Chambi Chachage
Siasa ni taaluma. Kama ilivyo kwa
taaluma yoyote, siasa ina wataalamu wake. Lakini si kila mtaalamu wa siasa ni
mwanasiasa. Na si kila mwanasiasa ni mtaalamu wa siasa.
Pengine utata huu ndio uliomfanya
Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, ajaribu kumpatia elimu ya
siasa kila mwanasiasa wa serikali yake. Ili kutimiza lengo hilo wanasiasa
walipelekwa katika chuo cha Kivukoni kupata mafunzo ya taaluma ya siasa na
itikadi.
Pamoja na jitihada hizo bado nchi
yetu ilijikuta ikifanya maamuzi mengi kwa kuzingatia utashi wa kisiasa badala
ya kuzingatia ushauri wa kitaaluma. Kwa mfano, mwaka 1981 Mwalimu Nyerere
aliunda tume iliyoongozwa na aliyekuwa Waziri wa Elimu, Jackson Makwetta. Tume
hiyo iligundua kuwa wanafunzi wengi wa sekondari hawapati elimu stahiki kwa
sababu lugha inayotumika kuwafundishia haileweki kwa wanafunzi walio wengi
achilia mbali walimu wao.
Kutokana na utafiti huo, wataalamu
hao walipendekeza kuwa wanafunzi wafundishwe kwa lugha ambayo wanaitumia katika
maisha yao ya kila siku. Cha ajabu dakika ya mwisho siasa iliingilia kati.
Pendekezo hilo likatupwa kapuni. Wataalamu kutoka Uingereza wakaletwa.
Wakafanya utafiti. Wakagundua kilekile ambacho wataalamu wetu walikigundua.
Lakini wataalamu hao wa Kiingereza wakatoa pendekezo tofauti. Wakasema tuongeze
bidii katika kufundisha Kiingereza.
Naam pendekezo la wataalamu
kutoka katika nchi inayozungumza ‘Kiingereza cha Malkia’ likaonekana ni la
kitaaluma zaidi. Lakini kumbe lilikuwa ni pendekezo la kisiasa tu. Ndio,
lilikuwa la kisiasa maana nyuma ya pazia kulikuwa na mkakati kabambe wa
kutupatia msaada wa kuchapa vitabu mbalimbali vya Kiingereza na kuleta
wataalamu kutoka Uingereza kuja kutufundisha Kiingereza eti ili tuweze
kukitumia kufundishia. Mkakati huu wa kisiasa ulilenga kuendeleza utegemezi
wetu kwa Uingereza, utegemezi ambao haujawahi kuvunjika kikamilifu toka siku
tulipojitwalia uhuru wetu wa kisiasa kutoka kwa Waingereza mnamo mwaka 1961.
Hivyo, misaada ikamwaga. Vitabu
vikachapishwa. Tukasoma ‘Kalulu the Hare’ na ‘Hawa the Bus Driver’. Picha za
sungura mwitu aitwaye Kalulu na dereva wa basi aitwaye Hawa zikatuvutia. Lakini
je elimu iliyowasilishwa na hadithi hizo ilitufikia? Au vitabu hivi vilikuwa ni
zana tu ya kutufundisha Kiingereza? Je, tulikuwa tunajifunza lugha ya
Kiingereza au tulikuwa tunajifunza mada halisi zinazohusu jamii yetu? Lo mpaka
leo najiuliza ni nini hasa nilijifunza!
Miaka mingi imepita sasa toka
tufanye uamuzi huo wa kisiasa na kuubatiza kuwa ni wa kitaaluma. Lakini taaluma
ya ufundishaji inaendelea kutudhihirishia kuwa sekta yetu ya elimu bado
inadorora hasa katika suala la ubora wa elimu japokuwa tumekuwa na mipango
mingi ya kuiendeleza. Baadhi ya wataalamu wetu wanaendelea kutukumbusha kuhusu
baadhi ya yale mapendekezo ya tume ya Makwetta. Je, tunawasikiliza? Au
tunatumia majukwaa ya kisiasa kutoa matamko ambayo yanakinzana na hali halisi
kama inavyoainishwa na tafiti za kitaaluma?
