Mshukiwa mmoja wa mashambulizi ya Boston auawa kwa kupigwa risasi

chechnya
Na Victor Melkizedeck Abuso

Polisi mjini Boston nchini Marekani wanasema kuwa mmoja wa washukiwa waliotekeleza mashambulizi ya bomu wakati wa mashindano ya riadha siku ya Jumatatu na kusababisha vifo vya watu watatu na wengine 170 kujeruhiwa ameuawa kwa kupigwa risasi.

Hata hivyo, polisi wanasisitiza kuwa mshukiwa mwingine bado anasakwa baada ya kukabiliana na polisi kwa kufwatuliana risasi.

Mshukiwa huyo amepoteza maisha akiwa kizuizini baada ya kupigwa risasi na badaye kuzuiliwa mjini Boston.

Awali, maafisa wa Ujasusi wa FBI nchini Marekani walitoa picha za washukiwa wawili wanaotuhumiwa kutekeleza mashambulizi hayo wawili .

Picha za washukiwa hao zilitolewa kupitia kanda za usalama za CCTV zikionesha wanaume wawili wakiwa wamevaa nguo nyeusi, kofia za mchezo wa baseball na wakiwa na mifuko migongoni.

Richard DesLauriers mmoja wa maafisa wa FBI amesema kuwa washukiwa hao ni hatari sana na wananchi wa Marekani hawastahili kuwakaribia.

Mepema juma hili, FBI ilitoa picha za kifaa cha jikoni kilichotumiwa kutekeleza mashambulizi hayo pamoja na washukiwa hao wakitupa mifuko yao katika eneo la kumalizia mbio hizo ndefu.

Mashambulizi hayo yalisababisha vifo vya watu watatu na kuwajeruhi wengine 170 wakiwemo watoto watatu ambao madaktari wanasema hali yao bado haijatengemaa.

Rais Barrack Obama amesema kuwa waliohusika na mashambulizi hayo watachukuliwa hatua kali za kisheria huku akiwahakikishia familia za walioathirika kuwa serikali iko pamoja nao wakati huu mgumu.

Siku ya Alhamisi rais Obama alizuru Boston na kuhudhuria ibada ya wafu ya watu watatu waliopoteza maisha yao na kuwaombea pia wale wanaopata matibabu Hospitalini.

Ibada hiyo pia ilihudhuria na Mitt Romney aliyekuwa mgombea urais nchini humo wakati wa uchaguzi Mkuu mwaka uliopita.

Via kiswahili.rfi.fr

Post a Comment

Previous Post Next Post