Na Hassan Muse Hussein, Garowe na Barkhad Dahir, Hargeisa
Viongozi wa Somalia na wananchi walielezea kushtushwa kwao na kulaani
baada ya kijana mmoja kumpiga risasi Sheikh Abdulkadir Nur Farah ndani
ya Msikiti wa Badar huko Garowe wakati wa sala ya Asr Ijumaa iliyopita
(tarehe 15 Februari).
Farah alipigwa risasi mgongoni wakati alipokuwa akiinama kusali.
Masaa baadaye, Rais wa Jimbo la Puntland Abdirahman Mohamed Farole
aliwalaumu hadharani al-Shabaab kwa mauaji hayo ya sheikh maarufu wa
Somalia, na kutangaza kukamatwa kwa Abdirahman Hussein Jama Bile
kuhusiana na mauaji.
Siku ya Jumamosi, polisi wa Somaliland waliwatia mbaroni washukiwa wawili zaidi huko Las Anod kuhusika na mauaji hayo.
"Mmoja wa watu wawili hao ambaye yuko mikononi mwetu anaaminika kuhusika
moja kwa moja na mauaji ya wiki iliyopita ya marehemu Sheikh Abdulkadir
Nur Farah, wakati mshiriki mwenzake aliwezesha kutoroka kwake,"
Abdullahi Said Guleid, naibu kamanda wa polisi huko Sool, aliliambia
gazeti la Dawan.
Alisema kuwa washukiwa walikamatwa wakati walikuwa wakiendesha gari
kuelekea mjini, kiasi cha kilomita 150 magharibi ya Garowe. Watu hao
wamehamishiwa Hargeisa na wako chini ya uchunguzi, Guleid alisema.
Suluhisho kwa itikadi kali
Sheikh Abdulkadir Nur Farah alizikwa
katika makaburi ya kaskazini ya Garowe siku ya Jumamosi (tarehe 16
Februari). [Hassan Muse Hussein/Sabahi]
Viongozi wa kidini Somalia nzima walilaani mauaji hayo na kutoa wito kwa
wananchi kutafuta suluhisho la siasa kali. "Tunalaani mauaji haya,"
alisema Sheikh Mubarak Haji Nur wa Buro, Somaliland. "Ni kinyume na
misingi ya Uislamu na utamaduni [wa Somalia]."
Nur pia alitoa wito kwa viongozi wa dini na wa Somalia kusimama pamoja dhidi ya wale wanaomwaga damu za wasio na hatia.
Sheikh Ahmed Abdisamad, mtumishi wa huko Puntland na kiongozi wa kamati
ya utendaji ya Balaza la al-Itisaam, kikundi cha kidini ambacho kiliapa
kupambana na uenezaji wa itikadi ya al-Shabaab, alitangaza Jumanne
(tarehe 19 Februari) kwamba yeye na viongozi wa dini nyingine wanapanga
kufanya mkutano mkuu katika siku zijazo kufanya utafiti kwa ajili ya
kuelewa vizuri chanzo ambacho kilisababisha wenye msimamo mkali nchini
Somalia na kutoa suluhisho linalozingatia dini ambalo litatumika na
umma.
Farole na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Somalia Mohamed Mohamud Guled
walisema wanayakaribisha na watatoa msaada wao kamili kwa mkutano wa
masheikh.
Abdisamad pia alipongeza mamlaka za Somaliland kwa kuwakamata washukiwa
kwa haraka. Alihimiza tawala za eneo nchini Somalia kuwashirikisha
wananchi ili kukabiliana kwa uthabiti dhidi ya al-Shabaab.
Ili kupambana na wenye msimamo mkali na kutafuta suluhisho thabiti,
jamii za Somalia zinapaswa kushirikiana kushughulikia masuala yote
yanayowakabili, alisema. Wakati kutokubaliana na matatizo yanapotokea,
watu wanapaswa kurejea katika uongozi ulioundwa wa kitaaluma na kisiasa.
"Makabila yetu, watumishi, majimbo, wafanyabiashara, wanajeshi na
vitengo vyote vya umma lazima viungane kwa lengo moja," aliiambia
Sabahi.
Sheikh Abdinasir Haji Ahmed wa Las Anod pia alilaani al-Shabaab kwa
mauaji hayo. "Sheikh huyo aliuawa na watu wakatili ndani ya al-Shabaab,
hususan wanakikundi cha Amniyad ambacho kinasifika kama watu waliotengwa
ambao wanawaua Waislamu."
Farah azikwa
Farah alizikwa katika makaburi ya kaskazini ya Garowe Jumamosi, mazishi
yaliyohudhuriwa na watumishi wa dini kutoka Somalia nzima, wananchi na
wawakilishi kutoka serikali ya Somalia na utawala wa Puntland.
Kabla ya kifo chake, Farah alieleza jinsi alivyoipinga al-Shabaab kwa
nguvu zote, na alikuwa ni mwanachama wa Baraza la al-Itisaam.
"Wanajiita vijana wa jihadi, lakini jihadi yao inawalenga Waislamu,"
Farah alisema katika mawaidha katika Msikiti wa al-Rawda tarehe 5
Januari. "Wamewaua Waislamu wengi, na wote mnajua kwamba mamia ya
Waislamu wanakufa katika milipuko. Ni wangapi walikufa kule Bosaso,
Garowe na Galkayo wakati wakiingia au kutoka msikitini? … Hii ni aina
yao ya jihadi."
Farah pia alizungumza katika mazishi ya Sheikh Ahmed Abdirahman, ambaye
aliuawa mwezi Disemba 2011 huko Bosaso alipokua akiondoka kutoka Msikiti
wa Al-Rawda baada ya sala ya alfajiri. Farah aliilaumu al-Shabaab kwa
kifo cha Abdirahman.
Jumuiya ya Kimataifa ya Wanazuoni Wa Kiislamu siku ya Jumapili waliomboleza kifo cha Farah na walilaani mauaji yake.
"Jumuiya inatoa wito kwa watu wa Somalia kuungana dhidi ya itikadi kali
ili kuwalinda watu wa jamii na kulinda maisha ya wanazuoni na raia wenye
uwezo mkubwa," shirka hilo lilisema katika taarifa iliyotiwa saini na
Mwenyekiti Yusuf al-Qaradawi na Katibu Mkuu Ali al-Qaradaghi.
Dahir Hassan,mwenye umri wa miaka 25 ambaye ni mwanafunzi wa masomo ya
Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki huko Bosaso alisema hii
ni mara yake ya kwanza kusikia mtu kuuwawa wakati anaswali. "Ilikuwa
inatushangaza kujua kwamba mtu aliuawa baada ya kuondoka msikitini,"
aliiambia Sabahi.
Hassan alisema alitazama video katika mtandao wa Youtube ikionyesha kukamatwa kwa Bile na kumwita "kijana, mdogo mpotofu".
"Watu wanaouawa ni watumishi wetu wa dini, chanzo chetu cha maarifa,"
alisema Hassan, akiongeza kwamba utawala wa Puntland utapaswa kutoa
walinzi wenye silaha kwa watumishi wa dini. "[Al-Shabaab] inataka
kuondoa nguvu ya taifa hili na wanazuoni wake, hali ambayo itasababisha
nchi yetu kukosa viongozi wasomi siku zijazo."
Chanzo: sabahionline.com


إرسال تعليق