WAKATI Spika wa Bunge, Anne Makinda akitangaza kufutwa kwa hoja zote
binafsi za wabunge kutokana na vurugu zilizotokea bungeni juzi na jana,
Chadema kimewataka wabunge wao wasiende kwenye Kamati ya Haki, Maadili
na Madaraka ya Bunge hadi pale rufaa zao 10 zitakapotolewa uamuzi.
Rufaa hizo ni pamoja na ile ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu
kulitaka Bunge lisitishe uamuzi wa kupewa ujaji wa Mahakama Kuu, jaji
mmoja kwa madai kuwa hana vigezo vya kuwa na nafasi hiyo.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alitoa msimamo huo jana baada
ya Spika Makinda kueleza bungeni kuwa Lissu ndiye kinara wa vurugu, huku
ikielezwa kuwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge
itamchukulia hatua za kinidhamu.
Kabla ya Spika Makinda kuahirisha Bunge, kulitokea mvutano kati yake na
Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari baada ya Makinda
kumweleza kuwa hajui kanuni hivyo atulie.
Hata hivyo, alimruhusu kuzungumza na ndipo Nassari alipopinga Kamati ya
Uongozi ya Bunge kufuta hoja binafsi za wabunge akieleza ni kinyume cha
kanuni za Bunge kufanyika kitu hicho.
Kabla ya Spika Makinda kujibu, Lissu alisimama na kuomba mwongozo wa
Spika akisema; “Mheshimiwa Spika tunataka utueleze tutaendelea kukata
rufaa hadi lini, wakati una rufaa zetu 10 kuanzia mwaka juzi na
hujazitolea uamuzi, naomba mwongozo wako Mheshimiwa Spika,” alisema
Lissu na kujibiwa na Spika Makinda kuwa, “Rufaa hizo zinafanyiwa kazi na
zitatolewa uamuzi.”
Makinda aliliahirisha Bunge kwa kile alichosema kukithiri kwa vitendo
vya utovu wa nidhamu ndani ya Bunge hilo na kufuta hoja binafsi ambazo
hutolewa na kuchangiwa baada ya kipindi cha maswali na majibu.
Makinda alisema: “Waheshimiwa wabunge, tangu Januari 30, hadi jana
(juzi) Februari 4, 2013 tuliamua kuwasilisha bungeni hoja binafsi za
wabunge ambazo ziliahirishwa katika mkutano wa tisa wa Bunge kwa nia
njema ya kujadiliana masuala makubwa ya kitaifa na kuishauri Serikali
nini kifanyike ili kukabiliana na matatizo mbalimbali yanayowahusu
wananchi.
“Hata hivyo, imelazimu kuahirisha mijadala yote ya hoja binafsi kutokana
na tabia iliyojitokeza ya utovu wa nidhamu kwa baadhi ya wabunge na
hivyo kuamua kwa makusudi kuanzisha vurugu na kulifanya Bunge kupoteza
heshima yake,” alisema Spika Makinda.
Alisema kutokana na hali hiyo, Kamati ya Uongozi imekubaliana kuwa suala
hilo lipelekwe kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili
ilichunguze na kuwasilisha mapendekezo yake kabla ya mkutano unaoendelea
kumalizika na kwamba hoja zote binafsi zisiwasilishwe kutokana na utovu
wa nidhamu ambao ungeweza kujitokeza katika hoja zilizobakia.
Hata hivyo, Lissu alisema kuwa kelele za kutetea taratibu na kanuni ndizo zinamfanya aonekane kuwa ana utovu wa nidhamu.
“Spika anaonyesha upendeleo wa waziwazi, anakiuka kanuni kwa makusudi.
Mimi nitasema, sitaogopa kamati, hata nikiitwa nitasema... Sasa
tunachokifanya, tumekutana leo (jana) na tumeandaa taarifa ya kutaka
Spika aondolewe yeye na naibu wake, hii tutaiwasilisha kama taarifa kati
ya kesho (leo) na keshokutwa (kesho),” alisema Lissu.
Chanzo: Gazeti la Mwananchi
Post a Comment