CHAMA Cha
Mapinduzi (CCM) kimesema kauli ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa kwamba kuna baadhi ya watumishi
wa vyombo vya dola wanaripoti kwake, kimesababisha baadhi ya wananchi
kukosa imani na vyombo hivyo.
Kauli hiyo
ilitolewa jana na Mkoa Maalum wa CCM Dar es Salaam baada ya kikao chao
kutathimini mambo na matukio mbalimbali yanayolitikisa taifa kwa sasa.
Katika
taarifa yao iliyosainiwa na Katibu wa Wilaya ya Dar es Salaam (ya
kisiasa - CCM), Daniel Zenda ilisema kuwa Dk. Slaa amekuwa akitoa kauli
hizo mara kwa mara tangu wakati wa kampeni za urais mwaka 2010, lakini
hajaitwa kuulizwa wala kuchukuliwa hatua.
“Lakini pia
kauli ya Dk. Slaa imesababisha wananchi wakose imani na Idara ya Usalama
na zaidi kupoteza imani juu ya uwezo wa serikali kuwalinda na
kuwahakikishia usalama wa maisha yao, ambapo ni jukumu la kikatiba la
serikali,” ilisema taarifa hiyo.
Vijana hao
wa CCM, wameitaka Idara ya Usalama kumhoji kwa kina Dk. Slaa athibitishe
madai yake kuwa baadhi ya watendaji wa taasisi hiyo muhimu na nyeti
wanaripoti kwake kinyume na utaratibu, kanuni na maadili ya taasisi
hiyo.
Chama hicho pia kimelaani vikali matukio ya kuvamiwa, kudhuru mwili na kuuawa kwa baadhi ya viongozi wa dini na wanahabari.
Kwa mujibu
wa taarifa hiyo, mkoa huo umesikitishwa na tukio la kushambuliwa
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF) na Mhariri Mtendaji wa New Habari
2006, Absalom Kibanda.
“Tunavitaka
vyombo vya dola kuwakamata, kuwachukulia hatua za kisheria wote
waliothibitika kuhusika na matukio ya namna hiyo bila kuangalia itikadi
za kivyama, cheo ama kundi.
“Na pia
kuyataka makundi ya kijamii, wanaharakati na wanasiasa kuacha
kuingilia/kuvuruga kwa namna yeyote taratibu za kisheria na kiusalama,”
ilisema taarifa hiyo.
إرسال تعليق