
Mhariri
Mtendaji wa Gazeti la Nipashe, Jesse Kwayu (wa kwanza kushoto) Mhariri
Mtendaji wa Free Media, Ansbert Ngurumo (aliyesimama kushoto( na Katibu
Mkuu Jukwaa la Wahariri, Nevil Meena (Kulia).
Hali ya
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda, imeanza
kuimarika baada ya kuanza mazoezi mepesi ya kusimama, kutembea, kuweza
kukaa kwa muda na kushiriki mazungumzo.
Taarifa
iliyotolewa na Katibu wa TEF, Neville Meena, imesema kuwa Kibanda ambaye
pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006), hali yake
inatia moyo na kuomba Watanzania waendelee kumuombea ili apone haraka.
Meena na
wahariri watendaji wengine wa magazeti ya NIPASHE, Jesse Kwayu na Free
Media, Ansbert Ngurumo, wapo nchini Afrika Kusini, jijini Johannesburg
katika hospitali ya Milpark, alikolazwa Kibanda, kumjulia hali wakati
akiendelea kupata matibabu kutokana na tukio la kushambuliwa.
“Jana
(Ijumaa) kutwa tulishinda naye hosipitalini na kwa ujumla hali yake
inaendelea kuimarika vizuri. Kama tulivyowaarifu tangu juzi, ameanza
mazoezi mepesi ya kusimama na kutembea na anaweza kukaa kwa muda na
kushiriki mazungumzo. Kwa hakika amechangamka na anatia moyo,” ilisema
taarifa ya Neville.
“Hata hivyo,
bado mwenyekiti wetu ataendelea kubakia hospitalini kwa matibabu zaidi
kama wanavyoshauri madaktari wake. Jambo la msingi tuendelee kumwombea
katika sala zetu na wale ambao watapata fursa wafike kumjulia hali na
kumtia moyo,” iliongeza taarifa hiyo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
إرسال تعليق