Wakenya wasubiri kwa hamu siku ya uchaguzi, waungana kwa matumaini ya amani

Mwanaume anayetembea akipita katika ukuta ulioandikwa kwa kupuliziwa rangi unaosema "Tunahitaji amani nchini Kenya" katika kitongoji ya Kibera huko Nairobi tarehe 27 Februari, 2013. [Phil Moore/AFP]
Na Bosire Boniface, Wajir na Rajab Ramah, Nairobi

Huku uchaguzi wa Kenya unaosubiriwa kwa hamu utakaofanyika tarehe 4 Machi ukiwa umekaribia, Wakenya wanasema wana matumaini makubwa na wana shauku, bado wanaungana katika matamanio ya tukio hilo kupita kwa amani.

Siku ya Jumatatu,wapiga kura wataelekea katika vituo vya kupigia kura kumchagua rais,magavana,maseneta,wabunge, wawakilishi wa wanawake kitaifa na wawakilishi wa kata. Kama hakuna kati ya wagombea nane wa urais atakayepata kura nyingi zaidi, duru ya pili ya uchaguzi utafanyika tarehe 11 Aprili.

Tofauti na ilivyokuwa katika uchaguzi uliopita ambapo kulikuwa na karatasi moja tu ya kupigia kura, wapiga kura sasa watatumia karatasi sita zenye rangi tofauti, moja kwa kila nafasi inayogombewa.

Takriban Wakenya milioni 14.3 walijiandikisha kupiga kura mwaka jana, ingawa wengi hawakuhakiki taarifa za uandikishaji wao mwezi Januari, hili halitaathiri uwezo wao wa kupiga kura, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilieleza.

Wapigakura wa Nairobi wana matumaini ya amani

Ouma Omollo, mwenye umri wa miaka 45, ambaye ni muuza magazeti katika Barabara ya Kenyatta huko Nairobi, alisema jitihada za amani ambazo wagombea wa urais waliahidi katika mkutano wa maombi na midahalo zimesaidia kupunguza wasiwasi miongoni mwa wafuasi wa wagombea hao.

Wagombea wa urais nchini Kenya, kutoka kushoto, James Ole Kiyiapi, Uhuru Kenyatta na Raila Odinga wahudhuria mkutano wa maombi tarehe 24 February, 2013 yaliyoongozwa na David Owuor (mwenye nguo nyeupe) mjini Nairobi. [Stringer/AFP]

"Tulijifunza somo letu katika vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi wa mwaka 2007-2008," alisema Omollo, ambaye atapiga kura yake huko Kibera. "Maskini waligombana na ndiyo waliopoteza zaidi. Lile lilikuwa ni somo hakuna yeyote atakayefikiria kulijaribu tena."

Takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 300,000 walikosa makazi wakati wa vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Omollo alitoa wito kwa IEBC kuimarisha elimu ya mpiga kura hadi siku ya uchaguzi, hususan katika maeneo ya vijijini na mijini ambayo yanakaliwa na watu maskini. "Nilikosa kushiriki katika uchaguzi wa majaribio tarehe 2 Februari," alisema, akiongeza kwamba ungeweza kumpa fursa ya kumfanya ajizoeshe mwenyewe na mchakato wa uchaguzi.

Alisema kwa kuwa na karatasi sita za kupigia kura kunaweza kusababisha kuchanganyikiwa. "Ila tu tuwe na taarifa ya kutosha kabla ya tarehe ya uchaguzi, tutapatwa na mshtuko mbaya," aliiambia Sabahi.

Joyce Njoki, mwenye umri wa miaka 30, ofisa tawala wa kampuni binafsi ya teknolojia ya habari huko Nairobi, alielezea woga wake kwamba uchaguzi utasababisha wimbi jingine la vurugu za kisiasa.

"Nina wasiwasi kama jitihada za amani zimeyeyusha chuki za kisiasa kutokana na kutokuwa na uvumilivu wa kikabila wa Wakenya," aliiambia Sabahi, akiongeza bila ya kujali matokeo ya uchaguzi yoyote, baadhi ya maeneo ya Nairobi na nchi kunaweza kuwa na mapigano.

"Ninajiandaa kwa hali mbaya, lakini ninaomba kwamba amani itawale," alisema, akiongeza kwamba ameanza kuhifadhi vyakula nyumbani kwake.

Siku ya kupiga kura, Njoki alisema yeye na mume wake watakwenda katika kituo cha kupigia kura mapema asubuhi kupiga kura zao na kurejea nyumbani kufuatilia kinachoendelea katika televisheni.

Mary Kimutai mwenye umri wa miaka 24, mwanafunzi wa mwaka wa mwisho wa sheria katika Chuo Kikuu cha Nairobi, alisema ana uhakika kwamba uchaguzi utakuwa wa amani kwa sababu mchakato wa kupiga kura utafanyika vizuri.

Kimutai, ambaye atarudi nyumbani kwake Eldoret kushiriki katika uchaguzi, alisema IEBC inaaminiwa na wananchi na imethibitisha uwezo wake kuendesha uchaguzi wa haki na wa kuaminika.

"Hapo awali, watu walichukua mitaa kwa sababu chombo na mahakama vimekuwa vikichukuliwa kama wafuasi, na kwa hiyo haviwezi kuaminiwa kupatanisha mgogoro wa uchaguzi au kusimamia uchaguzi wa kuaminika," aliiambia Sabahi. "Lakini sasa tuna chombo huru, mahakama iliyoundwa upya ambapo Wakenya wanaikubali na kuamini itafanya kazi nzuri."

