Juzi, tarehe 20 Februari, 2013, kulifanyika kongamano kubwa na muhimu
mjini Dar es Salaam. Kongamano hilo liliandaliwa na Taasisi ya Masheikh
na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania. Kwa bahati nzuri nilipata fursa ya
kualikwa na kuhudhuria. Ni kongamano lililowaleta pamoja Waislamu na
Wakristo kujadili suala la amani ya nchi yetu. Washiriki walitoka katika
nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu, Kusini mwa Afrika, Asia na hata Ulaya.
Aidha, kongamano hilo liliandaliwa pia kwa munasaba wa ziara ya Rais wa
Baraza la Waislamu Duniani (World Muslim Congress), Profesa Abdullah
Omar Naseef.
Miongoni mwa waliowasilisha neon ni pamoja na Rais
mstaafu wa awamu ya pili, mzee wetu Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Profesa
Abdallah Nasees, Mufti Issa ibn Shaaban Simba, Askofu Sylvester
Gamanwa, Dr. Muhammad Rukala n.k
Miongoni mwa mada zilizonigusa
kwa kiasi kikubwa ni ile iliyowasilishwa na Dr. Muhammad Rukala kutoka
Burundi, ambaye ni waziri mwandamizi katika serikali ya Burundi. Mada
yake ilijikita katika kuzungumzia vyanzo vya Migogoro ya wenyewe kwa
wenyewe katika nchi za Maziwa Makuu.
Mada yake ilikuwa nzuri na iliyowasisimua watu wengi. Ilibainika kuwa cheche ndogo ndiyo inayozaa moto mkubwa.
Sote tunafahamu kuwa vurugu za nchini Rwanda zilihusisha makabila
mawili ya Wahutu na Watusi na zilipoteza roho za watu wapatao milioni
moja. Ni mauaji ambayo yameendelea kuiumiza dunia na jeraha lake
limekuwa gumu kulitibu.
Mpaka sasa zaidi ya watu milioni 5 wameshapoteza maisha katika vita ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Burundi imeshapoteza maisha ya watu laki 7 kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.
Mwaka 2007 nchini Kenya ghasia za baada ya Uchaguzi ziligharimu roho za
watu wapatao 15,00. Hizi ni takwimu za kutisha, ingawa wengine wanaweza
wasishtuke. Ukifuatilia vyanzo vya migogoro na maafa hayo ni pamoja na
ukosefu wa stahmala “tolerance” baina ya wanajamii husika. Pembezoni mwa
vyanzo hivyo kuna uchochezi wa vyombo vya habari. Angalia kesi
zinazoendelea katika mahakama za kimataifa kuhusu matukio hayo utaiona
orodha ya wanahabari ikijitokeza pia.
Taifa letu limekuwa
likipitia katika wakati mgumu sana wa mpasuko wa kijamii. Matukio ambayo
yamekuwa yakitishia uhai wa taifa letu yameendelea kujitokeza. Katikati
ya wimbi hili vimejitokeza vyombo vya habari kutoa taarifa potofu. Kwa
kweli mimi binafsi sina imani kabisa na vyombo vya habari vya Tanzania.
Mwenendo wake unatia shaka na sio wa kuaminika. Vimekuwa sehemu ya
mpasuko wa kijamii kwakuchochea mpasuko wenyewe, na vimekuwa vikihubiri
urongo bila haya wala aibu. Baada ya kuuawa kwa Padri Evaristus Mushi
kule Zanzibar, vyombo vya habari viliibuka na mambo ya ajabu, huku
vikitawaliwa na kukurupuka. Kwa mfano:
Vilidai kuwa kuna watu
waliokuwa wamekamatwa huko Kenya kwa mauaji ya Padri Mushi. Lakini hapo
jana Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa makosa ya jinai nchini alikanusha
kutokea kwa tukio hilo, akisema hakuna watu waliokamatwa huko Kenya.
Vilidai kuwa kuna mkono kutoka nje katika mauaji hayo, huku Boko Haram
ikitajwa. Lakini vyombo hivyo vimesahau kuwa utafiti unaonesha kuwa
hakuna kundi lenye muundo wa kitaasisi au shirika linaloitwa Boko Haram.
Ukurupukaji huu uliashiriwa pia katika kongamano lililoandaliwa na
Taasisi ya Masheikh. Wakati wa kongamano hilo, lilitajwa gazeti moja
lililohusisha tukio hilo la Mtandao wa Al-Qaeda bila hata kufanya
utafiti wa kina. Serikali inatakiwa kuchukua hatua dhidi ya vyombo vya
habari kama hivyo vinavyotoa kauli za kupotosha, huku taarifa rasmi za
polisi zikitoa taarifa zinazopingana na taarifa potofu za vyombo vya
habari.
Kwa hakika, vyombo vya habari vinatakiwa kuliomba radhi taifa kwa kuupotosha umma. Mwenendo wake unatia shaka.
Ninahitimisha kwa kutoa tahadhari kuwa ukurupukaji wa vyombo vya habari vinatupeleka pabaya.
إرسال تعليق