
Kama unaishi jijini Dar-es-salaam na hususani kama unatumia njia
inayojulikana kama “Mbezi ya Chini” naamini kwamba umeshawahi kumuona
mtu huyo anayeonekana katika picha hapo juu. Kwa muda mrefu sasa (yaweza
kuwa miaka sasa) makazi yake yamekuwa hapo pembeni tu mwa daraja la
Mlalakuwa karibu kabisa na yalipo makao makuu ya Jeshi La Kujenga
Taifa(JKT) na pia karibu na yalipo mashirika mbalimbali yenye mlengo wa
kijamii kama vile Red Cross nk.
Kutokana na jinsi eneo hilo lilivyo maarufu kwa foleni takribani kila
jicho linalopita pale linamuona. Hujawahi kumuona? Kweli? Askari
Polisi(wa traffic police na wa kawaida) wanaokuwepo eneo lile mara kwa
mara wanamuona na wakati mwingine hata kupiga naye story mbili tatu.
Nimewahi kushuhudia lundo la askari polisi wakisimamisha magari na
pikipiki pale pale huku jamaa akiwa kakaa tu pale kimya akiangalia zoezi
linaloendelea bila kuwabughudhi.
Njia ya Mbezi ya Chini hutumiwa pia na lundo la “viongozi” wa nchi
hii wanaoishi maeneo ya Mbezi wanapita pale na kumuona. Wao pia, kama
mimi na wewe, wanamuona.Wanapotupa jicho pale wanamtizama na kuendelea
na safari zao.
Wahusika wa masuala ya afya, haki sawa, ustawi wa jamii nk. wanapita
pale asubuhi wakielekea kwenye “ofisi” zao zinazoshughulikia masuala
hayo na jioni wanarejea kutoka katika “ofisi” hizo na wanapita pale
kuelekea majumbani mwao na kumuacha pale pale!
Mahali pale ambapo mtu huyu ambaye ni wazi anaonekana kuwa na
matatizo ya akili(mental health issues) ameamua kuishi ni jalalani. Ni
pachafu na pasipotamanika. Kimsingi mazingira anayoishi huyu bwana
hayafai kwa mwanadamu kuishi. Isitoshe, pembeni yake tu, kuna mto ambao
umegeuzwa kuwa dampo la takataka. Karibuni kutwa nzima huyu bwana
hushinda amelala au ameketi katika kijigodoro kidogo na chakavu ambacho
nimeambiwa alitupiwa na watu waliokuwa wamelitumia kumpeleka mgonjwa
fulani hospitalini.
Sasa nimewahi kusoma na kusikia mahali kadhaa kwamba ukitaka kujua
undani wa jamii fulani tizama jinsi inavyowashughulikia watu hawa katika
jamii zao; wanawake, watoto na watu wenye matatizo ya akili(mental
health issues). Sote tunajua jinsi gani jamii yetu inashughulikia au
kutoshughulikia masuala ya wanawake. Tunatambua fika jinsi tunavyojali
au kutowajali watoto(ajira kwa watoto, watoto wa mitaani nk vinaweza
kukupa majibu ya haraka). Pia sasa,na mfano ulio mbele yetu, twaweza
tambua ni jinsi gani tunawajali au kutowajali wenzetu wanaokumbwa na
matatizo ya akili. Picha ya jamii yetu?
Sina uhakika na sera yetu ya taifa ya namna ya kushughulikia watu
wenye matatizo kama anayoonekana kuwa nayo huyu bwana lakini ni wazi
kwamba hastahili kuwa pale. Mbaya zaidi ni kwamba huyu yupo mahali pa
wazi. Mahali ambapo kama nilivyogusia hapo juu, naamini wahusika wa moja
kwa moja wanamuona kila siku na kuamua kwa makusudi kumpotezea tu.
Vipi kuhusu wale ambao wapo huko walipo na ambao hawaonekani?
Unaweza kujiuliza kwamba ndugu mwandishi, mbona wewe huendi basi na
kumuondoa pale? Ni kweli na swali lako litakuwa na mantiki. Pamoja na
hayo, utetezi wangu utakuwa kwamba sina utaalamu wowote wa kushughulikia
watu wenye matatizo ya akili(naamini kwa dhati kwamba huyu mwenzetu ana
matatizo hayo). Wapo wataalamu waliosomea na wenye uwezo zaidi wa
kumsaidia.
Nimeandika hapa kama kutoa wito. Nipo tayari kusaidiana na yeyote
mwenye utaalamu zaidi au wahusika wa moja kwa moja ambao naamini ni
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. Mtu huyu ni sehemu ya jamii yetu.
Kumsaidia ni kuwajibika na kuonyesha utu wetu. Kumuacha mtanzania
mwenzetu (na watanzania wengine wengi) katika hali kama ile sio sawa.
Kama jamii tunawajibika. Nakaribisha maoni na ushauri. Unaweza kutuma
maoni hapa kwenye post hii au kutumia bongocelebrity at gmail dot com.
Asante.
Post a Comment