
Mtoto
anayedaiwa nguo zake kuwaka moto wa maajabu na kuteketeza nyumba katika
kijiji cha Kabuku, wilayani Handeni mkoani Tanga, Christina Mjema (12
)pichani, hivi sasa yuko Dar es Salaam akiendelea vizuri baada ya
kuombewa. Mtoto
huyo, ambaye aliamriwa ahifadhiwe kituo cha polisi baada ya wananchi
kumuogopa,hata hivyo, kanisa lililoamua kumsaidia kwa maombezi limekuwa
likishuhudia mambo ya ajabu yakitokea kanisani hapo yanayodaiwa
kuambatana na nguvu za giza.
Mtoto huyo
anapatiwa huduma ya maombezi katika kanisa la House of Prayer shield of
Faith Christian Fellowship maarifa kwa jina la kanisa la `Mzee wa Yesu'
eneo la Boko Magengeni jijini Dar es Salaam.
Christina,
mwanafunzi wa darasa la sita shule ya Msingi Kabuku, Wilaya ya Handeni
mkoani Tanga, alikuwa anakabiliwa na tatizo la kuwaka moto nguo zake
bila ya yeye mwenyewe kuungua pamoja na kusababisha nyumba ya wazazi
wake kuteketea kwa moto.
Akizungumza
na NIPASHE, Mchungaji kiongozi msaidizi Justine Materu, alisema mtoto
huyo alifikishwa kanisani hapo Februari 20, mwaka huu, baada ya kupata
taarifa ya matatizo yake kupitia vyombo vya habari.
Alisema mara
alipofikishwa hapo wachungaji wa kanisa hilo walimfanyia maombezi
mazito kiasi ambacho hali hiyo imetoweka na ameanza kuishi kama watu
wengine.
Alisema kabla ya kumchukua, hali ya mtoto huyo ilikuwa mbaya kiasi ambacho hakuweza kuvaa nguo yoyote kwa kuhofia kuwaka moto.
"Tunamfanyia
maombi mazito ili hizi nguvu za giza alizokuwa nazo zitoweke kabisa,
tumeanza kupata mafanikio makubwa kwa sasa hawaki moto tena," alisema
Mchungaji Materu.
Mchungaji
Materu alisema kazi ya kuombea mtoto huyo imekuwa ngumu baada ya kila
siku kanisa hilo kuvamiwa na kundi la watu kutoka kijijini kwao wakitaka
wamchukue.
Alisema
kutokana na tatizo hilo wamechukua uamuzi wa kumzuia kanisani hapo
wakati wakiendelea kumfanyia maombezi hadi hapo watu waliohusika na
kumfanyia kitendo hicho waangamizwe.
"Tumemzuia
kurudi nyumbani kwao mpaka watu hawa wanaokuja hapa usiku
watakaposhindwa, tunapambana sana lakini kwa nguvu ya Yesu watashindwa,"
aliongeza kusema.
Aidha,
Mchungaji Materu alisema tatizo lililompata Christina limekuwa kitu cha
kawaida kwao, kwani mara nyingi wanatoa huduma ya maombezi kwa watu
wenye matatizo mbalimbali ya mateso yanayotokana na nguvu ya giza,
uchawi, mapepo na kupona kabisa.
Pamoja na
maombezi hayo, Christina bado anakabiliwa na tatizo la kukosa nguo baada
ya nguo zote kuungua moto, huku wazazi nao wakikabiliwa na umasikini
mkubwa kutokana na vitu vyao pamoja na duka lao kuunguzwa na moto huo wa
ajabu.
Kutokana na
tatizo hilo, mchungaji Materu amewaomba wasamaria wema kumsaidia mtoto
huyo ili aweze kuishi kama watoto wengine wakati anaendelea na huduma ya
maombezi.
Kwa upande
wake Christina alisema hali yake kwa sasa imerudi kama zamani, kwani
tangu afike eneo hilo hakupata tukio la kuwaka moto wala vitu
vinavyomzunguka haviwaki kama ilivyokuwa nyuma.
"Tatizo lile
naona limekwisha, naishi kwa furaha sana kuliko siku ya nyuma sikuweza
kukaa na watu kwani kila mara moto ulikuwa unawaka tu," alisema mtoto
huyo.
Matatizo ya
mtoto huyo yalianza mwezi Agosti mwaka jana baada ya kusimamishwa shule
kutokana na kuwa na matatizo ya kukimbia huku akidai anaitwa na bibi
mmoja anayeishi kijijini hapo.
Ilipofika
Februari 9, hali ilianza kubadilika baada ya nguo zake alizokuwa
amezivaa kuanza kuwaka moto ghafla pamoja na vitu mbalimbali
vilivyokuwemo nyumbani kwao kuteketea kwa moto.
Tukio hilo
limethibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Muhingo Rweyemamu kwa
kueleza kabla ya kufikishwa kanisani hapo kwa maombezi, wazazi wa mtoto
huyo waliomba kibali cha kuwaita waganga wa jadi maarufu kama rambaramba
ili watoe kile kinachodaiwa kuwa ni moto wa uchawi unaomtesa mtoto
huyo.
Kwa watu
watakaojitokeza kumsaidia mtoto huyo watume msaada wao kwa kutumia simu
namba 0763818244 na 0715346562 au wafike kanisani hapo moja kwa moja.
إرسال تعليق