Wakati
Chama Cha Wananchi CUF kikijiandaa na uchaguzi mkuu wa ndani ya chama
hicho kuanzia mwezi mei mwaka huu, kimesema hakitomvulia mwanachama
atakayejihusisha na makundi kwa kujitafutia uongozi.
Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad ameeleza hayo leo
wakati akifungua mkutano mkuu wa CUF Wilaya ya Mjini uliofanyika ukumbi
wa Jamat-Khan mjini Zanzibar.
Amesema mwanachama yeyote atakayebainika kujihusisha na makundi kwa
kutafuta uongozi, kamwe chama hakitomvumilia na anaweza kupoteza sifa ya
kugombea kuchaguliwa nafasi aliyoiomba.
Amefahamisha kuwa kila mwanachama ana haki ya kugombea nafasi yoyote
ndani ya chama na kuwahimiza kufanya hivyo bila ya woga, lakini
wasijihusishe na makundi katika kugombea nafasi hizo.
“Anayetaka kugombea nafasi ya Mwenyekiti Taifa, Katibu Mkuu na nafasi
nyengine zote ruksa, lakini hatutaki makundi kwani makundi ndio
yanayoua chama, na mimi nikiamua kugombea tutashindana kwa kura”,
alieleza Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Amesema chama cha CUF taifa kimejipanga kusimamia chaguzi hizo ili
ziwe huru na haki, na kuhakikisha kuwa kila mwanachama anataka kugombea
nafasi ya uongozi anapatiwa fursa hiyo.
Akizungumzia kuhusu uhai wa Chama hicho Maalim Seif amesisitiza haja
ya kufuatwa kikamilifu kwa katiba ya chama hicho, ikiwa ni pamoja na
kuitishwa vikao kwa mujibu wa katiba.
Ameeleza kuwa vikao ni muhimu katika kuimarisha uhai wa chama, kwani
ndivyo vyenye haki ya kujadili na kutoa maamuzi juu ya maendeleo ya
chama, sambamba na kuwahimiza kuendeleza Jumuiya za chama hasa za vijana
na wanawake.
Katibu Mkuu huyo wa CUF amekemea tabia ya wanachama kupikiana majungu
na kuwataka kutumia vikao halali vya chama kukosoana na kurekebishana.
Kushambuliwa kwa Kibanda na matukio ya kihalifu nchini.
Katika mkutano huo Maalim Seif amelaani vikali kitendo cha
kushambuliwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania ambaye pia
ni mhariri mtendaji wa kampuni ya New Habari Absalom Kibanda hivi
karibuni jijini Dar es Salaam.
Amesema Kibanda ni mwandishi mzuri, makini na mweledi, na kwamba
kitendo hicho cha dhulma na cha kinyama kimempotezea hadhi mwandishi
huyo anayetegemewa na taifa.
Ameliomba jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina kuwabaini
waliohusika na tukio hilo ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Nchimbi hakuitendea haki Zanzibar.
Akizungumzia kuhusu matukio ya kihalifu yaliyotokea Zanzibar likiwemo
la kuuwawa kwa Padri Evarist Mushi, Maalim Seif amesema Waziri wa mambo
ya ndani Emannuel Nchimbi hakuitendea haki Zanzibar kwa kutamka kuwa ni
kitendo cha ugaidi, na badala yake ameidhulumu Zanzibar kiuchumi.
Amesema sekta kuu inayotegemewa kwa uchumi wa Zanzibar ni Utalii,
hivyo kuitangazia dhama ya ugaidi ni kuidhulumu na kuipotezea fursa
zake.
Ameiomba serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kuziweka bayana
taarifa za uchunguzi wa tukio hilo ili wananchi waweze kuzifahamu na
hatimaye kuweza kuisafisha Zanzibar na dhana ya kigaidi.
Daftari la kudumu la wapiga kura.
Maalim Seif amewataka vijana kushajihishana kufuatilia upatikanaji wa
vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi, ili waweze kusajiliwa katika
daftari la kudumu la wapiga kura.
Amesema bado vijana wengi hawana ZAN ID huku wakiwa wameshatimiza
umri wa kupatiwa vitambulisho hivyo, na kuwataka kuongeza juhudi
kuvitafuta ili waweze kupatiwa haki hiyo ya kikatiba itakayowawezesha
kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Amerejea kauli yake ya kuwahimiza Wazanzibari kuendeleza umoja wao,
na kutokubali kuingizwa katika malumbano, ili kuinusuru Zanzibar
kurejeshwa ilikotoka.

Post a Comment