Shambulio la bomu latikisa ubalozi wa Ufaransa nchini Libya

French embassy after car bomb blast, in Tripoli, Libya
Shambulio lililotekelezwa katika ubalozi wa Ufaransa nchini Libya, 23 April 2013

Mlipuko wa bomu umetokea mapema jumanne hii katika ubalozi wa Ufaransa mjini Tripoli nchini Libya. Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, tukio hilo limesababisha uharibifu mkubwa wa majengo ya ubalozi huo na kuwajeruhi walinzi wawili waliokuwapo katika eneo hilo.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande amesema mamlaka za nchini Libya inapaswa kueleza kwa kina kuhusu shambulio hilo na kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria. Wizara ya mambo ya nje ya Libya imelaani shambulizi hilo na kuliita ni la kigaidi.

Waziri wa mambo ya nje wa Libya Mohammed Abdel Aziz ameiambia AFP kuwa serikali yake inalaani shambulio hilo ambalo limetekelezwa katika ofisi za Taifa ambalo liliisaidia nchi hiyo kufanikisha harakati za kuangushwa kwa Rais wa zamani wa nchi hiyo Moamer Ghaddafi.

Shambulio la jumanne hii ni la kwanza kutekelezwa katika ofisi za kigeni za nchini humo kwa mwaka huu, tukio la mwisho ni lile la kushambuliwa kwa ubalozi wa Marekani mjini Benghazi mwezi septemba mwaka jana ambalo lilisababisha vifo vya raia wanne wa Marekani akiwamo aliyekuwa balozi wa Marekani katika nchi hiyo Christopher Stevens.

Tangu kuangushwa kwa utawala wa Ghaddafi nchi hiyo imeendelea kukumbwa matukio ya kukosekana kwa usalama suala ambalo limechangia raia wengi wa kigeni kuondoka katika nchi hiyo. Via kiswahili.rfi.fr
 

Post a Comment

أحدث أقدم