Qunuut kwa maelezo ya Fuqahaa (wanachuoni wa fiqh), ni du'aa inayosomwa
katika Swalah katika sehemu maalum wakati mtu anapokuwa amesimama baada
ya kurukuu (au kabla kwenye kauli nyingine). Na inatumika katika Swalah
ya witr kwenye raka'ah ya mwisho baada ya kurukuu kwa kauli yenye nguvu.
Waumini wa Kiislamu wakiwa katika du'aa ya Qunuut
Qunuut ni du'aa itumikayo wakati wa matatizo, majanga na maafa
yanapowafika Waislam. Na wakati huo ndipo du'aa hii huombwa na huwa
inaombwa katika kila Swalah na si Swalah ya alfajiri tu kama
ilivyozoeleka na baadhi ya watu kwa kutumia baadhi ya hadiyth ambazo
hazijasihi kuhusiana na Qunuut ya kudumu (katika Swalah ya Alfajir).
Du'aa hii si fardhi bali ni Mustahab, na Swalah ya mtu ni sahihi kabisa
hata kama hajasoma Qunuut, na wala usiposoma Qunuut huhitaji kufanya
sijdatus-sahw (sijida za kusahau) kama wanavyodhani wengine. Inapendezwa
kufanywa wakati ikifikia dharura kama tulivyotaja juu. Na vilevile
wakati mwingine wa kuisoma Qunuut ni wakati wa Swalah ya Witr.
Ni kinyume na Sunnah kuisoma Qunuut kwenye Swalah za asubuhi na kudumu
nayo kama inavyofanywa kwani hilo halijathibiti katika hadiyth sahihi
kutoka kwa Mtume (Swallah Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam).
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) alisoma du'aa hiyo wakati Maswahaba zake sabini wajuzi wa
Qur-aan walipouliwa kwenye sehemu iitwayo Bi-ir Ma'uunah na Makabila ya
Bani Sulaym ya Ri'il, Dhakwaan, Ussayah wakati alipowatuma kwenda
kuwafundisha dini yao. Aliisoma du'aa ya Qunuut kwa muda wa mwezi mzima
dhidi ya hao Wauaji. (Hadiyth ya Anas iliyopo kwenye Al Bukhaariy na Muslim).
Pia kwenye Hadiyth nyingine iliyopokelewa na
Abu Hurayrah, inaonyesha kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) aliwahi kuwaombea baadhi ya Maswahaba waliokuwa wamepotea kwa
maadui, na aliomba kiasi cha mwezi kisha akaacha, na Abu Hurayrah
alipomuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwanini
ameacha kuwaombea, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
akamjibu,''Je,huoni kuwa washarejea?" (Al Bukhaariy na Muslim)
Hivyo, inaonyesha kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) alisoma Qunuut hiyo ambayo inaitwa Qunuut an Nawaazil kwa muda
ambao yale aliyokuwa akiyaomba, yamejibiwa ndipo akaacha.
Vilevile imethibiti kuwa alikuwa akiwaombea wale waliokuwa dhaifu,
wananyanyaswa na maadui na kuwa chini ya wavamizi kama hali tuliyonayo
leo huko Iraq, Afghanistan, Palestina, Chechnya na kwengineko.
Imepokewa pia kuwa Abu Maalik Al-Ash'ariy alisema: "Nilimuuliza baba
yangu, 'Ee baba yangu, uliswali nyuma ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi
wa aalihi wa sallam) na nyuma ya Abu Bakr, 'Umar, 'Uthmaan na 'Aliy
(Radhiya Allaahu 'anhum ajma'iyn). Je, walikuwa wakisoma Qunuut katika
Swalah ya alfajiri?' Akajibu, Ee mwanangu, hili ni jambo jipya
lililozushwa,'" (Imesimuliwa na wapokezi wote (watano) isipokuwa Abu
Daawuud). Hakika muongozo mzuri na bora ni ule wa Muhammad (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
Na Qunuut inaposomwa, basi ni vizuri kusoma kwa ile shida inayoombewa
kwa wakati huo; kama ni njaa au udhaifu au manyanyaso n.k., iombwe
kutokana na masuala hayo, na si kusoma du'aa ile iliyozoeleka kwenye
Qunuut 'Allahumma ihdiyna fiyman hadayta, wa'afina fiyman 'afayta...'
Du'aa hii inawezwa kusomwa kwenye Qunuut ya witr na si kwenye Qunuut ya
Nawaazil.
Na endapo utaswali nyuma ya Imaam anayesoma Qunuut katika Swalah ya
Alfajiri, basi unatakiwa umfuate na Swalah yako ni sahihi, kwani
kumfuata Imam ni wajibu, na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) kasema:
"Imaam amechaguliwa ili afuatwe" na akasema: "Msitofautiane na Maimaam wenu",
na pia katika Swahiyh Al-Bukhaariy amesema:
"Wanawaongoza katika Swalah; ikiwa wamepatia, (ujira) ni wenu na wao, na wakikosea, (ujira) ni wenu na (dhambi) ni zao."
Wa Allaahu A'alam
Chanzo; Alhidaaya.com
Post a Comment