Mwanaume anayetembea akipita katika ukuta ulioandikwa kwa kupuliziwa rangi unaosema "Tunahitaji amani nchini Kenya" katika kitongoji ya Kibera huko Nairobi tarehe 27 Februari, 2013. [Phil Moore/AFP] |
Na Bosire Boniface, Wajir na Rajab Ramah, Nairobi
Huku uchaguzi wa Kenya unaosubiriwa kwa hamu utakaofanyika tarehe 4
Machi ukiwa umekaribia, Wakenya wanasema wana matumaini makubwa na wana
shauku, bado wanaungana katika matamanio ya tukio hilo kupita kwa amani.
Siku ya Jumatatu,wapiga kura wataelekea katika vituo vya kupigia kura
kumchagua rais,magavana,maseneta,wabunge, wawakilishi wa wanawake
kitaifa na wawakilishi wa kata. Kama hakuna kati ya wagombea nane wa
urais atakayepata kura nyingi zaidi, duru ya pili ya uchaguzi utafanyika
tarehe 11 Aprili.
Tofauti na ilivyokuwa katika uchaguzi uliopita ambapo kulikuwa na
karatasi moja tu ya kupigia kura, wapiga kura sasa watatumia karatasi
sita zenye rangi tofauti, moja kwa kila nafasi inayogombewa.
Takriban Wakenya milioni 14.3 walijiandikisha kupiga kura mwaka jana,
ingawa wengi hawakuhakiki taarifa za uandikishaji wao mwezi Januari,
hili halitaathiri uwezo wao wa kupiga kura, Tume Huru ya Uchaguzi na
Mipaka (IEBC) ilieleza.
Wapigakura wa Nairobi wana matumaini ya amani
Ouma Omollo, mwenye umri wa miaka 45, ambaye ni muuza magazeti katika
Barabara ya Kenyatta huko Nairobi, alisema jitihada za amani ambazo
wagombea wa urais waliahidi katika mkutano wa maombi na midahalo
zimesaidia kupunguza wasiwasi miongoni mwa wafuasi wa wagombea hao.
Wagombea wa urais nchini Kenya, kutoka
kushoto, James Ole Kiyiapi, Uhuru Kenyatta na Raila Odinga wahudhuria
mkutano wa maombi tarehe 24 February, 2013 yaliyoongozwa na David Owuor
(mwenye nguo nyeupe) mjini Nairobi. [Stringer/AFP]
"Tulijifunza somo letu katika vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi wa
mwaka 2007-2008," alisema Omollo, ambaye atapiga kura yake huko Kibera.
"Maskini waligombana na ndiyo waliopoteza zaidi. Lile lilikuwa ni somo
hakuna yeyote atakayefikiria kulijaribu tena."
Takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 300,000 walikosa makazi wakati
wa vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Omollo alitoa wito kwa IEBC kuimarisha elimu ya mpiga kura hadi siku ya
uchaguzi, hususan katika maeneo ya vijijini na mijini ambayo yanakaliwa
na watu maskini. "Nilikosa kushiriki katika uchaguzi wa majaribio tarehe
2 Februari," alisema, akiongeza kwamba ungeweza kumpa fursa ya kumfanya
ajizoeshe mwenyewe na mchakato wa uchaguzi.
Alisema kwa kuwa na karatasi sita za kupigia kura kunaweza kusababisha
kuchanganyikiwa. "Ila tu tuwe na taarifa ya kutosha kabla ya tarehe ya
uchaguzi, tutapatwa na mshtuko mbaya," aliiambia Sabahi.
Joyce Njoki, mwenye umri wa miaka 30, ofisa tawala wa kampuni binafsi ya
teknolojia ya habari huko Nairobi, alielezea woga wake kwamba uchaguzi
utasababisha wimbi jingine la vurugu za kisiasa.
"Nina wasiwasi kama jitihada za amani zimeyeyusha chuki za kisiasa
kutokana na kutokuwa na uvumilivu wa kikabila wa Wakenya," aliiambia
Sabahi, akiongeza bila ya kujali matokeo ya uchaguzi yoyote, baadhi ya
maeneo ya Nairobi na nchi kunaweza kuwa na mapigano.
"Ninajiandaa kwa hali mbaya, lakini ninaomba kwamba amani itawale,"
alisema, akiongeza kwamba ameanza kuhifadhi vyakula nyumbani kwake.
Siku ya kupiga kura, Njoki alisema yeye na mume wake watakwenda katika
kituo cha kupigia kura mapema asubuhi kupiga kura zao na kurejea
nyumbani kufuatilia kinachoendelea katika televisheni.
Mary Kimutai mwenye umri wa miaka 24, mwanafunzi wa mwaka wa mwisho wa
sheria katika Chuo Kikuu cha Nairobi, alisema ana uhakika kwamba
uchaguzi utakuwa wa amani kwa sababu mchakato wa kupiga kura utafanyika
vizuri.
Kimutai, ambaye atarudi nyumbani kwake Eldoret kushiriki katika
uchaguzi, alisema IEBC inaaminiwa na wananchi na imethibitisha uwezo
wake kuendesha uchaguzi wa haki na wa kuaminika.
"Hapo awali, watu walichukua mitaa kwa sababu chombo na mahakama
vimekuwa vikichukuliwa kama wafuasi, na kwa hiyo haviwezi kuaminiwa
kupatanisha mgogoro wa uchaguzi au kusimamia uchaguzi wa kuaminika,"
aliiambia Sabahi. "Lakini sasa tuna chombo huru, mahakama iliyoundwa
upya ambapo Wakenya wanaikubali na kuamini itafanya kazi nzuri."
