KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime amesema kuwa wanaandaa
jalada la kuhusika kwa Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage kwa
ajili ya kuliwasilisha kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Kamanda Misime alisema jana kuwa wako mbioni kukamilisha jalada hilo ili
walipeleka kwa DPP kwa ajili ya kufikishwa mahakamani.“Ni kweli
tumepokea malalamiko ya Chadema na tunaandaa malalamiko ili kuwasilisha
kwa mwanasheria na Serikali,” alisema Misime.
Hayo yamekuja kutokana na vurugu zilizotokea kati ya wafuasi wa Chadema
na baadhi ya wabunge wa CCM, akiwamo Rage wakati walipokuwa wakigombea
mlingoti wa bendera kitendo kilichosababisha watu watatu kujeruhiwa
katika tukio hilo wikiendi iliyopita mjini Dodoma.
Hata hivyo, Rage amekana kuhusika na vurugu hizo akisema anaamini
uchunguzi kuhusu tukio hilo utamuweka huru kabla au baada ya kufikishwa
mahakamani kwa sababu hakushiriki wala kumpiga mwanaChadema aliyetangaza
kumshtaki.
“Sikumpiga. Historia yangu inaonyesha kuwa sijawahi kushiriki vitendo
vya vurugu wala mapigano kwa sababu yoyote ile. Mimi siyo mhuni wa
kupiga mtu. Nilichofanya ni kumlinda yule kijana asipigwe na wanaCCM
waliojaa hasira kwa yeye kuingilia mkutano wetu,” alisema Rage, ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya Simba.
Alisema kada wa Chadema ndiye chanzo cha vurugu hizo zilizoishia kwa
kujeruhiwa na wanaCCM baada ya kuvamia eneo la mkutano wa chama hicho.
“Baada ya kuona kitendo hicho, mimi pamoja na Mwenyekiti wa CCM wa
Iringa, Deo Sanga, kama viongozi tulimfuata kijana yule na kumsihi
asifanye hivyo baada ya kuona vijana wa CCM waliokuwapo eneo lile
wanaanza kupandisha jazba ambazo tusingemudu kuzizuia, lakini
hakutusikilizwa,” alisema.
Rage alisema baada ya kuona kijana huyo anaanza kushambuliwa na wanaCCM
ndipo alipolazimika kuingilia kati kuwaamulia na kumkinga asipigwe na
mawe na majabali yaliyokuwa yameshikwa na wanaCCM, ambapo kijana huyo
alifanikiwa kuchomoka na kukimbia.
Alisema kabla ya vurugu, kundi dogo la wafuasi wa Chadema lilikuwapo
eneo la mkutano wakiwa na bendera ya chama hicho bila kufanya vurugu
yoyote, ambapo yeye aliwasihi kuwaacha wasikilize sera za chama hicho
kwani mkutano ulikuwa wazi kwa wananchi wote bila kujali itikadi za
vyama.
Hata hivyo, picha zilizopigwa na kuchapishwa kwenye vyombo vya habari
zilimwonyesha Rage na wafuasi wa CCM wengine wakiwa katikati ya vurugu
hizo na juzi uongozi wa Chadema Wilaya ya Dodoma ulitangaza kumburuta
mahakamani mbunge huyo kwa tuhuma za kujeruhi, kung’oa na kuharibu mali
za chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Kauli ya Rage imetokana na kitendo cha uongozi wa Chadema wa Wilaya ya
Dodoma kutangaza nia ya kumshtaki baada ya kumpiga kada wao. Makada wa
CCM na Chadema walipigana Jumapili iliyopita wakati wa maadhimisho ya
miaka 36 ya CCM mjini Dodoma.
Vurugu hizo zilizuka baada ya wafuasi wa Chadema kukasirishwa na kitendo
cha vijana wa CCM kung’oa bendera yao wakati wakiendesha mkutano kwenye
eneo la Mwanga Baa mjini Dodoma.
Wafuasi hao wa Chadema walilazimisha kurudisha bendera yao wakati
mkutano ukiendelea, ndipo makada wa CCM waliojumuisha wabunge wa Jamhuri
ya Muungano walipoamua kuwapiga kwa kuwarushia mawe wafuasi hao na
kusababisha kuumia kichwani kwa kada wa Chadema.
Wabunge wa CCM waliokuwa katika tukio hilo ukiacha Rage ni pamoja na
Seleman Jafo, Said Mtanda, Mary Chatanda na Nyambari Nyangwine.
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai akizungumzia suala hilo alimtetea Rage,
akisema alikuwa akiamua ugomvi huo na kama isingekuwa yeye mauaji
yangetokea.
“Hakuhusika yeye alikuwa akiamua ugomvi na kama asingekuwepo mauaji yangetokea,” alisema Ndugai.
Katibu wa Wabunge wa CCM, Jenista Mhagama alisema kwamba hajapata taarifa za kuwapo kwa tukio hilo.
Chanzo: Gazeti la Mwananchi
إرسال تعليق