Neno la leo kutoka kwa mjengwa.

Ndugu zangu,


Kuna simulizi ya kwenye Biblia. Enzi za Mfalme Suleiman kuna watu waliolalamika sana, kuwa wanaishi kwenye manyanyasiko mno.



Kukawa na vijana waliokuwa na kiu ya kutaka mabadiliko ya uongozi wa mfalme. Walitaka watawaliwe na mfalme kijana.



Wazee walipoombwa ushauri wakatamka; kuwa vijana mara nyingi hupungukiwa na busara. Hivyo, si lazima mfalme awe kijana.


Vijana wale wakakaidi ushauri wa wazee. Wakampata Mfalme kijana. Naye alipokuwa madarakani, alitenda mara mbili ya dhambi alizotenda mtawala aliyetangulia.


 Mfano, kama mtawala aliyepita alitoa adhabu ya kuchapa kwa mjeledi, basi, mfalme kijana yeye alitaka atumie rungu. Hakukuwa na nafuu walioitarajia.


Ndugu zangu,



Juma la kwanza tu baada ya Bunge kuanza mwaka 2010, nikiwa njiani kutoka Singida nilisimama Dodoma. Hapo nilipata bahati ya kukutana na mmoja wa Wabunge vijana kutoka kambi ya upinzani.



Tulikaa na kunywa chai pamoja.  Alinitaka pia ushauri katika kazi yake. Hakika,niliingiwa na matumaini makubwa juu ya fikra zake za kimaendeleo pale alipoanza mazungumzo. Mathalan, kati ya dhambi kadhaa zinazofanywa na wabunge alizoziona, akaniambia juu ya kustaajabishwa kwake na tabia ya Wabunge kufoji risiti za safari zao ili wapate fedha zaidi.



“ Yaani kaka Maggid, sikujua kuwa Wabunge hawa wanafanya mambo kama watoto wa shule.

Yaani Mbunge anahangaika kufoji risiti za mafuta na kudai kuwa ametokea mahali fulani kuja hapa Dodoma wakati sio!” Aliniambia kwa uchungu mbunge yule kijana.

Lakini, mashaka yakanijia pale nilipomwuliza;



“ Sasa ukitoka hapa Dodoma umejiandaa na kipi cha  kwenda kuwaambia wapiga kura wako kwenye mkutano wako wa kwanza wa hadhara baada ya kikao chako cha kwanza Bungeni?”


Mbunge yule kijana aliniangalia na kuniambia; “ Naenda kwanza Dar kuhangaikia  gari yangu mpya!”



Nikawa nimekatishwa tamaa na Mbunge yule kijana. Kwamba katika juma la kwanza tu la kukaa Bungeni, tayari ameanza kufikiria kuhangaikia masuala yake binafsi, na si masuala ya wananchi waliompigia kura!



Naambiwa, naye siku hizi anapomaliza  vikao vya kuongea hata na jamaa zake tu, haraka sana hukimbilia kutoa ‘ bahasha za nauli’.


Siku hizi mbunge yule kijana ana gari zaidi ya ile aliyokwenda kuichukua Dar. Amekuwa mbunge-mfanyabiashara.



Sifikirii tena kwenda kumpa ushauri mbunge yule kijana, maana, naweza kuambulia kudhalilishwa kwa kupewa ‘bahasha ya nauli’ ya kurudia nyumbani kwangu.



Naam, ni heri ya ndugu yangu John Komba, hata akisemwa kuwa anasinzia Bungeni, bado ana mchango kwa jamii; kwa nyimbo zake zenye kuburudisha na kuelimisha.


Ndio, nchi hii inahitaji mabadiliko ya kimsingi, lakini, ni vizuri kutambua, kuwa wengine tunaofikiri kuwa wanaweza kutusaidia katika kuyafikia mabadiliko hayo, hawana tofauti kabisa na  baadhi ya tunaofikiria hawatufai.



Na hutokea, kuwa dhambi wafanyayo, na watakayoifanya, yumkini yaweza kuwa  ni mara mbili ya inayofanywa na baadhi ya waliopo sasa.


Ni Neno La Leo.


Maggid Mjengwa,


Iringa.


0788 111 765

http://mjengwablog.co.tz

Post a Comment

أحدث أقدم