Swali: Kusoma Du'aa Ya Qunuut Katika Swalah Ya Alfajiri Ni Sunnah..?


Qunuut kwa maelezo ya Fuqahaa (wanachuoni wa fiqh), ni du'aa inayosomwa katika Swalah katika sehemu maalum wakati mtu anapokuwa amesimama baada ya kurukuu (au kabla kwenye kauli nyingine). Na inatumika katika Swalah ya witr kwenye raka'ah ya mwisho baada ya kurukuu kwa kauli yenye nguvu.

Waumini wa Kiislamu wakiwa katika du'aa ya Qunuut

Qunuut ni du'aa itumikayo wakati wa matatizo, majanga na maafa yanapowafika Waislam. Na wakati huo ndipo du'aa hii huombwa na huwa inaombwa katika kila Swalah na si Swalah ya alfajiri tu kama ilivyozoeleka na baadhi ya watu kwa kutumia baadhi ya hadiyth ambazo hazijasihi kuhusiana na Qunuut ya kudumu (katika Swalah ya Alfajir). Du'aa hii si fardhi bali ni Mustahab, na Swalah ya mtu ni sahihi kabisa hata kama hajasoma Qunuut, na wala usiposoma Qunuut huhitaji kufanya sijdatus-sahw (sijida za kusahau) kama wanavyodhani wengine. Inapendezwa kufanywa wakati ikifikia dharura kama tulivyotaja juu. Na vilevile wakati mwingine wa kuisoma Qunuut ni wakati wa Swalah ya Witr.

Ni kinyume na Sunnah kuisoma Qunuut kwenye Swalah za asubuhi na kudumu nayo kama inavyofanywa kwani hilo halijathibiti katika hadiyth sahihi kutoka kwa Mtume (Swallah Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam).

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisoma du'aa hiyo wakati Maswahaba zake sabini wajuzi wa Qur-aan walipouliwa kwenye sehemu iitwayo Bi-ir Ma'uunah na Makabila ya Bani Sulaym ya Ri'il, Dhakwaan, Ussayah wakati alipowatuma kwenda kuwafundisha dini yao. Aliisoma du'aa ya Qunuut kwa muda wa mwezi mzima dhidi ya hao Wauaji. (Hadiyth ya Anas iliyopo kwenye Al Bukhaariy na Muslim).


Pia kwenye Hadiyth nyingine iliyopokelewa na Abu Hurayrah, inaonyesha kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwahi kuwaombea baadhi ya Maswahaba waliokuwa wamepotea kwa maadui, na aliomba kiasi cha mwezi kisha akaacha, na Abu Hurayrah alipomuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwanini ameacha kuwaombea, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamjibu,''Je,huoni kuwa washarejea?" (Al Bukhaariy na Muslim)

Hivyo, inaonyesha kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisoma Qunuut hiyo ambayo inaitwa Qunuut an Nawaazil kwa muda ambao yale aliyokuwa akiyaomba, yamejibiwa ndipo akaacha.

Vilevile imethibiti kuwa alikuwa akiwaombea wale waliokuwa dhaifu, wananyanyaswa na maadui na kuwa chini ya wavamizi kama hali tuliyonayo leo huko Iraq, Afghanistan, Palestina, Chechnya na kwengineko.

Imepokewa pia kuwa Abu Maalik Al-Ash'ariy alisema: "Nilimuuliza baba yangu, 'Ee baba yangu, uliswali nyuma ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na nyuma ya Abu Bakr, 'Umar, 'Uthmaan na 'Aliy (Radhiya Allaahu 'anhum ajma'iyn). Je, walikuwa wakisoma Qunuut katika Swalah ya alfajiri?' Akajibu, Ee mwanangu, hili ni jambo jipya lililozushwa,'" (Imesimuliwa na wapokezi wote (watano) isipokuwa Abu Daawuud). Hakika muongozo mzuri na bora ni ule wa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

Na Qunuut inaposomwa, basi ni vizuri kusoma kwa ile shida inayoombewa kwa wakati huo; kama ni njaa au udhaifu au manyanyaso n.k., iombwe kutokana na masuala hayo, na si kusoma du'aa ile iliyozoeleka kwenye Qunuut 'Allahumma ihdiyna fiyman hadayta, wa'afina fiyman 'afayta...' Du'aa hii inawezwa kusomwa kwenye Qunuut ya witr na si kwenye Qunuut ya Nawaazil.

Na endapo utaswali nyuma ya Imaam anayesoma Qunuut katika Swalah ya Alfajiri, basi unatakiwa umfuate na Swalah yako ni sahihi, kwani kumfuata Imam ni wajibu, na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:

"Imaam amechaguliwa ili afuatwe" na akasema: "Msitofautiane na Maimaam wenu",

na pia katika Swahiyh Al-Bukhaariy amesema:

"Wanawaongoza katika Swalah; ikiwa wamepatia, (ujira) ni wenu na wao, na wakikosea, (ujira) ni wenu na (dhambi) ni zao."

Wa Allaahu A'alam

Chanzo; Alhidaaya.com

Post a Comment

أحدث أقدم