Kimutai alisema alishiriki katika uchaguzi wa majaribio na kuona mchakato ni rahisi kuliko alivyotarajia. Hata wapiga kura wasio na elimu ya mchakato huo wataona upigaji kura ni rahisi na wenye uelekezaji mdogo, alisema.

John Karanja, mwenye umri wa miaka 23, mshona viatu katika soko la Muthurwa katika viunga vya Nairobi, alisema alitarajia wagombea urais ambao watashindwa kukubali kushindwa mara moja au kupeleka masuala yao mahakamani kama wana malalamiko.

"Tunatarajia muda kama huu walioshindwa watakubali kushindwa," aliiambia Sabahi. "Kama wanahisi wameibwa, wasiwahamasishe wafuasi wao kupinga kushindwa kwao mitaani, bali waende mahakamani. Ili kuepuka kusababisha wasiwasi usio wa lazima miongoni mwa wananchi, IEBC inapaswa kuharakisha na kutangaza rasmi matokeo ili kuepuka minong'ono."

Wakenya wa Kaskazini wafanya kazi kuepuka wasiwasi
Hashim Ali Abdi alisafiri kutoka Nairobi mahali anapofanya kazi kama meneja wa hoteli kwenda kwenye kijiji alichozaliwa cha Rhamu katika wilaya ya Mandera kushiriki katika uchaguzi.

Abdi alisema alikuwa na matumaini kuwa upigaji kura ungefanyika pasipo tukio lolote, licha ya wasiwasi wa sasa wa kuibuka kwa mapigano kati ya Degodia na Gurreh, makabila ya ndani mawili yenye historia ya ghasia juu ya nafasi zinazopigiwa kura.

"Wakati wote tumekuwa tukiishi pamoja, lakini siasa aghalabu zimekuja baina yetu," aliiambia Sabahi. "Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, makabila haya mawili yamekuwa na mapigano yasiyopungua mara nne, lakini kuna vikao vinavyoendelea kati ya jumuiya hizi mbili kuhakikisha utulivu kabla, wakati na baada ya kupiga kura."

Katika wilaya jirani ya Wajir, Ali Abdi Bishar, mkaazi mwenye umri wa miaka 39 wa Griftu, alisema pia ana matumaini ya uchaguzi kufanyika kwa amani.

"Tumekuwa katika siasa zinazofuata matakwa ya mtu binafsi zilizoendelea kwa muda mrefu ambazo ziliathiri tija zetu. Nimekuwa nikiangalia mbele kwenye siku hii ya kuchagua viongozi tunaowataka na kuwa mbali na siasa ili tuweze kupata maendeleo," aliiambia Sabahi.

"Baada ya kupiga kura, nitarudi nyumbani na kufuatilia matokeo kupitia vituo vya redio vya ndani," alisema. "Nina imani mgombea wa uchaguzi wangu atashinda; kama hatachaguliwa, nitakatishwa tamaa, lakini matumani yangu ni kwamba yeyote atakayeshinda ana mvuto wa watu wa dhati."

Huku siku ya kupiga kura inavyowadia, Shirika la Amani na Maendeleo (WPDA) la Wajir limekuwa likifanya mikutano kwenye ukumbi wa mji kuhimiza upigaji kura wa amani.

"Kitu tunachokiona sasa ni msaada wa dhati tu kwa mgombea husika na kufanya utani na wale wanaompinga," alisema mratibu wa WPDA Hussein Adan Mohamud, akiongezea kwamba hakujakuwa na ishara ya vurugu.

Wasiwasi wa wapiga kura wa Pwani

Vipeperushi vimesambazwa katika jimbo la Pwani vikiwataka wakaazi wa Pwani kutopiga kura, jambo lililosababisha wasiwasi. Harriet Mkawale, mkazi wa wilaya ya Kwale mwenye umri wa miaka 39, alisema watu wamekuwa wakitembelea majumbani wakishawishi watu kutoshiriki katika zoezi hili.

"Maofisa wa usalama wametuhakikishia usalama wetu, lakini kuna dalili za hofu kwa sababu hatujui ni nani anayeleta vitisho," aliiambia Sabahi. "Ni suala lenye utata kwa sababu kundi lililojitenga la Baraza la Jamhuri la Mombasa (MRC) limehubiri hadharani amani na kuwaomba wananchi kushiriki."

MRC awali ilitishia kugomea uchaguzi mkuu na kuleta ombi la kuizuia serikali ya Kenya isifanye uchaguzi katika Jimbo la Pwani, ambalo mahakama moja ya Kenya ilizuia mwezi Disemba.

Mkuu wa Polisi wa Jimbo la Pwani Aggrey Adoli alisema polisi wanachunguza chanzo cha vipeperushi hivyo. "Tumeweka hatua za ulinzi ili kuhakikisha kwamba watu wanashiriki katika zoezi bila ya kukatishwa. Pia tunaweka tahadhari kwa shughuli zozote zinazohusiana na ugaidi," aliiambia Sabahi.

Mkawale alisema atapiga kura licha ya mchanganyiko, na ataungana na familia yake nyumbani kusubiri matokeo.

Post a Comment

Previous Post Next Post