Mhe.
Sophia Simba ( Mb) akichangia ajenda kuhusu Utokomezaji na Umalizaji wa
Unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto wa kike wakati wa mkutano wa 57
wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Wanawake (CSW). Mkutano huu wa
wiki mbili unaendelea hapa Umoja wa Mataifa na Mhe. Simba anaongoza
ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aliyeketi nyuma ya Mhe.
Waziri ni Naibu Mwakilishi wa Kudumu, Balozi Ramadhan Mwinyi
Makatibu
Wakuu, Kijakazi Mtengwa ( Tanzania Bara) na Fatma Gharib Bilal (
Zanzibar ) wakifuatilia majadiliano kuhusu utokomezaji na umalizaji
unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto wa kike.
Mhe.
Sophia Simba akishiriki majadiliano ya mada iliyohusu umuhimu wa Takwimu
katika kushughulikia unyanyasaji wa kijinsia, Waziri alikuwa mmoja wa
wazungumzaji wakuu katika mjadala huo. mjadala ulikuwa umeandaliwa na
UNFPA, ikiwa ni sehemu ya mkutano wa 57 wa CSW,kulia kwa Waziri ni Naibu
Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA, Bi Anne -Brigitte Albractsen.
Kutokana
na wingi wa washiriki wa majadiliano kuhusu umuhimu wa Takwimu katika
kushughulikia unyanyasaji kuwa wengi kupitia uwezo wa ukumbi, baadhi ya
washiriki walilazimika kukaa chini kama inavyoonekana katika picha
Na Mwandishi Maalum
Waziri
wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mhe. Sophia Simba ( Mb)
amesisitiza kwamba, serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inatambua wazi kwamba unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto wa kike ni
ukiukwaji wa haki za binadamu na kwamba vitendo hivyo vina madhara
makubwa.
Kwa kulitambua hilo, Waziri anasema
serikali zote mbili ile ya Tanzania Bara na Visiwani, zimekuwa
zikichukua hatua pamoja na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuhakikisha
kwamba unyanyasaji dhidi ya kundi hilo la jamii wakiwamo watu wenye
ulemavu wa ngozi ( albino) unapunguzwa na hatimaye kutokomezwa.
Waziri ameyasema hayo jana alhamisi,
wakati alipokuwa akitoa mchango wake wakati wa majadiliano yaliyohusu
ajenda ya utokomezaji na upunguzaji unyanyasaji dhidi ya wanawake na
watoto wa kike.
Mhe.Sophia
Simba anaongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika
Mkutano wa 57 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya wanawake (
CSW), ambao umeanza siku ya jumatatu hapa Makao Makuu ya Umoja wa
Mataifa, New York , Marekani.
Amezitaja
hatua hizo kuwa ni pamoja na tatizo la unyanyasaji kuainishwa katika
Mpango wa Kitaifa wa Kupunguza Umaskini ambapo vitendo hivyo vinaelezwa
kama kiashiria cha umaskini.
Aidha
akaeleza pia kwamba mipango mbalimbali ya utekelezaji katika ngazi ya
kitaifa na kwa kushirikiana na sekta mtambuka imeundwa kwa pande zote
mbili za Muungano.
Vile
vile akabainisha kwamba, taasisi za kisheria kama vile Chama cha Majaji
wanawake, zimekuwa zikitoa mchango mkubwa katika kuwasaidia wanawake
fursa ya kupata haki.
Kama
hiyo haitoshi, Waziri Sophia Simba amesema, kwa upande wa vyombo vya
ulinzi na usalama kumeanzishwa pia mtandao wa Polisi wanawake lengo
likiwa ni kuwawezesha na kuwapa nyenzo za kushughulikia kikamilifu
matukio ya unyanyasaji wa kijinsia.
Pamoja
na juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali na wadau wengine, Waziri
Sophia Simba hakusita pia kubainisha baadhi ya changamoto zinazokwamisha
juhudi hizo.
Amezitaja
baadhi ya changamoto kuwa ni pamoja kutokuwapo kwa takwimu za uhakika
kuhusu vitendo vya unyanyasaji, takwimu ambazo zingeweza kuchangia
katika uaandaaji wa sera na mipango mbalimbali yenye kulenga kusukuma
maendeleo ya wanawake.
Akataja
changamoto nyingine kuwa ni ile ya kubadili mtizamo wa jamii kuhusu
suala zima la unyanyasaji wa jinsia na kwamba tatizo hilo linahitaji
kuendelea kufanyiwa kazi.
إرسال تعليق