KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida wananchi wa kijiji na kata ya Mkwajuni Wilaya ya Chunya Mkoani hapa wamemzika Mwanakijiji mwenzao akiwa hai wakimtuhumu kusababisha kifo cha Mkazi mmoja kijijini hapo.
Tukio hilo la kusikitisha limetokea Apri 26 mwaka huu majira ya Saa Nane Mchana katika Kitongoji cha Maweni Makaburini baada ya Mhanga aliyefahamika kwa jina la Victory Mwachirui(68) kuhudhuria mazishi ya Pita Barton(28)aliyefariki baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, Thobias Ismail amesema marehemu alipatwa na umauti akiwa anapatiwa matibabu kwa mganga wa jadi ambaye jina lake halikuweza kujulikana maramoja.
Amesema wakati taratibu za mazishi zikiendelea Ndugu wa marehemu walidai kuwa kifo cha Marehemu kilisababishwa na Mwachirui ambaye ni Katekista mstaafu kwa imani za kishirikina.
Ameongeza kuwa wakati kaburi likichimbwa kwa ajili ya kumzika marehemu ndipo vijana waliokuwa wakichimba waliagiza Wazee wa Mila wafike makaburini kwa ajili ya kuangalia utaratibu wa mazishi na kukagua ukubwa wa Kaburi ambalo lilikuwa limekwisha chimbwa.
Kutokana na mwito huo walifika wazee wanne akiwemo Mzee Mwachirui ambaye walimsisitiza kusogea jirani na kaburi ambapo baada ya kusogea alipigwa na Sururu kichwani na kuangukia kaburini huku akisindikizwa na marungu.
Baada ya Mzee huyo kupoteza fahamu Vijana hao walianza kutandika fito ndani ya kaburi kisha kufukia kwa udongo kiasi kwa lengo la kutenganisha na Mwili wa Marehemu Pita uliokuwa kwenye jeneza baada ya kuwazika kwenye kaburi moja.
Baada ya kukamilika kwa zoezi la mazishi kundi la vijana lilielekea hadi nyumbani kwa Mzee aliyezikwa akiwa hai na kuiteketeza nyumba yake huku wakiapa kutotoa siri wakidai Siri ya Jeshi.
Hata hivyo baadhi ya wananchi walitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Kijiji hicho aliyefahamika kwa jina la Credo Kayanza ambaye pia alitoa taarifa kwa Diwani wa Kata hiyo Chesco Ngairo ambao kwa pamoja walitoa taarifa Jeshi la Polisi ambao baada ya taarifa hiyo walifika eneo la tukio huku wakidhani lililotokea ni kuchomwa kwa nyumba pekee.
Jeshi la Polisi baada ya kufanya upelelezi na kubaini kitendo hicho waliwaamuru baadhi ya Vijana kufukua kaburi hilo zoezi ambalo lilifanyika baada ya Vijana hao kulipwa.
Baada ya kufukuliwa kwa kaburi hilo Mwili wa Marehemu Mzee Mwachirui ulichukuliwa na kupelekwa katika Hospitali ya Misheni ya Mkwajuni kwa ajili ya Uchunguzi huku Mwili wa Pita ukizikwa upya palepale.
Baada ya kukamilika kwa uchunguzi mwili wa marehemu ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi ambapo Marehemu alizikwa katika eneo tofauti na alipokuwa amefukiwa awali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo pia ametoa wito na kuwaasa wananchi na jamii kuacha tabia ya kuamini mambo ya ushirikina na uchawi kwa madai kuwa hauna faida kwao bali huchochea migogoro katika jamii zao.
Aidha ameongeza kuwa wakumbuke kitendo cha kujichukulia sheria mkononi ni kosa kisheria ambapo pia amewaomba wenye taarifa za walipo waliohusika na mauaji hayo kuzifikisha polisi haraka ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao ingawa hakuna aliyekamatwa kuhusika na tukio hilo.
Picha na E. Kamanga wa Mbeya yetu
|
إرسال تعليق