WABUNGE CCM WAWAKATAA
UPEPO mbaya ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) unazidi kuvuma, safari
hii wabunge wake wakimtaka Rais Jakaya Kikwete kuwafukuza kazi mawaziri
watatu.
Mawaziri wanaotakiwa kung’olewa ni Dk. Shukuru Kawambwa (Elimu na
Mafunzo ya Ufundi), Dk. Mathayo David Mathayo (Mifugo na Maendeleo ya
Uvuvi) na Dk. Fenella Mukangara (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo).
Kama Rais Kikwete atakubali kuwaondoa madarakani mawaziri hao, hii
itakuwa mara ya pili kwake kufanya hivyo. Mara ya kwanza ilikuwa Mei
mwaka jana.
Mwaka jana Rais Kikwete aliamua kuwaengua madarakani baadhi ya mawaziri
waliokuwa wakiandamwa kwa tuhuma mbalimbali, ikiwemo uwajibikaji mbovu.
Miongoni mwa walioenguliwa mwaka jana ni Dk. Haji Mponda aliyekuwa
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mustafa Mkulo (Waziri wa Fedha),
William Ngeleja (Nishati na Madini na Ezekiel Maige (Maliasili na
Utalii).
Msimamo huo wa wabunge wameutoa jana katika kikao baina yao na Rais
Kikwete kilichokuwa kikitathimini mwenendo wa chama na utendaji wa
wabunge.
Chanzo chetu ndani ya kikao hicho kilieleza kuwa baada ya Rais Kikwete
kutoa hotuba ya ufunguzi, baadhi ya wabunge walianza kuchangia, huku
wengine wakishutumiana kwa kuvujisha siri za vikao nje kwa waandishi wa
habari.
Wabunge hao walidai kuwa mawaziri hao watatu wamekuwa mzigo kwa Serikali ya CCM kutokana na utendaji wao kutokuwa wa kuridhisha.
Walisema matunda ya uwepo wa mawaziri hao kwenye wizara husika hayaonekeni, hivyo kumtaka Rais Kikwete awang’oe.
Waziri Kawambwa analaumiwa kwa kuzembea kwenye sekta ya elimu ambayo
inazidi kushuka kiasi cha kuifanya serikali ifute matokeo ya kidato cha
nne ya mwaka jana.
Walisema kufutwa kwa matokeo hayo ambayo asilimia 60 ya waliofanya
mtihani walipata daraja sifuri, kunadhihirisha uwezo mdogo wa Dk.
Kawambwa.
Wakati Kawambwa akibanwa kwa hilo, wenzake Mathayo na Mukangara
wanadaiwa kuwepo wizarani bila kuonesha ufanisi wowote.Wabunge hao
walidai kuwa Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi anayoiongoza Dk.
Mathayo ni nyeti na ilipaswa kuwa ya pili katika kuchangia pato la taifa
baada ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Walimshambulia Dk. Mathayo kuwa mzigo kwa wizara hiyo kwani alipokuwepo
Dk. Magufuli (Waziri wa Ujenzi) ilikuwa ikifanya vizuri tofauti na hivi
sasa.
“Tusioneane aibu, huyu Mathayo ameshindwa kazi, mwenyekiti muondoe kabla mambo hayajazidi kuwa mabaya,” alisema mbunge mmoja.
JK abariki mchakato wa urais
Mapema katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao hicho, Rais Kikwete
aliruhusu makundi ya wana-CCM wanaotaka kuwania urais 2015 kuendelea na
mchakato wa kuweka mikakati yao ya kampeni bila chuki.
Kwa mujibu wa chanzo chetu katika kikao hicho ambacho waandishi
hawakuruhusiwa kuingia, lengo kubwa lilikuwa ni kujadili masuala
mbalimbali ya kitaifa ikiwemo utekelezaji wa ilani ya uchaguzi katika
majimbo ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na ahadi za rais.
Rais Kikwete aliwataka wana-CCM wenye nia ya kugombea urais kuendelea na
mikakati yao kwa ustaarabu na kuepusha uadui kutokana na wapambe wao
kuwa na kambi zaidi ya moja.
