
Mripuko mkubwa umeutikisa mji wa Gao
kaskazini mwa Mali saa chache baada ya mapigano baina ya jeshi la
serikali na wapiganaji wa kiislamu. Awali jeshi la Ufaransa lilikuwa
limetangaza kuwa utulivu umerejeshwa mjini humo.
Kulingana na maelezo ya wanajeshi wa Mali, mripuko huo ulitokea
kaskazini mwa mji wa Gao, kwenye kizuizi cha barabara inayoingia katika
mji huo kutoka upande wa kaskazini. Kizuizi hicho kililengwa na
waripuaji wa kujitoa mhanga Ijumaa na Jumamosi.
Mapambano ya bunduki kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na wapiganaji wa
kiislamu katika maeneo yaliyokombolewa na vikosi vinavyoongozwa na
Ufaransa jana Jumapili, ndio mapigano ya kwanza makubwa kufanywa mjini
tangu kuanza kwa mgogoro huo.
Milio ya bunduki yatawala
Mirindimo ya silaha kubwa na ndogo ilitawala mji wa Gao kuanzia asubuhi
hadi alasiri, na ukimya ulirejea saa za magharibi, baada ya umeme
kukatwa na kuutumbukiza mji huo katika lindi la giza.
Hata baada ya hali kuwa shwari, wanajeshi wa Ufaransa na wenzao wa Mali
walibakia na wasiwasi kwamba wapiganaji wa kiislamu wanaendelea
kujificha mjini humo. Mkazi mmoja wa mji wa Gao alisimulia jinsi
alivyoshuhudia mripuaji wa kujitoa mhanga akiuawa.
''Kulikuwa na milio ya risasi kwa takribani saa moja, kisha akajitokeza,
akatembea peke yake kuwasogelea wanajeshi, akiwa na silaha. Wanajeshi
walipoona anawasogelea, walimfyatulia risasi, ndio akaripuka---Boom.''
Alisema.
Vyanzo vya habari kutoka idara ya usalama vimedokeza kuwepo kwa
wapiganaji wengi wa kiislamu mjini Gao, na kwamba wanajeshi wamewauwa
baadhi ya wapiganaji hao. Hata hivyo, madai yao hayajathibitishwa na
waandishi wa habari katika mji huo.
Bado waasi ni kitisho
Makabiliano makubwa yalianza jana asubuhi, baada ya wanajeshi wa Mali
kukwaana na wapiganaji wa kiislamu katikati mwa mji, karibu na kituo cha
polisi ambacho kilitumiwa na waasi kama makao yao makuu, kabla ya
kutimuliwa mwezi uliopita.
Ilibidi wanajeshi wa Ufaransa waingilie kati
Shahidi mmoja alisema kuwa wanajeshi wa Ufaransa walilazimika kuingilia
kati. Alisema pia kuwa kwa macho yake aliona mtu anayeamini kuwa ni
raia, akipigwa risasi. Kanali wa jeshi la Mali, Mamadou Sanake, amesema
kuwa waasi wamejipenyeza mjini wakitumia pikipiki, na wengine wakipita
katika mto Niger ambao unapita nyuma ya ofisi ya Gavana.
Muungano wa wapiganaji wa Jihad katika Afrika ya Magharibi, MUJAO,
umedai kuhusika katika mashambulizi dhidi ya wanajeshi na kuwatuma
waripuaji wa kujitoa mhanga.
Mashambulizi haya yanadhihirisha kitisho cha vita virefu nchini Mali
huku Ufaransa ikitafakari mpango wa kufungasha virago vyake na kuondoka
ikiyaacha majukumu mikononi mwa vikosi vya kiafrika. Ufaransa inataka
kuondoka haraka na kuyakabidhi majukumu ya kijeshi kwa kikosi cha Umoja
wa Mataifa cha kulinda usalama, na wiki iliyopita ilitangaza kwamba
itaanza kuwarudisha nyumbani wanajeshi wake mwezi Machi.
Jana, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi, Sergei Lavrov, aliikejeli
Ufaransa, akisema inavuna kile ilichopanda nchini Libya, ambako iliwapa
silaha waasi waliompindua aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, kanali
Muammar Ghadafi. Miongoni wa wapiganaji wa kiislamu kuna watuareg wengi
ambao walipigana bega kwa bega na wanajeshi wa serikali ya Ghadafi,
ambao baada ya kushindwa walikimbilia Mali, wakibeba silaha zao.
إرسال تعليق