Lakini siasa ni nini hasa? Kwa
ufupi siasa ni taaluma au shughuli inayohusiana na mamlaka. Na tunapozungumzia mamlaka
tunaongelea suala zima la mgawanyo wa madaraka na rasilimali. Hapa tunajiuliza
nani ana mamlaka juu ya suala fulani au rasilimali fulani, kwa nini na kwa
ajili ya manufaa ya nani? Pa tunajiuliza nani anadhibiti mamlaka hayo na kwa
namna gani?
Hivyo, mwanasiasa mwenye taaluma
ya siasa anategemewa kuwa na uwezo wa kutumia mamlaka yake kufanya maamuzi
yanayozingatia utaalamu husika. Kwa mfano, mwanasiasa ambaye hana taaluma ya ualimu
anaweza kutumia utalaamu wake wa kisiasa kuupima ushauri wa watalaamu wa elimu
na kuutumia ushauri huu kufanya maamuzi sahihi. Si lazima ajue kila kitu kuhusu
elimu lakini taaluma yake ya kisiasa inapaswa kumuandaa kuwa na uwezo wa
kutafakari, kuhoji, na kutumia taaluma zingine kwa manufaa ya jamii iliyompa
mamlaka yake.
Yule mwanasiasa mahiri wa
Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, alilitambua hilo. Pamoja na kuwa na taaluma
ya ualimu bado aliona ni vyema ampeleke msaidizi wake, Joan Wicken, katika Kijiji
cha Ujamaa Litowa ili ajifunze namna ya kuendesha shule ya msingi
inayojitegemea. Shule hiyo ilikuwa imeanzishwa na wanakijiji wenyewe ambao
baada ya kujifunza hali na mahitaji ya mazingira yao walijiundia mfumo wao
wenyewe wa elimu unaokidhi hali na mahitaji yao halisi.
Baada ya Joan Wicken kutoa mrejesho
wa uzoefu wake huko, Mwalimu Nyerere aliunda sera ya ‘Elimu ya Kujitegemea’.
Inasemekana kuwa kwa kiasi kikubwa sera hii ilitokana na taaluma asilia ambayo
Joan aliipata katika Shule ya Msingi ya Litowa. Pamoja na mapungufu yake, hii
ilikuwa ni jitihada ya aina yake ya kuoanisha maamuzi ya kisiasa na maamuzi ya
kitaaluma.
Je, mapendekezo ya kamati maalumu
iliyoundwa hivi karibuni na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ili kuipitia
upya sekta ye elimu yatazingatiwa na wanasiasa wetu? Waziri na Naibu Waziri wa
wizara hii wameshanukuliwa wakisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo
tutaanza kutumia lugha ya Kiingereza
kufundishia katika ngazi zote za elimu. Je, matamshi yao yanamaanisha
kuwa wameshafanya maamuzi yao ya kisiasa hata kabla tume waliyoiunda wao
wenyewe haijalifanyia utafiti wa kitaaluma suala hili? Je, utoaji wa elimu ni
mchezo wa kuigiza?
Kila kitu ni siasa. Hivyo, changamoto
iliyo mbele yetu ni kuhakikisha hatutenganishi maamuzi ya kisiasa na maamuzi ya
kitaaluma. Yanategemeana. Tukifanya maamuzi ya kisiasa bila kuzingatia ya
kitaaluma tutaishia kujiuliza ‘bora elimu au elimu bora?’ Na tukifanya maamuzi
ya kitaaluma bila kuzingatia ya kisiasa tutabaki tunauliza 'sera poa lakini
utekelezaji mmh?’
© Chambi
Chachage

إرسال تعليق