Idhaa
ya Kiswahili ya Deutsche Welle leo inaadhimisha miaka 50 tangu
ilipoundwa na kuanza kurusha hewani matangazo yake hapo tarehe 1
Februari 1963 na kusikika katika maeneo ya Afrika Mashariki na Kati.
Sherehe kubwa za kuadhimisha nusu karne hii zinafanyika kwenye makao
makuu ya DW, Bonn, ambazo zinahudhuriwa na wageni kutokea sehemu
mbalimbali wakiwemo mabalozi wa mataifa ya Afrika nchini Ujerumnai.
Hadi kufikia mwaka 1963, shirika la DW lilikuwa limeshatangaza kwa miaka
10 kwa kutumia lugha mbali mbali za Ulaya na halikutaka kulitelekeza
bara la Afrika. Ndipo hapo wakuu wa shirika hili wakatafuta lugha kuu ya
Kiafrika iliyokuwa ikizungumzwa katika eneo kubwa na Kiswahili
kubahatika kuteuliwa hasa kutokana na uhusiano wa kihistoria uliokuwepo
kati ya Wajerumani na wakazi wa Afrika Mashariki.
Wasomi wa Kijerumani pia walikuwa wakiongoza kwenye utafiti wa kiismu wa
lugha ya Kiswahili. Padri wa Kijerumani Ludwig Krapf ndiye aliyeandika
kamusi ya kwanza ya Kiswahili.
Tarehe 1 Februari 1963, Shirika la Utangazaji la DW lilizindua matangazo
yake maalum ya lugha ya Kiswahili yaliyolilenga eneo la Afrika
Mashariki na Kati.
Matukio muhimu duniani wakati huo
Matangazo hayo yalizinduliwa katika mwaka ambao ulikuwa pia na matukio
maalumu ya kihistoria: hotuba ya kihistoria ya Rais wa Marekani J.F.
Kennedy katika Berlin iliyogawanyika kwenye enzi za “Vita Baridi”.
Wakati huo ndipo Kennedy alipotoa ile kauli yake maarufu “Ich bin ein
Berliner”, yaani mimi ni Mberlin, kudhihirisha hisia zake za kuwaunga
mkono Wajerumani waliokuwa wametenganishwa kutokana na ukuta uliokuwa
umejengwa kuugawa mji wa Berlin.
Zanzibar nayo ilipata uhuru wake mwaka huo huo wa 1963 kutoka ukoloni wa
Muingereza, sawa na taifa la Kenya, ambalo baada ya vita vikali vya
kudai Uhuru, Rais wa kwanza wa Kenya huru, Jomo Kenyatta, akaingiya na
kaulimbiu yake ya “Harambee”.
Nako nchini Ujerumani kwenye ulingo wa kisiasa mwaka huo wa 1963, Ludwig
Erhard alichaguliwa kuwa kansela wa pili tangu Vita vya Pili vya Dunia
vilipomalizika, akisisitiza juu ya Ujerumani moja. “Tunataka kuwania
Ujerumani ambayo imeungana na ambayo itashirikiana na watu wote
duniani.” Alisema Kansela Erhard.
Mwaka huo wa 1963 ndio mwaka ambao mpiganiaji haki za Wamarekani wenye
asili ya Afrika, Martin Luther King, pamoja na wanaharakati wengine
250,000 walipoandamana kuelekea Washington. Martin Luther King alitoa
hotuba yake maarufu iliyopewa jina la "Nina Ndoto", ambapo alisema:
"Nina matumaini kwamba itafika siku ambapo watoto wa nchi hii
watatathminiwa kwa tabia na hulka zao badala ya rangi ya ngozi”.
Idhaa ya Kiswahili ya DW hivi sasa
Turejelee matangazo yetu. Leo hii Idhaa ya Kiswahili ni mojawapo ya
idhaa zilizopiga hatua zaidi kwenye matangazo ya Idhaa za DW.
Tunatangaza kwa muda wa masaa matatu kila siku tukilenga maeneo ya
Afrika ya Mashariki na Kati na eneo lote la Maziwa Makuu. Lengo letu ni
lile lile: habari mpya zisizopendelea upande wowote na za kuaminika.
Sambamba na utangazaji, tunaendelea kuweka matangazo yetu kwenye mtandao
na pia kwenye ukurasa wa Facebook. Tulikuwa idhaa ya kwanza ya
kimataifa ya Kiswahili iliyoanzisha matumizi ya “iPhones” kwenye habari.
Vyuo vikuu vingi vya Ulaya hivi sasa vinatumia ukurasa wetu kufundishia
Kiswahili. Tunawatumia wasikilizaji na wasomaji wetu habari kwa ujumbe
mfupi wa simu kila siku. Mtu anaweza kupata habari zetu pia kwenye
Twitter. Huwa pia tunawatumia wasomaji wetu kijarida cha habari kupitia
barua-pepe.
Waandishi na watangazaji wetu kutoka katika nchi tano za Afrika
Mashariki na Kati hushirikiana na waandishi wengine wengi walioko kwenye
maeneo mbalimbali Afrika na duniani kwa ujumla. Kuna makala za aina
mbali mbali kuanzia siasa, haki za binadamu, mazingira, wanawake na
maendeleo, vijana, afya na utamaduni.
Daima tumekuwa tukizingatia habari huru na zisizoelemea upande wowote na pia maingiliano mema ya kitamaduni.
Idhaa ya Kiswahili ya DW imekuwa ikitangaza kupitia masafa mafupi kwa
kipindi chote hiki cha miaka 50, lakini pia kutokana na ushirikiano kati
yetu na vituo vingine vya utangazaji nchini Tanzania, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo, Uganda, Rwanda, Burundi na Kenya, tunaweza
kukutangazia kwa kina yale yanayotukiya Afrika na ulimwenguni kote
kupitia vituo vya redio za FM.
Tunavishukuru sana vituo vyote tunavyoshirikiana navyo kwa kuwa ni
washirika wa kutegemewa. Tunajitahidi kuhakikisha kwamba tunawaletea
taarifa za uhakika na zisizoelemea upande wowote.
Kwa hakika, tunafurahia jinsi munavyoyapokea matangazo yetu na ujumbe, barua na maoni mbalimbali kuhusu matangazo haya.
Mimi pamoja na kundi zima la watangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW
tunawashukuru kwa kusikiliza matangazo yetu na kuwa mashabiki wetu
waaminifu.
إرسال تعليق