KUPIGWA RISASI KWA PADRI ZANZIBAR, CUF WATOA MKONO WA RAMBIRAMBI

Na Salma Said,
Chama Cha Wananchi (CUF) nacho kimetoa mkono wa rambirambi kwa wafiwa wote na wananchi wa Zanzibar kutokana na msiba mkubwa wa Padri Muchi huku akiliomba jeshi la polisi kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha linawakamata waliohusika na tukio hilo na kuwafikisha katika vyombo vya sheria

Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi kuhusiana na tukio hilo.

Kamishna Mussa ameahidi kuwachukulia hatua wale wote watakaopatikana kuhusika na tukio hilo kwa kuwafikisha katika vyombo vya sheria huku akitangaza msako mkali wa kuwabaini wote waliosababisha kifo hicho cha Pardi Muchi.
Waumini wa Kanisa la Minara Miwili Mji Mkongwe wamefadhaishwa na taarifa za kifo cha Padri Mushi ambapo walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya ibada ya siku ya Jumapili lakini baada ya kupokea taarifa hizo wameonekana kupigwa na mshangao mkubwa kutokana na kifo hicho cha ghafla.
Wakizungumza kwa masikitiko waumini hao wamesema hawakuwa wakijua chochote kilichotokea hadi hapo walipofika katika kanisa kwa ajili ya kufanya ibada.

“Tumetoka nyumbani tukiwa na matumaini makubwa sana na kufanya ibada zetu kwa amani lakini tulipofika hapa tumepokea taarifa za Pardi wetu kuwa amepigwa risasi jamani Mungu hiki ni nini mbona Zanzibar imegeuka kuwa nchi iasiyo na amani vipi tutaishi katika hali kama hii ya khofu na wasiwasi...Mungu tusaidie waja wako sisi” alisema mama mmoja huku akilia kwa majonzi makubwa.


Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohammed Aboud amesema serikali imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya Padri Muchi na kulitaka jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kutoa taarifa kamili.


“Kutokana na tukio hili la mauaji serikali imeliagiza jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina ili kuwatambua wale wote waliohusika na tukio hilo kwa ajili ya kuwachukulia hatua zinazofaa kwa mujibu wa sheria” alisema Aboud.


Aboud aliwaambia waandishi wa habari kwamba wakati uchunguzi unaendelea, serikali inawaomba wananchi wote kuwa watulivu na kuliachia jeshi la polisi kutekeleza wajibu wake wakati huo huo serikali inatoa mkono wa pole kwa familia ya marehemu na waumini wote wa kanisa la Katoliki na kuwa wavumilivu katika msiba huo mzito hasa katika kipindi hiki kigumu cha maombelezo.


Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu na Mawasiliano ya Umma wa chama hicho, Salim Bimani amewaambia waandishi wa habari kwamba matukio kama hayo ya kihalifu yanayoendelea kuitafuna Zanzibar yatazidi kuendelea iwapo serikali haijawa makini katika kutekeleza wajibu wake ikiwa pamoja na jeshi la polisi kuwajibika katika matukio kama hayo.


“Inasikitisha sana kusikia kwamba Padri amepigwa risasi matukio kama haya kwetu Zanzibar ni mageni sana hatujazowea kusikia matukio haya ya kushitusha lakini kwa utamaduni wetu matukio kama haya ni mapya sana, tunaliomba jeshi la polisi lifanye juhudi za makusudi ili kuwabaini watu wenye nia ya kuharibu amani na utulivu wa wazanzibar ambao wameunganishwa na uzanzibari wao bila ya kujali tofauti zao za kidini au tofauti za kivyama” alisema Bimani.


Wakaazi wa Mji Mkongwe wamesikitishwa na tukio hilo huku wakimueleza Padri Muchi kuwa alikuwa ni mtu mwenye mazowea makubwa na wakaazi wa Mji huko kutokana na mazowea yake alijenga urafiki mkubwa na wananchi wa Shangani karibu na Kanisa Katoliki ambalo alikuwa akifanya kazi zake.


Wananchi hao walisema Padri Muchi mazowea yake aliweza kuingiliana na wananchi wa Shangani kwa kiasi kikubwa na na alikuwa akihudhuria katika shughuli mbali mbali za harusi na mazishi kwa majirani zake jambo ambalo baada ya kusikia taarifa za kifo hicho wamefadhaishwa.


“Kwa kweli alikuwa ni mtu mzuri sana ni mtu tuliyemzowea akija katika shughuli zetu akisikia kuna maziko akihudhuria siku za sikukuu akija na tulikuwa pamoja ni mtu ambaye amejenga mazowea na wakaazi wa Shangani sana ni mtu mwema na alikuwa akiishi na watu vizuri...kifo chake kwa kweli kimetusikisha sana” alisema Mkaazi mmoja wa Mji Mkongwe.


Matukio kama hayo ya kihalifu yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika kipindi cha hivi karibuni ambapo mwaka jana zaidi ya watu watatu walipigwa risasi katika Manispaa ya Mji wa Zanzibar akiwemo Mfanya Biashara mmoja aliyepigwa risasi eneo la Bububu, Padri Ambrose Mkenda alipigwa Tomondo na mgeni mmoja mwenye asili ya Asia alipigwa risasi eneo la Mbweni Mjini Unguja.

Post a Comment

أحدث أقدم