DK Bilal awataka wanasayansi kujikita zaidi katika utafit

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Gharib Mohamed Bilal, akizungumza katika uzinduzi wa mkutano wa kwanza wa utafiti wa wanasayansi katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi cha Muhimbili (Muhas) na maadhimisho ya miaka 50 ya chuo hicho jana, jijini Dar es salaam. Picha na Aika Kimaro. 
Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Gharib Mohamed Bilal, amewataka wanasayansi wa sekta ya afya nchini na barani Afrika kujikita katika kufanya utafiti, ili kutatua matatizo yanayoikabili sekta hiyo,.
Akizungumza katika uzinduzi wa mkutano wa kwanza wa Wanasayansi wa Chuo Cha Afya cha Muhimbili (Muhas), Dk Bilal alisema maendeleo ya nchi yanatokana na ustawi mzuri wa sekta ya afya.
Alisema tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa ufuatiliaji mbovu wa masuala ya afya, ndiyo chanzo cha umaskini wa nchi nyingi.

“Kuna umuhimu wa kuingia kwa undani katika utafiti ili kujua ufumbuzi wa baadhi ya magonjwa na hata kupata utatuzi na jinsi ya kuyazuia,”alisema Dk Bilal.
Alisema tafiti zinahitajika mno katika jitihada za kutafuta ufumbuzi wa matatizo.
Makamu wa Rais alisema kwa sasa kiwango cha tafiti katika chuo hicho, kimeongezeka kutoka tafiti 10 mwaka 1999 hadi kufikia 87 mwaka 2012/2013.
Alisema mchango wa Muhas unatambulika kwa sababu ni moja ya vyuo 2,000 bora duniani .
Alisema kiwango cha elimu cha chuo hicho kwa kuangalia ubora na elimu, ni cha kujivunia.
Dk Bilal alisema matokeo ya chuo hicho kwa mwaka 2011 yalikifanya kushika nafasi ya 1716 duniani na nafasi ya 42 kwa nchi za Afrika.

“Katika ushindani wa vyuo vya Afrika Mashariki, kilishika nafasi ya nne na namba mbili kwa vyuo vya hapa nchini,” alisema Makamu wa Rais.
Aliongeza kuwa kwa sasa tafiti za chuo hicho zimetoa kipaumbele zaidi katika maeneo ya ugonjwa wa Ukimwi kifua kikuu, malaria, ukuaji wa watoto, magonjwa yasiyoambukiza, majeruhi na mengineyo.
Alisema zaidi ya asilimia 95 ya wakufunzi wa Muhas wenye Shahada ya Uzamivu (Phd) wameshapatiwa mafunzo na kuwezeshwa katika ufanyaji wa miradi ya tafiti mbalimbali nchini.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Ephata Kaaya, alisema mikutano ya tafiti na ufumbuzi wa matatizo ndani ya sekta ya afya, itasaidia katika kupunguza umaskini nchini.
Alisema Serikali imefanikiwa kutengeneza mazingira mazuri ya tafiti za afya na sekta nyingione.
Mkutano huo wa kwanza wa wanasayansi unafanyika kwa muda wa siku nne na kauli mbiu yake ni “Tafiti za Afya Punguza Umaskini.”

Post a Comment

Previous Post Next Post