“Tuangalie makundi ya urais 2015 yasishambuliane kwa kuvunja chama,
wenye nia hiyo ya kugombea waendelee na mikakati yao na si kujenga chuki
kwa makundi mengine.
“Mkumbuke kuwa kambi hizo za urais zinatakiwa kujitizama na wafuasi wao maana wafuasi wengi si wa kuaminika,” alisema Kikwete.
Rais Kikwete aliwafananisha baadhi ya wapambe na matango pori yanayoota
popote, ambapo alisema wamekuwa na tabia ya kutoa maneno huku na
kupeleka upande wa pili.
Tanzania Daima ilidokezwa kuwa Kikwete alikuwa na ajenda nne ambazo ni
urais 2015, kuwahimiza wabunge kutembelea majimbo yao ya uchaguzi,
kurudi majimboni kwao kusimamia ahadi zao, chama na zile za viongozi wa
kitaifa akiwemo yeye na kuisimamia serikali na kuikosoa bila kuibomoa.
Kwamba Kikwete aliwataka wabunge hao kutumia kauli za staha wanapoikosoa serikali kama ambavyo baadhi wamekuwa wakifanya.
“Mnatakiwa kuisimamia serikali na kuikosoa bila kuibomoa, lakini kuna
baadhi yenu mmekuwa mnaibomoa serikali kwa jinsi mnavyochangia huko
bungeni, hilo si jambo jema hata kidogo, waachieni wale wenzenu,”
alisema.
Katika hilo, wabunge walionya tabia ya baadhi ya mawaziri wanavyohusiana
na wabunge na wanavyoonekana kwa wananchi, lakini wakaitaka serikali
kutimiza wajibu wake ipasavyo kwa kutoa fedha za bajeti kama
zinavyopitishwa na Bunge.
Pia ubadhirifu unaofanywa kwenye halmashauri nchini, utendaji mbovu wa
baadhi ya wakuu wa wilaya na mikoa nchini, hivyo wakamtaka rais kukunjua
makucha yake kuondokana na uozo huo.
Kuhusu kutembelea majimbo, rais alisema kuwa baadhi ya wabunge
wameyatelekeza kwa kutorudi kusikiliza kero za wananchi na kutimiza
ahadi zao.
Aliwaonya kuwa kwa tabia hiyo wala wasije kuwaonea donge wale wanachama wengine watakaochaguliwa kuwa wabunge badala yao.
Lugola, Filikunjombe, Mpina wakaangwa
Baada ya mapumziko ya mchana, kikao hicho kiliendelea kwa wabunge kutoa
madukuduku yao ambapo chanzo chetu kinasema kuwa wabunge watatu
walishambuliwa kwa tabia yao ya kuikosoa serikali kwa kauli nzito.
Wabunge hao ni Kangi Lugola (Mwibara), Deo Filikunjombe (Ludewa) na
Luhaga Mpina wa Kisesa ambao hata hivyo wote hawakuhudhuria kikao hicho.
Lugola amekuwa mwiba mkali wa kuwashambulia mawaziri wa serikali
kutokana na utendaji wao kutoridhisha ambapo hivi karibuni wakati
akichangia hotuba ya bajeti ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala
Bora), alitishia kuwataja mawaziri na watendaji wanojihusisha na rushwa
pamoja na biashara ya dawa za kulevya.
Filikunjombe naye amekuwa akipinga kuunga mkono hoja za serikali huku
akitumia maneno makali kama vile ‘serikali kuvaa miwani ya mbao’,
kutokuwa sikivu na mengine kama hayo ambayo inaelezwa kuwa hata Rais
Kikwete jana aliyatolea mfano.
Chanzo chetu kilieleza kuwa aliyeibua sakata hilo ni mbunge mmoja wa
Tabora, akidai wenzao hao wamekuwa na tabia isiyokoma, na hivyo
kupendekeza kuwa kama wanataka ni heri wakahamia upinzani kuliko
kuendelea kuivua nguo Serikali ya CCM.
Hadi tunakwenda mitamboni jana, kikao hicho kilikuwa kikiendelea na kwa
mujibu wa ofisa mmoja wa chama, walitarajia kuwa kingemalizika usiku wa
manane.
Chanzo: Tanzania Daima
إرسال تعليق