimesema matokeo ya kidato cha nne ni janga la kitaifa
ambalo limesababishwa na kupuuzwa kwa madai ya walimu.
Kutokana na
Matokeo hayo, Chadema kimetaka Waziri Dk Kawambwa na watendaji wake
wajiuzulu ili kuruhusu mabadiliko ya kimfumo katika wizara hiyo. Waziri
Kivuli wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Suzan Lyimo alikizungumza na
waandishi wa habari jana alisema:“matokeo haya ni janga la kitaifa
ambalo serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka kulitatua.”
Alisema janga hilo ni matokeo ya serikali kudharau madai ya muda mrefu ya walimu ambao ndiyo wadau wakuu wa elimu nchini.
Lyimo ambaye
pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), alisema walimu wengi wenye
uwezo wamekuwa wakiacha ualimu na kutafuta ajira katika maeneo mengine
“Walimu
wamekuwa wakipuuzwa kwa muda mrefu, wapo wanaoacha kazi ili kutafuta
maslahi lakini wengine wako katika mgomo baridi na ndiyo maana ya
matokeo haya,” alisema Lyimo.

Post a Comment