TAMKO LA BAVICHA KUHUSIANA NA MATOKEO MABOVU YA KIDATO CHA NNE KWA MWAKA 2012



Kama muhimili wa vijana na masuala ya vijana nchini, Baraza la Vijana wa CHADEMA, BAVICHA limeshtushwa na kufedheheshwa na matokeo mabovu   ya Kidato cha Nne ya mwaka 2012 yaliyotangazwa siku chache zilizopita na Waziri wa elimu Nchini.

Mshtuko huu unatokana na ukweli kuwa 94% ya wanafunzi wote waliofanya mtihani wamefeli vibaya sana na haijawahi kutokea katika historia ya elimu nchini.

Ikumbukwe kupanda kwa kasi kiwango cha kufeli kwa wanafaunzi wa kidato cha nne mwaka huu ni muendelezo wa kushuka kwa kiwango cha ufahulu ambacho mtiririko wake unaanzia mwaka 2006.

Haya ni matokeo ya kupuuzwa kwa sauti za mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wa elimu ambao tumekuwa tukipiga kelele kuhusu hatma ya elimu ya nchi huku serikali ikibeza sauti hizo. Tafiti nyingi zimefanyika, mapendekezo mengi yametolewa lakini serikali daima imekuwa kiziwi juu ya tafiti na mapendekezo hayo



SABABU KUU YA MATOKEO MABOVU

BAVICHA inatambua kuwa matokeo haya mabovu kuwai kutokea Tanzania yanatokana na sababu moja kuu ambayo ni UDHAIFU wa serikali ya CCM. Kwa udhaifu huo, serikali hii;
·        Haijatambua umuhimu wa haki ya elimu kwa watoto na vijana wa Tanzania kwa ajili ya maendeleo ya nchi hii.
·        Imeshindwa kuweka miundombinu na mazingira wezeshi ya kutoa elimu bora kwa raia wake
·        Imeshindwa kutambua waalimu ni injini muhimu kwa Maendeleo ya nchi na hivyo kuwapuuza na kuwadharau siku zote
·        Imeamua kukumbatia mfumo wa elimu ambao uharamia wake ndio matokeo haya ambayo kwayo maisha ya vijana yanaharibika
·        Imeshindwa kufuatilia kwa ukaraibu matokeo ya tafiti mbalimabli za mashirika yasio ya kiserikali ambazo zimekuwa zikionyesha ubovu wa sekta nzima ya elimu na pia kupendekeza hatua za kuchukuliwa.

ATHARI ZA MATOKEO HAYA
1.    Wanafunzi 344,210 waliopata madaraja ya IV na 0 wanaungana na wenzao 481,295 walifeli darasa la saba mwaka 2008 na hivyo kufanya kundi hili lililoanza darasa la kwanza mwaka 2002 kuzalisha jumla ya vijana 825,505 wasioajirika popote kwa kuwa hawana ujuzi wala elimu ya kukidhi vigezo vya kuajiriwa.Kwa elimu ya Tanzania ilivyo, kundi hili halina hata uwezo wa kujiajiri kwa vyovyote vile.

2.    Kwa kuwa wanafunzi waliopata madaraja ya I,II na III ambao ndio wenye vigezo vya kujiunga na kidato cha tano na sita ni 23,520, ni wazi kuwa baadhi ya shule zitakosa wanafunzi wa ngazi hizo kwani uwezo  uliopo wa kudahili wanafunzi kwa ngazi hiyo ni zaidi ya wanafunzi 50000.

3.   Vyuo vikuu navyo kwa mwaka mwaka 2015 vitakosa wanafunzi wa kudahili kwani ni wazi kuwa kundi hili litalojiunga na kidato cha tano litachujika kutokana na wale watakaofeli kwa kuwa mazingira yanatoa mwanya huo ukiachilia mbali wale watakaoshindwa kujiunga na ngai hiyo kwa matatizo ya ada na nk. na hivyo kuchangia kukosekana kwa wataalamu ambao watakuwa wanahitajika kuzalishwa kwa wakati huo.  Vyuo vikuu nchini vinadaili wanafunzi zaidi ya 65,000 kwa mwaka wakati wanafunzi watakaokuwepo ni chini ya 23,520 hivyo kuvitia hasara vyuo hivyo kwa wakati huo. Kwa hali hii, serikali ya CCM haiwezi kufikia lengo lake la kudfikisha wanafunzi zaidi ya 300,000 ifikapo 2015 kama ilivyoahidi.

