MAHAKAMA Kuu nchini Kenya imeeleza kwamba haiwezi
kuamua iwapo Uhuru Kenyatta na William Ruto wanapaswa kugombea nyadhifa
katika uchaguzi mkuu ujao. Wawili hao wanakabiliwa na tuhuma za
kuchochea ghasia nchini Kenya baada ya uchaguzi uliokumbwa na utata na
kusababisha mapigano ya kikabila.
Ikiwa zimesalia wiki mbili tu kwa uchaguzi mkuu kufanyika Kenya,
inaonekana kuwa wananchi ndiyo watakaoamua kupitia kura, iwapo Uhuru
Kenyatta na William Ruto wanafaa au hawafai kuwa viongozi nchini. Uhuru
Kenyatta anawania urais katika uchaguzi mkuu utakaokuja katika muda wa
wiki mbili zijazo na makamu wake ni William Ruto.
Kesi hiyo iliwasilishwa na mashirika yasiyo ya serikali yaliyotaka
kubainishiwa iwapo viongozi hao wawili wa muungano wa kisiasa, Jubilee,
wana uwezo wa kuhudumu katika ofisi ya serikali wakati wanatuhumiwa kwa
kesi za uhalifu. Hali ambayo mashirika hayo yanaona ni kwenda kinyume na
katiba ya nchi.
Mahakama ilikuwa iangalie iwapo Uhuru na Ruto wangechaguliwa,
wataweza kutimiza jukumu la kuiongoza nchi, wakati wanatuhumiwa kwa
kuhusika na ghasia zilizoshuhudiwa Kenya baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka
2007, katika mahakama ya uhalifu ICC, mjini Hague Uholanzi. Uamuzi huu
umetolewa baada ya hapo jana kuwepo kikao cha mahakama hiyo ya uhalifu
ICC, kukagua hali ya kesi hiyo inayowakabili wawili hao.
Kesi hiyo iliyowasilishwa na mashirika yasiyo ya kiserikali
inaendelea katika mahakama kuu mjini Nairobi na inatarajiwa kutoa uamuzi
iwapo mahakama ina uwezo wa kutoa uamuzi juu ya wawili hao au iwapo
itahitaji usaidizi wa mahakama ya juu nchini kufikia uamuzi kuhusu hilo.
Zimesalia wiki mbili tu kwa uchaguzi mkuu kufanyika Kenya na uamuzi huu huenda ukawa na athari kubwa kwa uchaguzi ujao.
Mahakama inajaribu kuona iwapo Uhuru na Ruto ikiwa watachaguliwa
wataweza kutimiza jukumu la kuiongoza nchi, na wakati huo huo
kukabiliana na kesi inayowaandama katika mahakama ya uhalifu wa kivita
ICC mjini Hague Uholanzi, ambapo wanatuhumiwa kuhusika na ghasia
zilizoshuhudiwa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.
-BBC
-BBC
إرسال تعليق