Maafisa wa polisi 200 wa Somalia wapata mafunzo Djibouti

Wajumbe wa kikosi cha polisi cha Somalia wakipunga mkono kabla ya kuondoka kwenda kwenye kozi ya mafunzo ya miezi mitatu huko Djibouti. [Stuart Price/AU-UN IST/AFP]
Wajumbe wa kikosi cha polisi cha Somalia wakipunga mkono kabla ya kuondoka kwenda kwenye kozi ya mafunzo ya miezi mitatu huko Djibouti. [Stuart Price/AU-UN IST/AFP]
Miaka miwili baada ya kuwafunza maafisa wa polisi 500 wa Somalia, jeshi la polisi la Djibouti limeanza kuwafunza 200 zaidi.


Maafisa wa polisi wa Somalia, ambao wamewasili Djibouti hapo tarehe 18 Januari, wameandikishwa katika Chuo cha Polisi Idriss Farah Abaneh, ambako wanajifunza namna ya kudumisha utulivu na kuimarisha usalama. Mkupuo mpya wa maafisa unajumuisha wanawake 16, na mafunzo yatadumu kwa miezi mitatu.

"Polisi wanaume na wanawake wa Somalia watakabiliwa na kazi pevu ya kuweka usalama na utulivu baada ya miongo miwili ya fujo," alisema Balozi Mdogo wa Somalia huko Djibouti Abdirahman Mohamed Hirabe.

"Serikali ya Rais Hassan Sheikh Mohamud imeweka misingi kikosi cha polisi chenye uwezo wa kulinda usalama kwa ufanisi," aliiambia Sabahi. Alizishukuru Djibouti, Italia na Misheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) kwa kusaidia katika juhudi hizi za mafunzo.

"Maafisa wa polisi wanaofunzwa na na washirika wetu watalinda usalama wa Wasomali na kuwakamata wahalifu na majambazi kwa kuendesha uchunguzi wa kipolisi kama lilivyo jesho lolote la polisi duniani," Hirabe alisema.

Alisema kuwa maafisa wa polisi watapelekwa katika maeneo yaliyokombolewa na vikosi vya AMISOM kutoka kwa al-Shabaab.

"Wasomali na Wadjibouti wana lugha mmoja, utamaduni mmoja na dini mmoja," alisema, na kuongeza kuwa ni rahisi kwa vikosi vya Somalia kupewa mafunzo kwa Kisomali.

Polisi wa Somalia wanapewa mafunzo Djibouti katika makubaliano baina ya Djibouti na Umoja wa Afrika yaliyotiwa saini mwezi Januari 2012.

Adaweh Abdi, mshauri wa masuala ya sheria katika Wizara ya mambo ya Ndani ya Djibouti alisema, "Mafunzo yanayotolewa kwa maafisa wa polisi 200 wa Somalia yanahusu kazi za msingi za polisi, mbinu za uchunguzi, uzuwiaji wa uhalifu na taratibu za uchunguzi wa kimahakama."

"Mara watakapopata ujuzi wa msingi, maafisa wa polisi wa Somalia waliopata mafunzo hapa wataweza kuwalinda wananchi wenzao," aliiambia Sabahi. "Lengo ni kufanyakazi nzuri. Ili kufanya hivyo, ni muhimu kwa aina hii ya mafunzo kurudiwa, hivyo ndivyo jinsi ya kupata matokeo ya kuridhisha katika kipindi kifupi."

Mohamed Dabaleh, meneja wa idara ya mahusiano ya nchi mbili ndani ya Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Djibouti, alisema, "Djibouti, kama ilivyo kila nchi imechangia makeshi kwa AMISOM, pamoja na jumuiya ya kimataifa inahitaji kufanya kila kitu kilichomo katika uwezo wake kuleta amani, usalama na utulivu nchini Somalia."

"Tutaendelea kuisaidia Somalia kwa sababu ni nchi ndugu kwetu na kila kinachotokea kule kinatuathiri kwa njia moja au nyengine," aliiambia Sabahi.

Post a Comment

أحدث أقدم