Kimutai alisema alishiriki katika uchaguzi wa majaribio na kuona
mchakato ni rahisi kuliko alivyotarajia. Hata wapiga kura wasio na elimu
ya mchakato huo wataona upigaji kura ni rahisi na wenye uelekezaji
mdogo, alisema.
John Karanja, mwenye umri wa miaka 23, mshona viatu katika soko la
Muthurwa katika viunga vya Nairobi, alisema alitarajia wagombea urais
ambao watashindwa kukubali kushindwa mara moja au kupeleka masuala yao
mahakamani kama wana malalamiko.
"Tunatarajia muda kama huu walioshindwa watakubali kushindwa," aliiambia
Sabahi. "Kama wanahisi wameibwa, wasiwahamasishe wafuasi wao kupinga
kushindwa kwao mitaani, bali waende mahakamani. Ili kuepuka kusababisha
wasiwasi usio wa lazima miongoni mwa wananchi, IEBC inapaswa kuharakisha
na kutangaza rasmi matokeo ili kuepuka minong'ono."
Wakenya wa Kaskazini wafanya kazi kuepuka wasiwasi
Hashim Ali Abdi alisafiri kutoka Nairobi mahali anapofanya kazi kama
meneja wa hoteli kwenda kwenye kijiji alichozaliwa cha Rhamu katika
wilaya ya Mandera kushiriki katika uchaguzi.
Abdi alisema alikuwa na matumaini kuwa upigaji kura ungefanyika pasipo
tukio lolote, licha ya wasiwasi wa sasa wa kuibuka kwa mapigano kati ya
Degodia na Gurreh, makabila ya ndani mawili yenye historia ya ghasia juu
ya nafasi zinazopigiwa kura.
"Wakati wote tumekuwa tukiishi pamoja, lakini siasa aghalabu zimekuja
baina yetu," aliiambia Sabahi. "Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita,
makabila haya mawili yamekuwa na mapigano yasiyopungua mara nne, lakini
kuna vikao vinavyoendelea kati ya jumuiya hizi mbili kuhakikisha utulivu
kabla, wakati na baada ya kupiga kura."
Katika wilaya jirani ya Wajir, Ali Abdi Bishar, mkaazi mwenye umri wa
miaka 39 wa Griftu, alisema pia ana matumaini ya uchaguzi kufanyika kwa
amani.
"Tumekuwa katika siasa zinazofuata matakwa ya mtu binafsi zilizoendelea
kwa muda mrefu ambazo ziliathiri tija zetu. Nimekuwa nikiangalia mbele
kwenye siku hii ya kuchagua viongozi tunaowataka na kuwa mbali na siasa
ili tuweze kupata maendeleo," aliiambia Sabahi.
"Baada ya kupiga kura, nitarudi nyumbani na kufuatilia matokeo kupitia
vituo vya redio vya ndani," alisema. "Nina imani mgombea wa uchaguzi
wangu atashinda; kama hatachaguliwa, nitakatishwa tamaa, lakini matumani
yangu ni kwamba yeyote atakayeshinda ana mvuto wa watu wa dhati."
Huku siku ya kupiga kura inavyowadia, Shirika la Amani na Maendeleo
(WPDA) la Wajir limekuwa likifanya mikutano kwenye ukumbi wa mji
kuhimiza upigaji kura wa amani.
"Kitu tunachokiona sasa ni msaada wa dhati tu kwa mgombea husika na
kufanya utani na wale wanaompinga," alisema mratibu wa WPDA Hussein Adan
Mohamud, akiongezea kwamba hakujakuwa na ishara ya vurugu.
Wasiwasi wa wapiga kura wa Pwani
Vipeperushi vimesambazwa katika jimbo la Pwani vikiwataka wakaazi wa
Pwani kutopiga kura, jambo lililosababisha wasiwasi. Harriet Mkawale,
mkazi wa wilaya ya Kwale mwenye umri wa miaka 39, alisema watu wamekuwa
wakitembelea majumbani wakishawishi watu kutoshiriki katika zoezi hili.
"Maofisa wa usalama wametuhakikishia usalama wetu, lakini kuna dalili za
hofu kwa sababu hatujui ni nani anayeleta vitisho," aliiambia Sabahi.
"Ni suala lenye utata kwa sababu kundi lililojitenga la Baraza la
Jamhuri la Mombasa (MRC) limehubiri hadharani amani na kuwaomba wananchi
kushiriki."
MRC awali ilitishia kugomea uchaguzi mkuu na kuleta ombi la kuizuia
serikali ya Kenya isifanye uchaguzi katika Jimbo la Pwani, ambalo
mahakama moja ya Kenya ilizuia mwezi Disemba.
Mkuu wa Polisi wa Jimbo la Pwani Aggrey Adoli alisema polisi
wanachunguza chanzo cha vipeperushi hivyo. "Tumeweka hatua za ulinzi ili
kuhakikisha kwamba watu wanashiriki katika zoezi bila ya kukatishwa.
Pia tunaweka tahadhari kwa shughuli zozote zinazohusiana na ugaidi,"
aliiambia Sabahi.
Mkawale alisema atapiga kura licha ya mchanganyiko, na ataungana na familia yake nyumbani kusubiri matokeo.
Via sabahionline.com
إرسال تعليق