4.    Kwa hali hii, ni ukweli usiofichika kuwa serikali ya CCM haiwezi kufikia lengo la kuwa na Taifa lililoelimika ifikapo 2025 kama inavyobainishwa kwenye dira (Vision 2025) na badala yake itafanikiwa kuwa na Taifa la watu mbumbumbu kwa wakati huo

5.    Kutokana na serikali dhaifu iliyopo madarakani kushindwa kubuni vyanzo vya ajira ili kuweza kuajiri watu wake wenye taaluma, ujuzi na wasio na ujuzi, ni dhahiri kuwa vijana hawa zaidi ya 800,000 watakuwa wanajihusisha na vitendo viovu kama ukabaji, madawa ya kulevya, wizi na ujambazi pamoja na ukahaba na hivyo kuwa na jamii ya watu waovu daima


HATUA ZA KUCHUKUA
1.    BAVICHA tunaitaka serikali kutangaza hali hii kuwa ni janga la Taifa na hivyo hatua za haraka kama vile, kutangaza sasa elimu bora ndio kipaumbele cha serikali kwa raia wake, kuboresha bajeti ya elimu ikiwemo kuboresha maslahi ya walimu na mazingira yao ya kufanya kazi.

2.    Kama suala la uharaka na la kutatua tatizo moja kwa moja, ni lazima kufumua mfumo wa elimu uliopo na kuhakikisha tunakuwa na mfumo unotambua vipaji vya watu na kuviendeleza kuliko kuendelea na huu wa kulazimisha elimu ya kukariri.

Licha ya mfumo huo, ni vema sasa wakaguzi wa shule wakapewa meno ya kuchukua hatua pale wanapobaini mambo hayaendi sawa kwenye baadhi ya shule kwani ni wazi kuwa kuna shule ambazo hazikidhi viwango vya kuitwa shule lakini bado zinaachwa kuendelea kuitwa shule.

3.    Kama sehemu ya uwajibikaji, BAVICHA inasisitiza kuwa Waziri, Katibu Mkuu pamoja na Mkurugenzi wa elimu ya Sekondari wajiuuzulu mara moja ndani ya siku 14 kama ilivyokwisha tangazwa na chama.

4.    Wananchi wanapaswa kuzingatia ukweli kuwa serikali ya CCM imeshindwa kutekeleza ahadi yake ya kutaka ufahulu kwa madaraja ya I, II na III kufikia asilimia 70 ifikapo 2009. Tumeshapita 2009 na leo hii ufahulu kwa madaraja hayo ni 6% tofauti 37% ya mwaka 2004. Suluhisho pekee hapa ni kuiondoa CCM madarakani kwa kuwa imeshindwa kutekeleza ilani yake na pia kushindwa kuisimamia serikali yake dhaifu.

5.    Wakati tunasubiri CCM kungo’oka madarakani Mwaka 2015, BAVICHA  tunaagiza viongozi wa Wilaya na Mikoa kufanya  mawasiliano na vijana ambao wamekumbwa na kadhia hii ili washiriki maandamano tutakayoyaandaa kwa  lengo la kuishinikiza serikali iliyoharibu maisha yao;

·        Kumtaka waziri, Katibu Mkuu wa Wizara na Mkurugenzi wa Sekondari kujiuzulu iwapo hawatakuwa wamefanya.

·        Kuishinikiza serikali sasa ifanye kipaumbele kuwa elimu bora kwa raia wake na hivyo pamoja na mambo mengine kuhakikisha walimu bora wanapatikana, bajeti ya elimu inaongezeka ikiwa ni pamoja na kuongeza mishahara na marupurupu ya waalimu kuanzia na bajeti ya mwaka 2013/2014

·        Kuitaka serikali ya CCM ieleze hatma ya maisha ya vijana waliofelishwa na mfumo mbovu wa elimu inaousimamia

6.    BAVICHA, tutawaagiza wabunge wetu vijana kuhakikisha kwenye vikao vijavyo vya bunge, Serikali inatoa hatma juu ya janga hili la kitaifa na majibu muafaka juu ya hatma ya malaki ya vijana waliofelishwa na vile vile kuhakikisha wanayapa masuala yote ya elimu kipaumbele namba moja kwenye mijadala ya kibunge

7.     Aidha, BAVICHA katika vikao vyake vikubwa viwili vilivyopita iliona tatizo hili na kuamua kuunda kamati ndogo kuangalia sekta nzima ya elimu inavyoathiri hali za Vijana nchini na kuja na mapendekezo yake. Kwa hatari hii ya Matokeo ya Kidato cha nne, kamati hii itazingatia hali hiyo na kupanua wigo wa kazi zake.
Imetolewa leo tarehe 21/02/2013, Jijini Dar es salaam na;
Deogratias Munishi
Katibu Mkuu – BAVICHA

Post a Comment

أحدث أقدم