MKAKATI wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kugatua madaraka kwa
kutafsiri sera yake ya majimbo, umeanza kazi rasmi katika kanda zake 10,
na sasa Kanda ya Ziwa Magharibi imetangaza kikosi kazi kilichosheni
wataalamu wa fani mbalimbali.
Kanda hiyo
inayohusisha mikoa ya Geita, Kagera na Mwanza, ilizinduliwa wiki
iliyopita mkoani Mwanza, mbele ya Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman
Mbowe.
Mkutano wa
uzinduzi wa kanda hiyo uliohudhuriwa na wajumbe wa mabaraza ya uongozi,
wabunge na madiwani kutoka mikoa hiyo, uliwachagua watu sita kuunda timu
ya muda ya uratibu wa kanda kwa miezi mitatu.
Waliochaguliwa
kuongoza kanda hiyo ni Peter Mekere (Mwenyekiti), Dk. Rodrick Kabangila
(Makamu Mwenyekiti), Renatus Bujiku (Katibu), Cecilia Odemba (Mhazini)
na Tungaraza Njugu.
Mekere ni
mtaalamu mshauri wa biashara na utawala na mafunzo ya biashara. Ana
shahada ya biashara na uongozi na stashahada ya ualimu. Ni mwenyekiti wa
kamati ya fedha na mipango ya Shirika la nyumba la Taifa (NHC), Kanda
ya Ziwa.
Kabangila ni
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Afya, Bugando, daktari bingwa wa
magonjwa ya binadamu na Makamu wa Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania
(MAT).
Ana shahada
ya uzamili ya magonjwa ya wanadamu, shahada ya udaktari, shahada ya
uzamili, epidemilojia na utafiti wa huduma za afya.
Bujiku ni
mwalimu, mtaalamu mshauri, ofisa wa kanda ya ziwa wa shirika la ACORD
kwa muda sasa. Ana shahada ya uzamili, uongozi na mipango, shahada ya
Elimu, Stashahada ya Maendeleo na misaada ya kiutu.
Njugu
amekuwa Meneja wa shirika la kijamii (CACT-Mwanza 2008-2010), meneja wa
Chama cha Akiba na Mikopo (MWAUWASA SACCOS 2007 hadi sasa) ana cheti cha
uhasibu kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) na cheti cha
sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Odemba ni
Meneja masoko katika usafiri wa anga, mkurugenzi wa kampuni ya uwakala
ya usafiri wa anga, na amewahi kuwa katibu wa kamati ya uhamasishaji ya
vuguvugu la mabadiliko (M4C) kanda ya Ziwa.
Akizungumza
na gazeti hili, Mekere alisema: “Timu yetu imetokana na watu wenye
taaluma mbalimbali ambao wamekuwa wakitafuta nafasi kukisaidia chama
kupitia taaluma zao. Tunaipongeza CHADEMA kwa kuanzisha sera ya majimbo
kuandaa Watanzania kupata maendeleo kwa haraka kwani utaratibu huu wa
majimbo ya chama unarudisha mamlaka kwa wananchi, na ni maandalizi ya
kuongoza nchi.
“Kwa
utaratibu huu wananchi wamerudishiwa madaraka yao, wana nafasi ya kuamua
kuhusu rasilimali zao na kupanga namna ya kuzitumia. Utaratibu huu
unaharakisha maendeleo tofauti na mfumo wa kimikoa uliowekwa na CCM.”
Post a Comment